3.3 NINI MAANA YA MTU ANAYETOKA ZANZIBAR/TANZANIA BARA
3.3.1 Moja kati ya zilizokuwa nguzo kuu za Muungano ni ile ya uwakilishi wa Zanzibar ndani ya Muungano kupitia Rais wa Zanzibar ambaye alikuwa Makamo wa Rais wa Muungano kwa kupitia wadhifa wake wa Urais wa Zanzibar. Baada ya Marekebisho ya 11 ya Katiba Rais wa Zanzibar aliondolewa katika nafasi ya Makamo wa Rais kwa kupitia wadhifa wake. Badala yake Makamo wa Rais anapatikana na utaratibu wa Mgombea Mwenza. Chini ya ibara ya 47(3) ya Katiba ya Muungano, Mgombea Mwenza anateuliwa kwa Kanuni kuwa iwapo Rais ni mtu anayetoka upande mmoja wa Jamhuri ya Muungano, Makamo wa Rais awe ni mtu anayetoka upande wa pili wa Muungano.
3.3.2 Suala ni kuwa mtu anayetoka upande mmoja wa Muungano ni sifa ya uzawa, ukaazi au ya mahusiano? Mtu anaweza, kwa mfano kutoka Zanzibar kwa sababu ya kuzaliwa ama kwa sababu ameishi Zanzibar au kwa sababu wazazi au mmoja wa wazazi wake ametoka Zanzibar lakini yeye mwenyewe hajazaliwa wala hajawahi kuishi Zanzibar.
3.3.3 Nafasi ya Urais (iwe Rais au Makamo) ni muhimu katika Muungano, Ni moja ya nguzo zake kuu. Aidha Katiba ndio muongozo wa uteuzi wake. Hivi sasa kuna madai kuwa hakuna utaratibu wa kubadilishana zamu za Urais baina ya Bara na Zanzibar kwa vile haijaelezwa ndani ya Katiba wala Sheria yoyote. Kutokana na utaratibu uliopo (angalau ndani ya CCM) ya uteuzi wa mgombea Urais, tunaanza kuandika Kanuni kuwa Zanzibar itaendelea kutoa Makamo wa Rais.
Lakini kwa vile maana ya mtu anyetoka upande mmoja wa Jamhuri ya Muungano hajafafanuliwa ndani ya Katiba, kesho itakuja Hoja kuwa neno hilo halikutafsiriwa ndani ya Katiba wala Sheria, hivyo sifa moja yoyote ya uzawa, ukaazi au uhusiano inafaa. Sijui kama kuanzia hapo patakuwa tena na Muungano huu tunaoujua leo. Njia rahisi ilikuwa ni kusema kwamba mtu anayetoka Zanzibar ni yule ambaye ana sifa ya kuwa Mzanzibari chini ya Sheria za Zanzibar.
3.3.4 Serikali ya Muungano ilikataa wazo hilo kata kata wakati wa kujadili Muafaka baina ya SMZ na SMT hapo mwaka 1994. Kamati ya Shellukindo iliwahi hata kupendekeza Sheria ya Mzanzibar ifutwe kwa vile inatoa dhana ya uraia wa aina mbili (Angalia uk. 10 – Dondoo 2.6 la Ripoti ya Shellukindo). Serikali ya Muungano hata hivyo katika muafaka wa 1994 ilikubali kuwa kuifuta Sheria hiyo ni makosa, na hivyo iendelee kuwepo kwa vile ndiyo inayofafanua nani ana haki ya kuchagua na kuchaguliwa katika uchaguzi wa Zanzibar. (Angalia uk. 10 – Dondoo 2.2.2.1 ya Taarifa ya Muafaka).
Hivyo suala hili muhimu halina majibu ndani ya Katiba na Sheria zetu na ni wazi kuwa ni mbegu ya mzozo wa baadae.