Tukio la hivi karibuni ambapo wajumbe wanaounda kundi la Umoja wa Katiba wa Wananchi (UKAWA) kuamua kuyakana makubaliano yaliyofikiwa baina yao na Rais Kikwete kupitia Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), haliwezi kupita bila kuhojiwa.
Itakumbukwa kuwa wajumbe wa UKAWA kupitiaTCD walikutana na Rais Jakaya Kikwete Septemba 8, 2014 kuzungumzia mustakabali wa Katiba Mpya. Sipendi kudurusu yale yaliyojiri kwenye kikao hicho kwani mengi yameshaandikwa na waandishi wa habari.
Kimsingi mengi yaliongelewa lakini kikubwa walikubaliana kwenye maeneo yafuatayo. Mosi, vikao vya Bunge Maalum la Katiba (BMK) viendelee mpaka mwisho Oktoba 4, 2014. Pili BMK kwa sasa inafanya kazi yake kwa mujibu wa sheria (GN), namba 254 (tangazo la Serikali), kitu kisichompa Rais mamlaka ya kukivunja kwa sasa.
Makubaliano mengine yaligusia Uchaguzi Mkuu 2015 na za Serikali za mitaa. Kwa vile Uchaguzi Mkuu utafanyika kwa kutumia Katiba ya 1977, ni vyema yakafanyika mabadiliko madogo ili kuruhusu uchaguzi huru na wa haki.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa kikao hicho, John Cheyo, mabadiliko hayo yatalenga kuwezesha uwepo wa tume huru ya uchaguzi; mshindi wa urais apatikane kwa zaidi ya asilimia 50, kuruhusu mgombea binafsi na matokeo ya urais kupingwa mahakamani.
Ni katika msingi huu, nashawishika kuamini kuwa makubaliano haya pamoja na mabadiliko yaliyofikiwa, yalitosha kabisa kujibu matakwa ya UKAWA katika suala zima la kusitishwa kwa Katiba ili hatimaye kuruhusu mjadala kuhamia katika mambo mengine juu ya mjadala kuhamia katika Uchaguzi Mkuu 2015.
Hata hivyo, kwa mshangao wa wengi, siku moja tu baada ya makubaliano haya kufikiwa, UKAWA wakasikika wakipaza tena sauti kuashiria msimamo wao juu ya madai ya kusitisha kwa vikao vya BMK, licha ya wenyewe kufahamu kuwa Rais Kikwete hakupewa mamlaka ya kusitisha.
Nianze kuchambua mada hii kwa kugusia mambo makuu matatu. Mosi, muda uliobaki kuelekea Uchaguzi Mkuu 2015. Pili, staili ya kuvizia matukio ya kisiasa na tatu nchi inatawaliwa kwa mujibu wa sheria na katiba.
Licha ya UKAWA kutambua kuwa muda uliobaki kuelekea Uchaguzi Mkuu 2015 ni mfupi, na kwamba chama chao bado hakijajijenga sana katika soko la wapiga kura vijijini kama ilivyo kwa mahasimu wao Chama Cha Mapinduzi (CCM), inashangaza viongozi wake wakiendelea kung’ang’ania hoja ya kusitishwa kwa vikao halali vya BMK.
Haingii akilini kwamba ni wakati gani watazinduka kwenda kuwapigia hodi wapiga kura vijijini, ilhali wakijua hoja wanayoing’ang’ania kwa sasa haina tija.
UKAWA wanazidi kupoteza muda huku wakiwachanganya wanachama na wapenzi wake wasijue dira na mwelekeo wa chama. Hawajui wataanza kujipanga lini kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu 2015 na wa Serikali za Mitaa. Kwanini kupoteza muda ilhali wakijua Bunge haliwezi kusitishwa kwa shinikizo au vitisho?
Wakati UKAWA wakizidi kupoteza muda kwa hoja isiowaongezea mitaji (wapiga kura), mahasimu wao kwa upande mwingine wanachanja mbuga chini ya Katibu Mkuu Abdulrahman Kinana na Nape Nnauye wakipita huku na kule kote nchini kunadi sera za chama na kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya chama chao.
