Katika sehemu hii ya nne na ya mwisho ya makala hii iliyobeba anuani ‘Kwa nini Waislamu nchini wawe chini ya Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (BAKWATA)”, ninapenda kwa dhati kabisa kuwashukuru wasomaji wa Gazeti hili la
JAMHURI ambao huwasiliana nami na kutoa maoni yao.
Namshukuru sana msomaji kutoka Pangani, Tanga aliyeniambia kuwa sasa ameelewa umuhimu wa Waislamu kuwa chini ya Bakwata na akataka elimu hii itolewe zaidi kwani huko Pangani kuna msikiti Waislamu hawakufanya uchaguzi wa Bakwata ngazi ya msikiti kwa madai wao hawako chini ya Bakwata! Makala hii inakusudia kujibu baadhi ya hoja zilizonifikia kutoka kwa wasomaji wetu.
Bakwata ni chombo cha Serikali?
Swali hili limekuwa likijirudia sana katika ndimi za watu mbalimbali na hata kalamu za baadhi ya waandishi wa ndani na nje ya nchi, kiasi cha baadhi ya watu kuamini kuwa Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata) ni chombo cha
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ukweli ni kuwa Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata) si chombo cha serikali wala chama chochote cha siasa nchini. Hili linathibitika kutokana na ukweli unaobainishwa na nukta zifuatazo:
1. Bakwata ni jumuiya ya kidini isiyo ya kiserikali iliyoandikishwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mujibu wa Sheria ya Jumuiya za Kijamii (Socities Act) wakati vyombo vya serikali ni vile vinavyoanzishwa kwa sheria zinazotungwa
na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
2. Bakwata si chombo cha serikali kwa kuwa vyombo vya serikali huwa chini ya wizara za serikali vikiwajibika huko na kuwa na bajeti zinazosimamiwa na serikali na kupitishwa na Bunge pamoja na kufuatiliwa na Kamati za Kudumu za Bunge kwa kule kutumia kwake mapato ya serikali katika kuendesha mambo yake.
3. Bakwata si chombo cha serikali, kwa kuwa kwa mujibu wa Katiba yake hakuna kiongozi yeyote wa Bakwata anayeteuliwa na mamlaka ya kiserikali kama ilivyo ada ya vyombo vya serikali. Bakwata viongozi wake na wawakilishi wa vikao mbalimbali kutoka ngazi ya msikiti, kata, wilaya, mkoa na taifa wanachaguliwa na Waislamu wenyewe na wanateuliwa na mamlaka zilizoundwa ndani ya Bakwata kwa mujibu wa Katiba yake.
Ukizingatia ukweli huu utaona dhahiri kuwa Bakwata si chombo cha serikali wala chama chochote cha siasa bali “ni chombo cha kudumu kilichoundwa mwaka 1968 kuratibu, kusimamia na kuongoza shughuli zote za Waislamu nchini Tanzania (Tanzania Bara) kwa lengo la kutekeleza wajibu wa Waislamu wa kuendeleza na kuimarisha itikadi yao ya kidini, kukuza na kuimarisha ushirikiano, umoja na udugu miongoni mwao na kwamba umma wa Kiislamu popote ulipo una wajibu mkuu wa kuwa na ‘Kauli Moja’ inayotafsiri Umoja na Mshikamano baina yao kama Allaah Mtukufu alivyowaamrisha katika Qur’aan Tukufu Sura ya 3 (Surat Ali-Imraan), Aya ya 103.”
Bakwata haipo kwa masilahi ya Waislamu!
Hoja hii ni miongoni mwa yale yaliyowafanya baadhi ya Waislamu kutotekeleza amri ya Allaah Mtukufu ya kujenga umoja na mshikamano baina yao na kufuata maagizo ya Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) ya kuutii uongozi wa Waislamu na kukumbwa na propaganda chafu zenye dalili ya kukufurisha (takfiir) kwa kuzusha kauli: “Sisi ni Waislamu na wale ni Bakwata”. Ni dhahiri kuwa kinyume cha “Waislamu” si “Bakwata” bali “wasio Waislamu” na asemaye hayo anamaanisha kuwa upande wa Bakwata si Waislamu. Astaghfiru Llaah!
