3.4 JEE TANZANIA INA UCHUMI MMOJA AU CHUMI MBILI
3.4.1 Ingawa katika Kitabu cha Muafaka baina ya SMT na SMZ inaeleza kuwa “Tanzania ni nchi moja yenye uchumi mmoja wenye mazingira tofauti” lakini katika utekelezaji Serikali zote mbili zinaonyesha kuwa na jibu tofauti – kwamba uchumi wa Tanzania Bara na Zanzibar ni tofauti. Hata katika hali halisi ndivyo ilivyo. Mtafaruku uliopo unatokana na ukweli kwamba ingawa chumi ni mbili lakini nyenzo zote kuu za uchumi zinadhibitiwa na Serikali ya Muungano. Nyenzo kama vile udhibiti wa sera za fedha, kodi na mahusiano na nchi za nje hazimo mikononi mwa Zanzibar ingawa Zanzibar inategemea ijiendeshe kiuchumi.
Dalili au sababu zinazoonyesha wazi kuwa Tanzania ina chumi mbili ni pamoja na zifuatazo:
(i) Masuala ya Maendeleo ya Uchumi sio ya Muungano; hivyo kila upande una Wizara yake inayoshughulikia uchumi, mipango na sera zake za uchumi na bajeti yake.
(ii) Kila upande una Mfuko wake Mkuu wa Serikali na hivyo mapato yake.
(iii) Kila upande una jukumu la kushughulikia huduma za jamii, miundo mbinu n.k.
(iv) Kila upande una Sera na Sheria zake za biashara na uwekezaji na hata Sheria za ajira.
Pamoja na ukweli huo Katiba ya Muungano haiweki bayana na ndio inayofanya kusiwe na majibu ya wazi ya suala hili kwa sababu zifuatazo:
(i) Kodi ya Mapato, Mikopo ya nje na Biashara za Nje bado yamefanywa ni mambo ya Muungano. Kodi ya Mapato ambayo ni nyenzo kuu ya uchumi wa visiwa ambao ni “Service oriented” badala ya kuwa “resource based” kama ilivyo kwa Bara, bado ni jambo la Muungano kisera,
ingawa mapato halisi yanatumika Zanzibar.
(ii) Sera za fedha na mahusiano ya kikanda yapo chini ya Serikali ya Muungano bila ya kuwa na uwazi wala Sheria inayoilazimisha kushughulikia maslahi ya kiuchumi ya Zanzibar.
3.4.2 Kutokana na kutokuwepo majibu ya wazi na pia kuwepo mtafaruku ya lipi hasa ndio sahihi, ndio maana Kero za Muungano zinaonekana kuzidi badala ya kupungua kwani maisha ya watu hasa wa Zanzibar yamedidimia kutokana na uchumi wa Zanzibar kuanguka kutokana na zao la karafuu kushuka bei. Mategemeo pekee ya kiuchumi au uwekezaji katika nyanja zote hasa za huduma. Hata hivyo Zanzibar haiwezi kuweka sera huru na za kuvutia za kiuchumi kuliko Tanzania Bara kwa vile haina mamlaka katika eneo hilo. Mfano mzuri ni kushindwa kwa miradi ya EP2, Bandari Huru na Off-Share Companies.