Wazee kadhaa mkoani Mbeya walifunga barabara kwa muda ili kumwomba Mungu (siyo mungu) aepushe ajali zinazotokea mara kwa mara mkoani humo.

Kama ilivyotarajiwa, tukio hilo limeibua mjadala miongoni mwetu. Mjadala huo ulijiegemeza zaidi katika maeneo makuu mawili.

Mosi, wapo waliosema kitendo cha wazee wale kilikuwa cha kishirikina, na kwamba ushirikina hauna nafasi katika ulimwengu wa leo. Kwao wao, wazee kupeleka maombi yao kwa huyo ‘Mungu’ asiyeonekana lilikuwa kosa! Sina hakika kama kauli ingebaki kuwa hivyo hivyo endapo shughuli hiyo ingefanywa na mapadri au masheikh. Hili nitalijadili.

Pili, wapo walioona kitendo cha wazee wale kilikuwa cha kupoteza muda hasa kwa kuwakwamisha wasafiri. Kundi hili linaamini kuwa ajali zinazotokea Mbeya na kwingineko si jambo la kumtwisha Mungu mzigo, bali ni uzembe wetu wenyewe – hasa wale wenye dhamana ya kusimamia vyombo vya usafiri. Hili naliona lina ukweli.

Msimamo wa kundi hili la pili umenifanya nirejee kwenye kijitabu cha Tujisahihishe kilichoandikwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mei 1962. Mwalimu aliamini kuwa yapo mambo tunayokwama kwa sababu ya kutotumia akili zetu vizuri. Kwa heshima kubwa naomba niyanukuu maneno hayo ya Mwalimu kutoka kwenye kijitabu hicho. Mwalimu anasema:

Sababu moja ambayo ilituzuia sisi Waafrika kuendelea ni majibu ya urahisi kwa matatizo makubwa. Shamba letu kama halikutoa mavuno ya kutosha, jibu lilikuwa wazi; au limelogwa au ni amri ya Mungu. Watoto wetu walipokuwa wagonjwa daima, jibu lilikuwa rahisi; au walilogwa au ni amri ya Mungu. Nyumba yetu ilipopigwa radi ikaanguka, jibu lilikuwa rahisi; au ni uchawi au ni amri ya Mungu. Majibu ya namna hii huzuia binadamu kupata sababu za kweli za matatizo yao, na kwa hiyo yanazuia akili kutafuta njia za kweli za kuondoa matatizo hayo.

Siku hizi, tumeanza kutumia majibu mengine rahisi, mambo yakienda mrama, badala ya kutumia akili zetu na kutafuta sababu za kweli, tunalamu Wazungu, au Wahindi, au ukoloni, au ukoloni-mpya, au vibaraka n.k. Yawezekana kweli kwamba kosa ni la Wazungu, au Wahindi, au ukoloni, au ukoloni-mpya, au vibaraka n. k.-lakini yafaa akili ifikie jibu hilo baada ya uchaguzi wa kweli, siyo sababu ya uvivu wa kutumia akili! Uvivu wa kutumia akili unaweza kufanya tutumie dawa kuondoa matatizo ambayo si ya dawa hata kidogo. Nikienda kwa mganga anitibu maradhi yangu, namtazamia kuwa kazi yake ya kwanza ni kujua hasa, siyo kwa kubahatisha, naumwa nini; kazi yake ya pili ni kujua sababu ya ugonjwa wangu; kazi yake ya tatu ni kujua dawa ya ugonjwa wangu. Daktari asipojua ugonjwa wangu na sababu zake hawezi kujua dawa yake. Akinipa dawa nikapona, atakuwa kaniponya kwa bahati tu, kwa desturi daktari wa namna hiyo hawezi kumponya mgonjwa, na ni daktari wa hatari sana.

Kadhalika, chama ambacho nia yake ni kuwa daktari wa matatizo ya jumuiya hakina budi kiwe na tabia ya kujua matatizo yenyewe, sababu za matatizo hayo, na dawa yake. Bila kujua matatizo na sababu za matatizo hayo hakiwezi kujua dawa yake. Daktari anayejidai kuwa anajua kila kitu, na kumbe hajui kitu, ni hatari zaidi kuliko daktari anayekiri kuwa hajui kitu. Kadhalika, kiongozi anayejidai kuwa anajua kila kitu, na kumbe hajui, ni hatari zaidi kuliko yule anayekiri kuwa hajui kitu na yuko tayari kujifunza. Kwa kweli huyu wa pili si hatari hata kidogo kwa sababu kama nilivyosema mapema, ufunguo wa elimu ni kule kutambua kuwa hatujui kitu!Mwisho wa kunukuu.

Kamwe, sitochoka kutoa mwito kwa wananchi, na hasa viongozi wetu wote kusoma vitabu vya Mwalimu Nyerere. Ndani ya vitabu vyake yamo mambo mengi yenye manufaa.

Maneno haya yanajidhihirisha kwenye matendo yetu. Leo, kuna makundi mengi na makubwa ya watu wanaodhani kwa kushinda yakisali makanisani au misikitini yatayabadili maisha yao. Huko ni kujidanganya. Sidhani kama kina Bill Gates, Mzee Mengi, Mzee Dewji, Mzee Bakhresa na wengine wa aina yao walisali tu mali zikawashukia. Mali inapatikana kwa kufanya kazi.

Pale tunapokwama tumekuwa wepesi wa kuamini tumelogwa au kumsingizia Mungu kwamba yeye ndiye anayetushushia ulofa. Sidhani Mungu wa kweli hufurahi kuwaona watu wake aliowaumba kwa mfano wake, aliowapoa akili na utashi kuliko viumbe wote, wakiishi kwa dhiki. Siamini.

