Rais Jakaya Kikwete ametangaza Tume ya Kimahakama kuchunguza sakata la Operesheni Tokomeza. Tume inaongozwa na Jaji Hamis Msumi.

Katika kitabu chake cha Uhuru wa Mahakama, Jaji Barnabas Samatta amenukuu sifa kadha wa kadha za mtu anayepaswa kuwa jaji.

Miongoni mwa aliowanukuu ni Jaji Ramaswamy wa Mahakama ya Juu ya India, aliyetaja sifa ya jaji kuwa: “Ni lazima awe mweledi wa sheria, mwenye hekima za kibunge, mwanahistoria, mtafutaji wa ukweli, mwenye upeo wa kinabii, uwezo wa kuhimili matakwa ya wakati huu, shupavu wa kuyamudu mahitaji ya baadaye na kuamua kwa dhati kutotawaliwa na vionjo binafsi na upendeleo.”

Maneno haya nayaunganisha kwenye faraja tuliyoipata baada ya Rais Kikwete kukamilisha ahadi yake ya kuunda Tume hiyo kama alivyoahidi mwishoni mwa mwaka jana. Tume imepata majaji weledi na wenye sifa zilizotajwa na Jaji Ramaswamy. Matarajio ya wengi ni kuona ukweli juu ya Operesheni Tokomeza unajulikana na kuwekwa wazi.

Hatua hii ya kuundwa kwa Tume imepunguza yale niliyokusudia kuyaandika hapa. Na pengine nitumie fursa hii kumsihi komredi mwenzangu, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, awaache kwanza kina Profesa Alexander Songorwa na Profesa Jafari Kidegesho, waendelee na dhima zao kama ilivyoamuriwa na mamlaka ya uteuzi hadi hapo tutakapopata matokeo ya Tume ya Jaji Msumi.

Wiki iliyopita, Wizara ya Maliasili na Utalii, kwa mara nyingine ilikuwa kwenye wingu zito la migogoro inayosababishwa na Nyalandu. Kuna dhana kwamba Waziri huyu anaandamwa kwa sababu kuna watu ambao hawakufurahi kuona akishika wadhifa huo.

Hao wenye mawazo hayo wanakosea. Warejee kwenye maandishi. Nyalandu amekosolewa muda mrefu sana tangu akiwa Naibu Waziri katika Wizara ya Viwanda na Biashara. Aliyekuwa Waziri wake, Cyril Chami, alikiona cha moto; na kama ilivyotarajiwa, alitupwa nje ya Baraza la Mawaziri na yeye Nyalandu akasogezwa Maliasili na Utalii. Hapo nako tumeona. Balozi Khamis Kagasheki kaondoka, na nafasi yake imeshikwa na Nyalandu. Hapo unaweza kujiuliza, huyu bwana ana ngekewa ya aina gani? Je, ni mchapakazi hodari au ni bingwa wa kuwaundia mizengwe wenzake ili yeye abaki? Sijui.

Naipongeza Ikulu kwa umahiri wake katika kulishughulikia suala la maprofesa hao wawili — Songorwa na Kidegesho. Bado tunasubiri kuona uamuzi huo huo ukifanywa kwa Aloyce Nzuki, ambaye licha ya kuifanya Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) kuongeza idadi ya watalii kutoka wastani wa laki 8 hadi kufikia milioni 1.2 hivi; amefukuzwa! Nyalandu ana mzio na maprofesa na madaktari? Hilo tutalijadili mbele ya safari.

Tangu alipowatimua maprofesa hao, wadau wa uhifadhi tulijitokeza kuhoji uhalali wa hatua hiyo. Tulijua hakuwa na mamlaka ya kuwaondoa. Katibu Mkuu Kiongozi alitoa majibu ambayo mwenye kujua alitambua kuwa Nyalandu hakuwa sahihi. Hakufanya kwa bahati mbaya, bali alikusudia kwa sababu ni ukweli ulio wazi kuwa kwa umakini wa wakurugenzi hao, na kwa kazi murua waliyoifanya ndani ya kipindi kifupi, Nyalandu alijua hao si watu wa kaliba anayoitaka! Yeye anataka kuonekana mkubwa, na kwa hiyo wanaomfaa ni wale wa “Yes Sir”.

Tambo za Nyalandu za kukamata pembe za ndovu kule Singida na kwingineko, ni matokeo ya hao hao aliowafukuza. Waliifanya wakiwa wameshatupwa nje. Walisukumwa na uzalendo na mtandao walionao na watoa habari wanaowaamini na kuwaheshimu. Hao si watu wa kupewa taarifa halafu wakaitumia kupata pesa! Lakini kwa kuwa Nyalandu ni mwanasiasa, na kwa kuwa anataka aonekane ameijaza barabara nafasi ya Kagasheki, akaibuka haraka haraka kwa ndege kwenda kupigwa picha ili aonekane amefanya kazi!

