Waziri wa Ujenzi, Dk. John MagufuliKatika toleo lililopita (Na. 202), niliandaa moja ya nukuu katika ukurasa wa 19 wa gazeti hili. Ilikuwa ni nukuu ya Rais wa 42 wa Marekani, Bill Clinton aliyoitoa katika Mkutano wa Taifa wa Chama cha Democrat Julai 26, 2004.

Siku hiyo, Clinton ambaye jina lake halisi ni William Jefferson ‘Bill’ Clinton, alitoa siri ya mafanikio ya Wamarekani kiuchumi, akisema, “Wamarekani wanafanya kwa bidii. Hii ndio maana watu wengi wana nafasi ya kuishi ndoto zao.”

Ni maneno machache, yaliyonifanya niyatafakari takribani wiki nzima na hasa wakati huu ambao Watanzania tunaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu. Matokeo yake yatatupa Rais wa awamu ya tano.

Wakati natafakari hivyo, tayari wanasiasa wapatao saba walikuwa wamechukua fomu kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Miongoni mwao wako wanasiasa ambao wana umaarufu mkubwa ikilinganishwa na wengine.

Hakuna siri kwamba wenye umaarufu ni mgombea wa Chadema, Edward Lowassa anayewania nafasi hiyo kwa kofia ya Ukawa na Dk. John Pombe Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Kumbuka Ukawa inaundwa na vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD.

Gumzo la mjini ni wanasiasa hao na hoja ya msingi ni nani mwenye nafasi ya kumshinda mwenzake? Ni nani mkombozi wa kweli kwa Watanzania ambao kwa sasa wamepigika kiasi cha kubaki njiapanda katika mustakabali wa maisha yao ya kila siku.

Lakini wakati Watanzania hao wakiwaza hivyo, wamesahau kwamba wenyewe ni ndiyo wenye jukumu la kutimiza ndoto zao—nazungumzia kujikomboa kiuchumi. Kwa mfano kundi la wafanyakazi ndilo linalotegemewa kwa kuleta maendeleo ya nchi.

Ndilo kundi la kupanga mipango kwa kile kinacholimwa na kuvunwa na Watanzania, lakini ajabu ya Mungu kwa sasa wamekuwa si tena wale wa kuwategemea kutokana na tathmini kwenye mitandao kwamba wako ‘bize’ na mitandao ya kijamii kuliko kazi.

Binafsi nimevutiwa na tathmini nitakayoichambua baadaye baada ya kuipima na kuona kuwa inafaa Watanzania wakalisha elimu hii. Nimejiridhisha kuhusu ukweli wake. Mmoja wa wachangiaji amefanya tathmini hiyo na kuibuka na ratiba ya siku na ya wiki ya baadhi ya wafanyakazi.

Kwa mfano, kuna wakaofika kazini saa 2.30 hadi saa 3.00 asubuhi badala ya saa 1.30 au 2.00 asubuhi. Akifika tu kama kawaida, anawasha compyuta na kuingia Jamii Forum au JF, kadhalika ku-log in facebook, twitter na instagram.

Humo anasabahi watu wengi wakiwa ni marafiki zake na ndugu zake ambako anawapa michapo ya matukio kama vile michezo, siasa, Bunge, Disco nakadhalika huku akimalizia kutupiana utani na mwenzake ambaye pengine muda si mrefu naye alikuwa ameingia ofisini, tena akiwa amechelewa.

Kwenye utani wao unaambatana na kuangalia mavazi namna ya kutengeneza nywele, kama vile, “nywele zako nzuri… mara ooh gauni lake limekupendezea, mara fulani shati lako leo zuri,” mara umependekeza nakadhalika.

Wakimaliza hapo, ni mwendo wa kupata kifungua kinywa, ambako wahudumu wa ofisi nao hupata nafasi ya kufanya usafi wa ofisi, maana nao hutokea wamechelewa au kuingia muda unaofanana saa 3.00 asubuhi.

