Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege mkoa wa Mtwara, Daimon Mwakosya, akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, kuhusu uwanja huo kuvamiwa na wananchi kutokana na kukosa uzio, alipofika uwanjani hapo kujionea maendeleo yake.
Muonekano wa eneo ambapo bomba la gesi limepita ikiwa ni ndani ya eneo la Uwanja wa Ndege wa Mtwara.
Muonekano wa nyumba 5 kati ya 55 zilizovamia eneo la Uwanja wa Ndege wa Mtwara. Uwanja huo ni moja ya viwanja vya ndege 11 ambavyo Serikali imepanga kuvifanyia maboresho.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akitoka kukagua kivuko cha MV. Kilambo kinachotoa huduma kati ya kijiji cha Kilambo, mkoani Mtwara na Namoto, Msumbiji.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akikagua moja ya maboya kwa ajili ya usalama kwa watumiaji wa kivuko cha MV. Kilambo, kinachotoa huduma kati ya kijiji cha Kilambo na Namoto – Msumbiji. wakati alipofanya ziara yake mkoani Mtwara.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akishiriki katika zoezi la uchanganyaji wa zege katika ujenzi wa barabara ya Tangazo-Kilambo yenye urefu wa KM 9.3, Mkoani Mtwara.
Naibu Waziri wa ujenzi, Elias Kwandikwa, ameiagiza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA) na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), kulihamisha bomba la gesi lililopitishwa katika maeneo ya Uwanja wa Ndege wa Mtwara kabla ya bomba hilo halijaleta madhara kwa watumiaji wa Uwanja huo.
Akizungumza mkoani Mtwara, mara baada ya kukagua uwanja huo, ikiwa ni siku kadhaa baada ya kutokea kwa tukio la ajali ya bomba la gesi katika maeneo ya Buguruni kwa Mnyamani mkoani Dar es salaam na kusababisha madhara kwa wananchi, Naibu Waziri huyo amesema kuwa uwepo wa bomba hilo katika uwanja huo si salama na huenda ikapelekea watoaji huduma za usafiri wa anga kusitisha au kutokuleta kabisa huduma zao kutokana na hofu, hali itakayopelekea Serikali kukosa mapato.
“TAA, TPDC na wataalam wa Wizara hakikisheni mnafanya kikao kuona namna ya kulihamisha bomba hili kwani jambo hili si salama na pia baadhi ya mashirika ya ndege ya kimataifa yakibaini kama kuna uwepo wa bomba la gesi katika uwanja huu wanaweza kusitisha huduma zao”, amesema Naibu Waziri Kwandikwa.
Ametoa rai kwa watendaji wa Taasisi mbalimbali za Serikali kutochukua maamuzi ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali kabla ya kushirikisha uongozi wa wilaya au mkoa kwa pamoja ili kupata ushauri wa maeneo ambayo yanafaa kwa ujenzi wa miundombinu hiyo.
Aidha, Naibu Waziri huyo amewaagiza wamiliki wa nyumba takriban 60 waliojenga katika eneo la uwanja huo kuondoka mara moja kabla Serikali haijawachukulia sheria kwa kosa la kuvamia uwanja huo.
Amewaonya wataalam waliopo kwenye Halmashauri hapa nchini upande wa ardhi kutokugawa viwanja kwa wananchi hususan katika maeneo ambayo si sahihi kama vile ya uwanja wa ndege kwani hali hii hupelekea ucheleweshaji wa maendeleo.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Kwandikwa amekagua kivuko cha MV Kilambo kinachotoa huduma zake katika mto Ruvuma kati ya Tanzania na Msumbiji pamoja na kivuko cha MV Mafanikio kinachotoa huduma zake kati ya Msemo na Msanga Mkuu na kuwataka wasimamizi wa vivuko hivyo kuhakikisha wanaboresha huduma pamoja na usalama wa vivuko hivyo kwa kuhakikisha kunakuwa na vifaa vya kutosha vya uokoaji.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Uwanja huo, Bw. Daimon Mwakosya, ametaja changamoto walizonazo ikiwa ni pamoja na mgogoro wa mpaka kati ya uwanja wa ndege na kijiji jirani cha Mangamba na uwanja kukosa uzio wa usalama.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Bw. Evod Mmanda, ameipongeza Serikali kwa kuchukua jitihada za dhati kwa kutatua kero mbalimbali za wananchi na hivyo kumuomba Naibu Waziri huyo kuliangalia suala la upitishwaji wa bomba la gesi katika uwanja huo kwa jicho la pekee.
Naibu Waziri Kwandikwa ameanza ziara ya kikazi katika mkoa wa Mtwara ambapo pamoja na mambo mengine amekagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na wizara yake kujionea maendeleo yake.