Pili, wakati UKAWA wakiendelea kuishi kwa fikra mgando ya kuvizia huku wasubiri matukio ya kisiasa kutokea kwa mahasimu wao CCM, kwa mfano masuala ya ufisadi, Akaunti ya Malipo ya Nje (EPA), Akaunti ya Escrow, IPTL, mawaziri mizigo nk, wenzao CCM wanajipanga kuanzia ngazi ya shina, matawi hadi Taifa kunadi sera kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu 2015 na Serikali za Mitaa.
Ifahamike kwamba katika mfumo wa demokrasia, mshindi anapatikana kwa njia ya kupiga kura ya wengi wape. Hakuna ushindi unaopatikana kwa staili ya kususia, kulalamika, shinikizo, kuandaa maandamano yasiyokuwa na mwisho wake, la hasha. Bali njia pekee ya kupata ushindi ni kwa kurubuni wapiga kura wengi.
Mbinu hizi za kuvizia matukio ya kisiasa na kuweka mashinikizo kama alivyotaja Mbowe wakati akifunga Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Chadema, kamwe haziwezi kuwafikisha mbali. Maazimio aliyotaja hayana tija. Watambue kuwa dhana ya demokrasia ya “wengi wape” ndiyo msingi mkuu katika mukhtadha wa ushindani.
Hoja ya tatu, Mwenyekiti Mbowe na wajumbe wa UKAWA watambue kuwa vikao vinavyoendelea bungeni (BMK) ni vya halali kwa mujibu wa sheria namba 254. Wasipoteze muda wao katika hoja wanazojua hazitekelezeki.
Licha ya kutambua kuwa nchi inatawaliwa kwa mujibu wa sheria, UKAWA wameendelea na msimamo wa kusitishwa kwa vikao vya BMK ilhali wakifahamu fika kuwa Rais hakupewa mamlaka ya kisheria ya kusitisha vikao hivyo kwani vinaendelea kwa mujibu wa sheria namba 254.
Haihitaji elimu ya chuo kikuu kung’amua kuwa UKAWA wanamvizia Rais Kikwete (mtego), kuwa endapo atathubutu kusitisha vikao hivyo, basi watumie mwanya huo kumshtaki kwa kuvunja Katiba ya nchi. Mbinu hizi za kuvizia kisiasa ni fikra ambazo zimepitwa na wakati.
Mwenyekiti Mbowe na wajumbe wake watambue kuwa vikao vya Bunge vinaendelea kwa mujibu wa sheria. Wakubali kusahau yaliyopita. Warudi wakae chini wabuni mbinu za kuwafikia wapiga kura. Kuandaa migomo na maandamano ya nchi nzima ni uchochezi usiokubalika na Serikali yoyote duniani.
Waachane na maazimio haya ya kipuuzi. Mwisho wa siku CCM wakija kuwapiga bao la kisigino mwaka 2015 wataanza kulalamika Tume ya Uchaguzi haifai, Katiba mbovu, kura zimechakachuliwa nk. Yanini kusubiri mpaka haya yatokee? Muda ndiyo huu wa kujipanga.
Watambue kuwa Watanzania hawana muda wa kupoteza na lugha za vitisho, wanajua kuchambua pumba na mchele. Mbowe, nendeni vijijini mkauze sera na siyo kupiga kelele Dodoma.
Kelele za chura hazimzuii ng’ombe kunywa maji. Tumieni muda huu mfupi uliobaki kunadi sera zenu na siyo vikao vya BMK. Mtego huu hautamnasa Rasi Kikwete. Vikao vya BMK vitaendelea mpaka Oktoba 4, 2014 na si vinginevyo.
Makala hii imeandikwa na John M. Kibasso
Simu: +255 713 399 004 / +255 767 399 004
E-mail: [email protected]