Kabla ya kuanza safari ya kwenda kwenye chai, huenda akatokea rafiki yao, naye utasikia, “Jamani naomba nisubirini kidogo, niweke handbag yangu au briefcase yangu, nasubirini…” huko kwenye chai mijadala inaendelea hadi saa 5.00 asubuhi.

Wakirudi ni michapo na kusoma barua pepe kabla ya kwenda kupata chakula cha mchana. Kichekesho sasa. Ratiba ya chakula hichjo huwa ni saa 6.00 mchana badala ya kusubiri angalau saa 7.00 mchana. Ratiba ya msosi hugharimu saa nzima na hujumisha ratiba binafsi.

Wanarudi saa 8.00 mchana huku mkononi wakiwa wamebeba chakula ili waje kula wakiwa ndani na kuiba muda wa mwajiri. Msosi wa pili anakula kama hataki maana ameshiba, sema anajibidisha kula kula tu.

Saa 9.00 alasiri atashika majalada mawili matatu na ikifika saa 9.30 anaanza kujiandaa kutoka saa 10.00 kwa kujiweka sawa nywele na kadhalika kabla ya kuwahi vikao vya pombe; harusi, miradi binafsi na miadi mingine. Huyo ni Mtanzania mzalishaji anayetaka maisha mazuri-kudadadadeki.

Ni ratiba ya wiki nzima huku kukiwa na visingizo vya siku kama vile, Jumatatu huitwa Blue Monday (Hapo huwakuta watu wakiugua homa ya kuzidisha kipimo cha ulevi –hangover), habari mpya za wikiendi nakadhalika.

Jumanne huwa ni maandalizi ya sendoff au bag party za Jumatano na Alhamisi wakati Jumatano yenyewe, ni mwendo wa kufuatilia mechi za Ligi ya Mabingwa Ulaya, kuhudhuria sherehe za Sendoff au maandalizi ya sendoff au bag party za alhamisi. Yaani ni vichekesho tupu.

Alhamisi ni kuhudhuria sherehe hizo kabla ya kufanya maandalizi ya harusi za Ijumaa, Jumamosi aun pengine hata Jumapili. Huyo ni Mtanzania mzalishaji anayetaka maisha mazuri.

Kama hakwenda huko basi ujue lazima atakuwa na vikao ama viwili au zaidi vya kamati ya maandalizi ya sherehe zilizotajwa za sendoff, bag party, harusi, au kusafiri kwenda kuona familia au dili binfasi.

Mtu huyohuyo hakosi matukio muhimu kuihudhuria ya misiba ya majirani, watu wa karibu, watu wa mbali, ndugu jamaa na marafiki kabla ya kutembelea au kupeleka watoto  shule au hospital.

Hapohapo hakosi kuchomoa vifaa vya ofisini kama vile daftari, karatasi, rimu, kalamu, kuchapisha na kutoa fotokopi kwa kutumia vifaa vya ofisi, lakini kwa matumizi ya shule ya mwanano au nduguyo au wewe mwenyewe. Hufanya hayo, bila hata hofu.

Katika uchambuzi huu, mtoa mada anasema kwamba mienendo hii hii huwezi kuikuta nchi zilizoendelea ambako Rais mstaafu Clinton anasema “Wamarekani wanachapa mzigo” kiasi cha kusaidia nchi masikini.

Ndiyo maana nasema kwamba, wakati Watanzania tumeweka matumaini yetu kwa Lowassa na Magufuli, bila shaka tumesahau namna wengine walivyombeba Rais Jakaya Kikwete ambaye anamaliza miaka 10 na maswali “Maisha Bora kwa Kila Mtanzania” yako wapi.

Kama hatuwazi kubadili katiba, kwa mujibu wa sheria na maridhiano na kwa upuuzi huu tunaofanya, sioni kama Lowassa au huyo Magufuli anayeweza kutukomboa. Tuanze kukomboa fikra zetu kabla ya kufikiria mtu atatukomboa.