Ni Nyalandu huyu huyu ambaye anajua wiki iliyopita ndovu watatu wakubwa kweli kweli (jumbo) waliuliwa Monduli. Hajajitokeza hadharani kutangaza habari hiyo mbaya! Hajachelewa, huenda akatangaza. Tunasubiri awaite waandishi wa habari katika hoteli moja kati ya Serena, Sea Cliff (Dar es Salaam) au Mount Meru, Arusha! Ukumbi wa mikutano pale wizarani kwake, au pale TANAPA, Arusha hauna hadhi ya yeye kuingia na kuzungumza mambo ya kitaifa! Anapokutana na wanahabari Serena Hotel, kwa mfano, siku hiyo lazima moja ya taasisi za Wizara yake ilipe wastani wa Sh milioni 3 hadi Sh milioni 4. Hiyo ni kwa siku moja tu! Malipo haya yangeweza kuokolewa kwa kutumia kumbi za Wizara yake! Anataka aonekane akiwa katika mandhari inayolingana na hadhi yake! Huyo ndiye Nyalandu ambaye akiguswa, analalama. Eti anaonewa gele! Anadai wanaomsema ni majangili tuliotumwa kuvuruga vita ya ujangili!

Tume ya Kimahakama itatusaidia kutegua mafumbo tuliyofumbwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge, na wanasiasa waliodiriki kumwaga chozi bungeni ili kukoleza hoja zao. Bungeni ukimwaga chozi wanaokutazama watakuamini haraka. Alianza Waziri Mkuu, na juzi juzi Sheikh Jongo naye akalia, lakini hapo hapo machozi yakakata. Huzuni ikamtoka na kuanza kutetea Serikali Mbili! Machozi ni kitulizo na kijenzi cha hoja!

Mosi, Tume itusaidie kujua ni kwa namna gani Waziri anaweza kuwajibishwa, lakini Msaidizi na Mshauri wake Mkuu, akabaki; na punde si punde akapandishwa cheo! Je, ina maana wakati wa Operesheni Tokomeza alikuwa likizo?

Pili, iweje Paul Sarakikya, aliyekuwa mwenye dhamana ya kukabiliana na majangili na ujangili, asiwajibishwe, badala yake abaki wizarani, na mara moja, huyu “mtuhumiwa” mwenzake, yaani Nyalandu, amteue kuongoza Idara ya Wanyamapori kwa kumwondoa Mkurugenzi aliyeikuta Idara ikinuka rushwa na kukumbatia majangili?

Sarakikya ndiye aliyekuwa Mkurugenzi Msaidizi Uzuiaji-Ujangili. Yeye ndiye aliyekuwa kiungo kati ya wizara na vyombo vingine wakati wa Operesheni Tokomeza. Kuundwa kwa Operesheni hiyo kulikuwa ni matokeo ya Sarakikya na wenzake kwenye Idara yake kushindwa kazi! Ndiyo, kama wangekuwa wamefaulu, Tokomeza ingeletwa kwa sababu gani? Ujangili uliongezeka wakati wa uongozi wake, na kwa hiyo Profesa Songorwa alichokutana nacho ni ukubwa wa tatizo ambalo hakuna yeyote awaye, anayeweza kuliondoa ndani ya mwaka mmoja!

Profesa Songorwa ametumia miezi 12 kupambana na mfumo mbovu kabisa uliojaa urasimu na rushwa; na ambao kwa namna yoyote asingeweza kuuondoa kwa miaka hata kama ni miwili. Askari Wanyamapori wanampenda kwa sababu wanajua uwezo wake. Huyu si mwanasiasa. Haendeshi mambo kisiasa.

Nimepata kuandika kuwa wanaomfahamu Sarakikya wanajua anavyopenda kushinda ofisini. Wanasema ni mtu wa “njoo kesho”. Wanamtaja kama mmoja wa viongozi wasiokuwa na uamuzi; na hapatikani pale anapohitajika. Anatajwa kuwa na kiburi na kasi ndogo ya utoaji uamuzi isiyoweza kuhimili kasi ya utendaji kazi kwenye tasnia ya wanyamapori. Maneno haya yanaweza yasimfurahishe, lakini huo ndiyo ukweli.

Sarakikya alishakaimu nafasi hiyo kabla ya Profesa Songorwa kuondolewa kibabe. Wakati huo wala hatukuona kama ujangili umepungua. Mtu mwenye sifa zote hizo, anakabidhiwa kuiongoza Idara ya Wanyamapori! Nyalandu si mjinga, anajua afanyalo. Unyenyekevu wa Sarakikya usio wa kawaida kwa Nyalandu, akijitahidi kuonekana mdogo mbele ya Waziri licha ya kukaribia kustaafu, ilikuwa ishara ya wazi kwamba si bure!

Mara kadhaa Sarakikya alipewa taarifa za ujangili, lakini akawa mzito au mgumu kutoa ushirikiano. Mimi ni shahidi wa majibu yake ya kukatisha tamaa. Hawezi kubisha. Aliwataka watumishi wake wanaopambana na majangili walipwe posho za kujikimu kutoka kwa wamiliki wa vitalu vya uwindaji na wadau wengine kwenye tasnia hiyo.

