MAADHIMISHO ya Siku ya Kiswahili Duniani (MASIKIDU), yalifanyika Julai 7, 2024 nchini Tanzania, Afrika Mashariki, Afrika na duniani kote ambako lugha ya Kiswahili inazungumzwa.

Lengo la maadhimisho haya ni kuitikia mwito wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) la kuitangaza Julai 7, kila mwaka kuwa Siku ya Kiswahili Duniani.

Uamuzi huo ulitangazwa Novemba 2021, katika Mkutano wa 41 wa Nchi Wanachama wa Shirika hilo uliofanyika jijini Paris, Ufaransa. Maadhimisho ya kwanza yalifanyika Julai 7, 2022 na ya pili Julai 7, 2023.

Hivyo, maadhimisho haya ni ya tatu kufanyika tangu kutangazwa kwa uamuzi huo. Aidha, maadhimisho ya mwaka huu yamefanyika baada ya Julai 7 ya kila mwaka kutambuliwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuwa Siku ya Kiswahili Kimataifa Julai 1, 2024.

Uamuzi huo ulifanywa katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa nchini Marekani. Nchini Tanzania Masikidu yalianza kwa Mbio za Masafa za Kiswahili Msimu wa Pili zilizofanyika jijini Arusha. Mbio hizo ziliandaliwa na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) kwa kushirikiana na Kampuni ya African Sports Agency (ASA).

Uzinduzi wa mbio hizo ulifanywa Juni 26, 2024 na Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha, Maximilian Iraghe katika Viwanja vya Makumbusho ya Azimio la Arusha. Juni 29, 2024 ilikuwa siku rasmi ya kuanza kwa mbio hizo.

Mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro aliyewaongoza wakimbiaji katika mbio hizo. Mbio za Masafa za Kiswahili kwa mwaka 2024 ziliwahusisha washiriki zaidi ya 600 kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Aidha, katika kuelekea kilele cha Masikidu kuliandaliwa Mjadala wa Kitaaluma uliofanyika Julai 3, 2024 katika Maktaba Mpya, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Mjadala huo uliandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kupitia Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI), Bakita na Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA).

Malengo ya kuwapo kwa mjadala huo yalikuwa kuonesha kukua na kuenea kwa lugha ya Kiswahili. Kulikuwa na kushirikishana taarifa zinazohusiana na ufundishaji na maendeleo kwa ujumla ya lugha ya Kiswahili katika nchi za Ufaransa,

Urusi, Italia, Misri, Austria, Ghana, Burundi, Zimbabwe na Uganda. Pia, Programu ya Kalam Salaam iliandaliwa na kufanyika Julai 4, 2024 katika Kituo cha Sanaa na Utamaduni cha Alliance Franaise. Programu hiyo iliandaliwa na Kampuni ya uchapishaji ya Mkuki na Nyota na Bakita, na ilidhaminiwa na Ubalozi wa Ufaransa kupitia Kituo cha Sanaa na Utamaduni cha Alliance Franaise.

Matukio katika Kalam Salaam yalihusisha burudani, filamu ya Vuta N’Kuvute, mjadala kuhusu Kiswahili na fursa za maendeleo duniani na maswali na majibu. Washiriki waliojibu maswali kwa usahihi walipewa zawadi za vitabu. Vilevile, katika kuelekea kilele cha Masikidu Julai 5, 2024 kulikuwa na matembezi  ya wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo vya Dar es Salaam.

Washiriki wengine walikuwa ni wadau wa Kiswahili, waendesha baiskeli, waendesha pikipiki na vikundi vya mbio za taratibu. Matembezi hayo yalianzia Viwanja vya Biafra, Kinondoni hadi katika Viwanja vya Posta, Kijitonyama, Dar es Salaam.

Mgeni rasmi wa matembezi hayo alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ambaye katika hotuba yake alisema Dar es Salaam ni miongoni mwa mikoa yenye shughuli nyingi za kibiashara hapa nchini.

Alisema kwa kiwango kikubwa, shughuli zote hizo zimekuwa zikifanyika kwa kutumia lugha ya Kiswahili kama kiungo cha mawasiliano kwa wenyeji na wageni. “Nitumie fursa hii kutambua mchango wa lugha ya Kiswahili katika ukuzaji wa uchumi kwa Jiji letu la Dar es Salaam pamoja na taifa kwa ujumla kwani,

Kiswahili ndiyo lugha yetu inayotumika kwenye shughuli mbalimbali za uzalishaji mali,” alisema Chalamila. Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Bakita, Consolata Mushi anasema matembezi hayo yamekuwa fursa muhimu ya kuelimisha na kufurahia utajiri wa lugha ya Kiswahili.

Akasema kuelekea Julai 7, 2024 ni muhimu kwa kila mmoja kujivunia na kushiriki katika kukikuza na kukitangaza Kiswahili popote alipo. Aidha, Julai 6, 2024 Bakita kwa kushirikiana na wadau wengine wa Kiswahili liliandaa Mjadala wa Wazi wa Mwanamke Hazina uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Lengo la mjadala huo lilikuwa kuonesha namna mwanamke alivyopitia katika hatua mbalimbali za maisha kutoka kutwezwa utu wake hadi kushiriki kikamilifu katika shughuli za uongozi, siasa, uchumi, ujasiriamali, sanaa, michezo, ulinzi na usalama na shughuli nyingine nyingi.

Mjadala huo ulihudhuriwa na watu mbalimbali, wakiwemo wanafunzi wa vyuo vikuu na wadau wa Kiswahili. Miongoni mwa mapendekezo yaliyotolewa katika mjadala ni kuwako kwa majukwaa ya mara kwa mara ya aina hiyo, kuwaweka pamoja vijana wa kike na wa kiume kwa ajili ya mafunzo ya kujitambua na kufanya makongamano ya mara kwa mara ya lugha ya Kiswahili.

Kilele cha Masikidu 2024 kitaifa kilifanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Dar es Salaam Julai 7, 2024. Mgeni rasmi wa kilele hicho alikuwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro. Akitoa ujumbe wa Masikidu, Rais Samia Suluhu Hassan aliwataka viongozi wa dunia kutumia Kiswahili kukuza utangamano na amani miongoni mwao.

Alisema kuwa Kiswahili kina nafasi kubwa katika kuwaleta watu pamoja na kufundisha maadili. “Natoa rai kwa viongozi wenzangu kote ulimwenguni kutumia Kiswahili katika kukuza utangamano, kujenga na kulinda amani na mshikamano.

“Kiswahili ni fursa ya kufanikisha malengo ya maendeleo ya nchi zetu, bara letu la Afrika na dunia kwa ujumla,” anasema Rais Samia. Aidha, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro anatoa mwito wa matumizi ya lugha ya Kiswahili katika maeneo mengine muhimu, ikiwa ni pamoja na katika matumizi ya akili mnemba.

ITAENDELEA…

Tujivunie Kiswahili, Moja ya Tunu za Taifa Letu.

Mhariri Mkuu wa BAKITA +255 713 616 421

[email protected]/