Kwa maneno ya Mwalimu, na kwa yale yanayotokea Mbeya na nchini kote, tunathibitisha kuwa hatujatumia akili kuyakabili matatizo yetu. Ajali haziwezi kumalizwa kwa aina hii ya utendaji kazi wa trafiki. Trafiki wanachofanya ni kusimamisha gari, kuomba leseni na kadi ya gari. Wanakagua bima na stika ya wiki ya usalama. Huo ndio ukaguzi wao. Huwezi kumaliza ajali kwa mbinu hiyo. Gari likipata ajali anayeadhibiwa ni mmiliki! Ajabu sana. Ifike mahali gari likipata ajali aadhibiwe dereva. Pia tuangalie upana wa barabara na umri wa magari. Tumekuwa dampo la magari yasiyofaa.

Kidogo nirejee kwenye hoja ya kwanza ya tambiko ambalo Wazungu na Waarabu wameremba lugha kwa kuita sala, dua, maombi- lililofanywa na wazee wale. Kwanza nitangaze maslahi kwenye hili jambo. Nimebatizwa. Naamini Mungu yupo. Lakini siamini kama Mungu pekee wa kweli ni yule tunayehubiriwa makanisani, misikitini na kwingineko. Mungu ameaminiwa Afrika kwa maelfu ya miaka kabla ya ujio wa Waarabu na Wazungu.

Kabla ya ujio wao, sisi Waafrika tulikuwa na dini zetu. Bahati nzuri hadi leo wapo wenzetu waliobaki nazo. Wageni walipokuja wakaona njia nzuri ya kututawala ni kuanza kututawala akili. Wakafanya kila waliloweza kutuaminisha kuwa mambo yetu yote ni ya kishenzi. Wakasema kusali chini ya miti au mapangoni yalikuwa mambo ya kishenzi, na kwamba ustaarabu ni kusali ndani ya majengo au katika maeneo mahsusi waliyopanga wao.

Wakatuaminisha kuwa majina yetu ni ya kijinga, kishenzi na yamekaa kimkosi-mkosi. Wakafikia hatua ya kutufanya tuamini kuwa majina ya Wazungu na Waarabu ambao hata hatuna nasaba nao, ndiyo majina yenye kuleta neema na heri. Wakaona kubatizwa au kusilimishwa pekee hakutoshi, isipokuwa tuongezwe majina ya ‘ndugu zao’, nasi tukatakiwa tuyakane majina ya ‘kishenzi’ yaliyo chanzo cha mikosi!

Leo Wakristo au Waislamu wakikusanyika barabarani wakaomba Mungu ili ajali zikome, sote tutawaunga mkono. Wakikusanyika kuomba mvua sote tutaona wamefanya jambo la maana sana. Wakiomba neema kwa kutumia majina ya Kizungu tutasema wanatumia majina ya “Watakatifu”. Haya haya yakifanywa na Waafrika, na tena tukiomba kwa kutaja majina ya mababu na mabibi waliokufa miaka mingi tutaambiwa tunaomba ‘mizimu’. Iweje Mzungu aliyekufa yeye awe ‘mtakatifu’, lakini Mwafrika aliyekufa awe ‘mzimu’? Huu ni utumwa mbaya. Wazungu na Waarabu wamefanikiwa kwa kiwango cha juu mno kutuachia udhaifu huu na Waafrika hawaelekei kujikomboa kutoka kwenye mtego huu mbaya.

Tunaambiwa kwenye hadithi za kimapokea kuwa zamani zile wazee wetu walipoona mambo fulani fulani hayaendi vizuri, kama vile kuwapo baa la njaa au kiangazi, waliomba Mungu. Wakasikilizwa. Mvua zikanyesha na neema ikastawi katika nchi. Leo hayo mambo tumeyaita ya ‘kishenzi’ hata kama matokeo yake ni chanya kama yale ya makanisani na misikitini bado tutaaminishwa kuwa tunamwabudu shetani. Shetani gani anayetoa neema kwa wenye kuhitaji? Kutawaliwa ni kitu kibaya.

Wapo watabiri wa ‘kisasa’ wanaoitwa ‘watu walioingiwa na Roho Mtakatifu’. Wanaitwa ‘wanenao kwa lugha’. Tunao Waafrika wengi wa aina hiyo wanaofanya makubwa na mazito kuliko hayo, lakini wanaitwa ‘watu wenye mapepo’ au ‘wapiga ramli’.

Hatuwezi kuendelea kwa kuamini kuwa mambo yoooote ya Waafrika ni ya kishenzi, ni ya kishetani, ni ya ki-mapepo. Hatuwezi kuendelea kwa kuamini majina yetu ni ya kipuuzi, na kwamba yenye neema na baraka ni yale ya Kizungu au Kiarabu. Huu ni utumwa mbaya. Hatuwezi kuendelea kwa kuamini kuwa rangi ya ngozi zetu ni ya nuksi, kwa hiyo tufanye kila linalowezekana tufanane na Waarabu na Wazungu.

Kwa wazee wa Mbeya naungana nao kwa dhana ya kuendesha maombi ya asili-maombi ya Kiafrika maana hata sisi tunamwamini Mungu yule yule asiyeonekana. Wameonyesha Uafrika wetu halisi. Wamefanya jambo jema mno. Nisilokubaliana nalo ni hili la kumsukumia Mungu makosa yanayosababishwa na uzembe na udhaifu wetu wenyewe. Waafrika hatuna budi tujitambue.