Kibebe alitolewa kwenye pori ambalo mauaji ya ndovu yamepamba moto kweli kweli. Ameshindwa huko, lakini Nyalandu akamsogeza wizarani. Kiongozi ambaye ametoka kwenye pori ambalo kuna mauaji ya kimbari ya ndovu, anapandishwa cheo! Wanaondolewa Waziri, Mkurugenzi na sasa kuna zengwe Katibu Mkuu aondolewe, lakini huyu huyu aliyekuwa porini anapandishwa cheo ili atawale mapori na hifadhi zote!

Ni Kibebe huyu huyu akiwa Msaidizi wa Mwangunga, ushauri wake mbaya ulimfanya Waziri huyo atengue Azimio la Bunge la ugawaji vitalu. Kwa ushauri wake, Mwangunga aliongeza miaka mitatu ya umiliki wa vitalu, kinyume cha Azimio la Bunge.

Licha ya Bunge kuzima mpango huo, Kibebe hakukwama. Amehakikisha baada ya kupandishwa cheo anamshauri na kufanikiwa kumfanya Nyalandu atangaze mambo mawili yenye utata. Mosi, ni uongezaji muda wa umiliki wa Vitalu vya Uwindaji wa Kitalii kutoka miaka mitano hadi miaka 15! Pili, muda wa uwindaji wanyamapori kutoka miezi sita hadi miezi tisa! Hapa ina maana wanyamapori wetu wapigwe risasi mwaka mzima bila kuachiwa muda wa kuzaa.

Wawili hawa ni matunda ya Emmanuel Severe na kwa hiyo kuwapo kwao kwenye nafasi walizokabidhiwa na Nyalandu ni mwendelezo wa yale yale yaliyokuwapo wakati wa Mkurugenzi huyo.

Aprili 2, mwaka huu magazeti kadhaa yalimnukuu Sarakikya akisema: “Vitendo vya ujangili vimepungua kwa asilimia 58…Kupungua kwa vitendo hivyo vya ujangili kunatokana na jitihada za Serikali kuhakikisha inalinda maliasili za Taifa.”

Hapa ndipo penye utata zaidi kwani taarifa hiyo ya Wizara ilitolewa siku 37 tu baada ya Waziri Nyalandu kutangaza kwa mbwembwe kuwaondoa kazini Profesa Songorwa na Profesa Kideghesho.

Ujangili hauwezi kupungua, tena kwa asilimia 58, katika kipindi cha siku 37 tu baada ya maprofesa kuondolewa kazini. Kama ni kweli ujangili umepungua, basi bila shaka yoyote mafanikio hayo yatakuwa ni matokeo ya juhudi za muda mrefu, zaidi ya siku hizo 37. Na, kama tunakubaliana kwa hili, haya yatakuwa ni matokeo ya juhudi za waliofukuzwa na Nyalandu.

Wiki iliyopita Nyalandu ameusaidia umma kumtambua vizuri. Profesa Songorwa akiwa amerejeshwa kazini kwa maelekezo ya mamlaka ya juu ya uteuzi, Nyalandu akaamua kumwaibisha kwa kumfukuza katika ukumbi ambako walikuwa wakiwasilisha taarifa ya Wizara kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira.

Alimfukuza atoke nje akihoji alikuwapo ukumbini hapo kama nani. Mwenyekiti wa Kamati, James Lembeli, hakuwa na namna. Akabariki jambo hilo. Hiyo haikushangaza kwa sababu kwa siku kadhaa wawili hao walikuwa pamoja mbali wakijadili namna ya kusonga mbele. Lakini baadhi ya wajumbe, hasa wabunge wanawake hawakufurahishwa na tukio hilo. Ukiacha madaraka, kiumri Profesa Songorwa ni mkubwa. Waafrika tuna utaratibu wa mdogo kuwa na staha kwa aliyemzidi umri hata kama hampendi. Profesa Songorwa ni msomi na mcha Mungu. Hakupinga uamuzi wa Waziri hata kama ni mdogo kiumri. Akatoka nje akiwa amejiinamia, lakini bila shaka moyoni akiwa na faraja!

Jaji Samatta katika kitabu chake cah Uhuru wa Mahakama, Ukurasa wa 166 anawaasa waandishi wa habari kwa kusema: “Wanahabari msimwonee mtu yeyote yule. Lishughulikieni kila suala linalojitokeza kwa mujibu wa sheria za nchi na kanuni za maadili ya fani yenu. Pambaneni na wale wote nchini wanaokubaliana na matamshi ya kutisha aliyoyatoa Napolean Bonaparte, mtawala wa Ufaransa katika karne ya 19 aliposema, ‘Kuna kitu kimoja tu hapa duniani, nacho ni kuendelea kupata fedha na fedha zaidi, mamlaka na mamlaka zaidi. Vitu vingine vilivyobaki havina maana’.”

Kila nikimtazama Nyalandu na wafuasi wake ndani na nje ya Wizara ya Maliasili na Utalii naona falsafa yao ni: “Fedha na Fedha Zaidi, Mamlaka na Mamlaka Zaidi. Vitu Vingine Vilivyobaki Havina Maana”.