Nasema ni propaganda chafu kwa kuwa Bakwata kwa mujibu wa Katiba yake inaundwa na Waislamu waliopewa uanachama huru na wa moja kwa moja kutoka ngazi ya msikiti hadi taifa. Unaposema Bakwata unamaanisha ni mkusanyiko wa maimamu na maamuma Waislamu wa misikiti yote inayochagua viongozi kwa mujibu wa Katiba ya Bakwata na viongozi na wajumbe wa vikao mbalimbali wa ngazi ya kata, wilaya, mkoa na taifa. Kama Waislamu hawapatikani katika mkusanyiko huu unaosimamisha Swala Tano kila siku watapatikana wapi?
Kwa kuwa Bakwata inaendeshwa kwa vikao na kikao kikuu chenye maamuzi ya mwisho ni Mkutano Mkuu wa Bakwata unaowaleta pamoja Mheshimiwa Mufti na Sheikh Mkuu akiwa ndiye mwenyekiti, wajumbe wa Baraza la Ulamaa, Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu na wajumbe wa Halmashauri Kuu wakiwemo Katibu Mkuu na manaibu wake wawili, wadhamini wa Baraza, masheikh wote wa mikoa na wilaya, wenyeviti wote wa halmashauri za mikoa na wilaya, makatibu wote wa mikoa na wilaya na wawakilishi wa Jumuiya za Wanawake na Vijana; ikiwa mkusanyiko huu utaridhia kufanyika yale yasiyo na masilahi na Uislamu na Waislamu basi tatizo halitakuwa chombo kinachoitwa ‘Bakwata’ bali ni Waislamu
wenyewe waliopewa dhamana na Waislamu wenzao (jamii) na hapo neno la karibu litakuwa: “Jamii inapochagua uongozi hupata unaoistahili”.
Kwa kuwa viongozi wa Bakwata wanatokana na uchaguzi unaofanywa kuanzia ngazi ya msikiti ambapo wajumbe wa mkutano mkuu wa msikiti ni Waislamu wote wanaoishi katika eneo la utawala la msikiti huo na wanaswali katika msikiti huo, na kwamba kikao chenye maamuzi ya mwisho ni mkutano mkuu tulioueleza, ni dhahiri kuwa hoja ya kimantiki haitakuwa “Bakwata haipo kwa masilahi ya Waislamu” bali “Waislamu hawapo kwa masilahi yao”.
Bakwata ilianzishwa kwa fikra ya Mwalimu Nyerere kwa lengo maalumu?
Hakuna hoja isiyo na mantiki kama hoja hii. Kwa nini? Waislamu wanatambua kuwa umoja ni jambo aliloliamrisha kwao Mwenyezi Mungu na Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) na kwamba ni wajibu wao kulifikia lengo la kuwa na ‘kauli moja’ inayotafsiri umoja na mshikamano baina yao na ili kufikia hilo panahitajika nyenzo ya kuwaleta Waislamu pamoja chini ya kiongozi mkuu mmoja.
Kama Mwalimu Nyerere ndiye aliyewakumbusha Waislamu wajibu wao huu na akawasaidia kufikia lengo hilo kwa kuundwa Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania, basi hatuna budi, kwa dhati kabisa, kumshukuru Rais wa Kwanza wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwa wema huu aliotufanyia. Tumshukuru Mwalimu!
Lakini jambo la kujiuliza, vipi fikra ya Mwalimu Nyerere ya Waislamu kuwa chini ya chombo kimoja chenye nguvu kinachowaunganisha ionekane kama ‘nuksi’ ya chombo wakati historia inatuonyesha kuwa asilimia kubwa ya waliokuwa katika hizo jumuiya za Kiislamu za kimaeneo na kikabila ndio hao hao waliogeuka kuwa viongozi na watumishi wa Bakwata?
Namkumbuka marehemu mzee Khatibu Mavura akielezea safari yake ya kutoka East African Muslim Welfare Society
(EAMWS) hadi Bakwata. Bali wapo wengi walio hai kina mzee Suleiman Hega, Sheikh Mohamed Mtulia, mzee Abdul Mwanamdege wa Kyaka, Kagera na wengineo.
