Na Mwandishi Wetu
Urusi kwa sasa inaongoza duniani kwa kuwa na vikwazo vingi vya kiuchumi, nafasi inayoiweka kwenye shaka ya kuporomoka kiuchumi.
Marekani na mataifa ya Ulaya wanazidi kubuni vikwazo vipya ambapo hivi karibuni wameiwekea vikwazo 2,778 na kuifanya kuwa na jumla ya vikwazo 5,530.
Kutokana na vikwazo hivyo, fedha ya Urusi, ‘ruble’ inaporomoka kwa kasi na sasa thamani yake ni dola za Marekani 128 kwenye soko la hisa la dunia.
Hivyo ni kama Urusi inaendesha vita mbili kwa wakati mmoja; upande mmoja wanajeshi wake wanapigana vita Ukraine kwa upande mwingine inapigana vita ya vikwazo vya kichumi ilivyowekewa na mataifa ya Magharibi.
Vita ya nchini Ukraine imedumu kwa siku 20, sasa wakati vita ya kupambana na vikwazo ikizidi kupamba moto huku Rais Vladimir Putin akichukua hatua ya kudhibiti fedha za kigeni kupitia benki kuu ya taifa hilo.
Ni kama Urusi imejiandaa vya kutosha kupambana na vita zote mbili kwa wakati mmoja kutokana na ukweli kuwa benki kuu imehifadhi dhahabu yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 128.5 katika hazina yake.
Kiwango hicho kinaifanya Urusi kuizidi Marekani kwa takriban dola bilioni 4 ya hifadhi ya fedha za kigeni hatua inayoelezwa kufikiwa kipindi cha kuibuka ugonjwa wa corona.
Wachunguzi wanasema taifa hilo lilianza kujiandaa kukabiliana na kitisho chochote cha kiuchumi takriban miaka mitatu iliyopita, ambapo lilianza kubadilisha hazina yake ya fedha.
Urusi ilianza kuhamisha fedha kutoka kwenye dola kwenda kwenye dhahabu na sarafu nyingine kama vile sarafu ya ‘yuan’ ya China.
Kwa mujibu wa Benki Kuu ya Urusi, kupitia soko la hisa, Moscow Exchange (MOEX), inapima uzito wa vikwazo na namna ya kupambana navyo kwa muda wa miezi sita.
Ripoti ya Gold Statistics iliyotoka Septemba 2021, inaonyesha Marekani ilikuwa na hifadhi ya dhahabu tani 8,133.53 ikifuatiwa na Ujerumani iliyokuwa na hifadhi ya dhahabu tani 3,359.11 huku Urusi yenyewe ikiwa na hifadhi ya dhahabu tani 2,298.55.
Kutoka na Benki za Urusi kuondolewa kwenye mifumo ya kifedha ya kimataifa, maseneta kadhaa nchini Marekani bado wanahisi kupitia hifadhi hiyo ya dhahabu ya Urusi vikwazo ilivyowekewa vinaweza visifanye kazi.
Maseneta hao wanafikiria kumshinikiza Rais Joe Biden kupitisha muswada utakaodhibiti kampuni na mashirika mengine nchini Marekani kufanya biashara na Urusi kwa kutumia thamani ya dhahabu.
Seneta Angus King wa Jimbo la Maine, ni mwanzilishi wa hoja hiyo ambapo muswada unaofikiriwa kuibuliwa ameupa jina la ‘Bipartisan Bill’, ukilenga kupitishwa na kuiondoa Urusi moja kwa moja kwenye uchumi wa dunia.
Seneta huyo anaungwa mkono na Seneta John Cornyn wa Texas, Bill Hagerty wa Tennessee na Maggie Hassan wa New Hampshire, wote wakiamini hatua hiyo itasababisha hazina ya dhahabu iliyo nayo Urusi ishindikane kuuzika.
Mfumuko wa bei
Wakati hali ikiwa hivyo kwa Urusi, nchini Marekani na mataifa ya Ulaya wameanza kuonja matokeo ya vikwazo wanavyoiwekea Urusi ambapo mfumko wa bei ya petroli na mazao ya chakula umekuwa mkubwa.
Bei za chakula kama ngano, shayiri na mahindi ambayo huzalishwa kwa wingi Ukraine na Urusi imeanza kupanda kwa haraka katika mataifa ya Ulaya na Marekani.
Mbali na Ulaya kupanda haraka kwa bidhaa mbalimbali katika mataifa yaliyo jirani na Urusi nako kunaonyesha uchumi wa dunia unaelekea kuyumba na huenda usikae imara ndani ya kipindi kifupi.
Marekani inatajwa kutokuwa kwenye nafasi ya kufanya vizuri kiuchumi kutokana na vyama vyake viwili; Republican na Democratic, kuwa kwenye uhasama ukiwahusu Rais Joe Biden na Donald Trump aliyeondoka madarakani mwaka 2020.
Mvutano huo unampa wakati mgumu Biden kufanya uamuzi sahihi ambapo baadhi ya mipango yake, ukiwemo ‘Stimulus Package’ ukipata upinzani ukituhumiwa kuongeza gharama za maisha kwa Wamarekani.
Wiki iliyopita Biden amekaririwa akijitetea kuwa mfumuko wa bei kwenye vyakula umesababishwa na Urusi kusitisha usafirishaji wa mazao yake nchini humo.
Putin akizungumza na wananchi wa Urusi kwa njia ya runinga na redio Alhamisi ya wiki iliyopita, alisema Urusi itaibuka ikiwa imara na huru hata kama imewekewa vikwazo.
Alisema vikwazo vya mataifa ya Magharibi vitawaharibu wao wenyewe na kwamba wameviweka ili kutaka kuharibu hali halisi ya vita inayoendelea nchini Ukraine.
Alisema kutokana na mataifa yanayoisaidia Ukraine kufanya hivyo hadharani hata yeye anaomba mataifa jirani wajitokeze kuwasaidia kupigana vita wananchi wa Jimbo la Donbass.
Aidha, kama njia ya kujibu mapigo, Urusi nayo imeweka wazi nia yake ya kuzuia huduma zake kama nishati ya umeme, pembejeo za kilimo, dawa na mawasiliano katika mataifa ya Magharibi.
Katika hatua hiyo Urusi inatarajia kuzuia takriban vitu 100 ambavyo havitaruhusiwa kusafirishwa nje ya taifa hilo.
Kampuni zilizojiondoa Urusi
Kampuni zilizojiondoa Urusi ni zile zinazotoa huduma ya internet na kutegemea matumizi ya internet kwa kiwango kikubwa.
Kampuni hizo ni Dell, Apple, Amazon, Tiktok, VISA na Mastercards pamoja na Netflex.
Kujiondoa kwa kampuni hizo pia kunatajwa kusababishwa na hatua ya Urusi kudhiti internet nchini humo kuwa ya kasi ndogo ili kujilinda dhidi ya propaganda.
Kampuni nyingine ni ya kuuza vyakula ya Mac Donalds na ya mafuta ya BP ambapo kujiondoa Urusi kutaisababishia hasara ya dola za Marekani bilioni 25.
BP imekuwa Urusi kwa miaka 30 na ilikuwa ikishirikiana na Kampuni ya Roseneft ya Urusi latika kutafiti, kuchimba, kusafirisha na kuuza petroli na gesi asilia.
Hali ya vita kwa sasa
Kwa sasa kumezuka kitisho cha matumizi ya silaha za kibiolojia ambapo Marekani na Urusi zote zinatupiana lawama kila mmoja akimtuhumu mwenzake kutaka kutumia silaha hizo.
Na wakati mgogoro mzito ukiibuka kuhusu silaha za kibiolojia, majeshi ya Urusi yameongeza mashambulizi huku zikiwa zimebaki kilometa chache kuukaribia Mji Mkuu wa Ukraine, Kiev.
Miji kadhaa ya nchi hiyo ukiwamo mji wa Mariupol unapungukiwa huduma za chakula, maji na umeme; hali inayosababisha wapiganaji wa Ukraine kuzidi kukata tamaa.
NATO, Marekani na Umoja wa Ulaya wanazidi kujiweka pembeni wakihofia kuwa wakiingia kwenye vita hiyo kunaweza kuzuka vita ya tatu ya dunia.
Tangu kuanza kwa vita ya Ukraine, takriban watu 1,500 wameripotiwa kuuawa huku wakimbizi wanaoikimbia Ukraine wakiripotiwa kufikia milioni 2.5 kwa sasa.