Vipi udhaifu wa Bakwata uliotokana na udhaifu wa kiuongozi na kiutumishi kwa baadhi ya viongozi na watumishi uhusishwe na aliyetoa fikra njema? Hivi, kwa mfano, Waislamu wakishindwa kukiendesha Chuo cha Waislamu
Morogoro (MUM) ambacho ni fikra iliyotoka kwa Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, mzee Benjamin William Mkapa ambaye aliyatoa majengo ya umma – Chuo cha Tanesco Morogoro kuwapa umma (Taasisi ya Maendeleo ya Waislamu – Muslim Development Foundation kwa niaba ya Waislamu, chini ya Mwenyekiti marehemu mzee Kitwana Kondo (Allah Amrehemu), Makamu Mwenyekiti Alhaj Abdulrahman Omar Kinana na Katibu Alhaj Balozi Daktari Ramadhani Kitwana Dau na wenzao) itakuwa kushindwa huko ni kwa sababu fikra ya kuwa na chuo kikuu na mtoa majengo ya umma kuwapa umma ni Rais mstaafu Benjamin William Mkapa? Ni kweli? Mantiki inakubali? Kama ni kweli, nini sababu ya kushindwa kufikia malengo mema kwa taasisi zilizolenga mawanda makubwa na zilizoanzishwa kwa fikra, utashi na nguvu ya Waislamu wenyewe kama Baraza la Misikiti Tanzania (BAMITA), Jumuiya ya Vijana wa Kiislamu Tanzania – Tanzania Youth Muslim Association (TAYMA) na Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania?
Nihitimishe makala hii kwa kuwanasihi Waislamu kuitekeleza falsafa ya Mheshimiwa Kiongozi Mkuu wa Waislamu nchini Mufti na Sheikh Mkuu (Shaykhul Islaam) Sheikh Abubakar Bin Zubeir Bin Ally Mbwana ya Jitambue, Badilika, Acha
Mazoea kwa kujitambua kuwa sisi ni Waislamu na nguvu yetu, kama ilivyo kwa jamii yoyote iwayo, ipo katika umoja na mshikamano baina yetu; tubadilike kutoka kujitia utumwani mwa historia na propaganda hasi na kusimama imara kuweka daraja thabiti baina ya viongozi wetu/masheikh wetu na wasomi wetu wa fani mbalimbali chini ya moyo wa kutoa na kujitolea; tuache mazoea ya mifarakano, chuki binafsi, fitna, kupigana ngwala wenyewe kwa wenyewe na kushughulishwa
na nani anafanya nini badala ya kuridhishwa na uzuri na ubora wa kile kinachofanyika. Haitusaidii chochote kuendelea kufukua makaburi ya wale waliopita, kwani Qur’aan Tukufu Sura ya 2 (Surat Al-Baqarah), Aya ya 134 imeshakata shauri: “Hao ni watu waliokwishapita. Watapata waliyoyachuma, nanyi mtapata mtakayoyachuma; wala hamtaulizwa nyinyi waliyokuwa wakiyafanya wao.”
Shime tujenge umoja na mshikamano chini ya Kiongozi Mkuu Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania na tuchangie fikra na uwezo wetu wa hali na mali kutekeleza madhumuni ya Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata) huku tukizingatia
maelekezo ya Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Qur’aan Tukufu Sura ya 8 (Surat Al-Anfaal), Aya ya 46 kuwa: “Na mjilazimishe kumtii Mweyezi Mungu na kumtii Mtume wake katika hali zenu zote, wala msitofautiane kikawa chanzo
cha neno lenu kuwa mbalimbali na nyoyo zenu kutengana, mkaja kuwa madhaifu na nguvu zenu kuondoka na ushindi wenu; na subirini mnapokutana na adui. Hakika Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wenye kusubiri, kwa kuwasaidia, kuwapa ushindi na kuwapa nguvu, na hatawaacha.”
Haya tukutane Jumanne ijayo In-Shaa-Allaah.
Sheikh Khamis Mataka ni Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata).
Simu: 0713603050/0754603050