3.2 NINI MAANA YA JAMBO LA MUUNGANO
3.2.1 Suala hili lina sehemu mbili zifuatazo:
(a) Mambo ya Muungano ni mangapi; na
(b) Jambo linapoitwa ni la Muungano maana yake ni nini.

Mambo ya Muungano ni Mangapi:
3.2.2 Jibu rahisi kwa watu wengi kuhusiana na suala hili ni kuwa mambo ya Muungano ni 22 kama yalivyoainishwa na Katiba ya Muungano katika Jedweli la Kwanza. Lakini hata Jadweli hilo limeorodhesha zaidi ya mambo 22 kama ifuatavyo:
(i) Katiba ya Muungano
(ii) Mambo ya nje
(iii) Ulinzi
(iv) Usalama
(v) Polisi
(vi) Hali ya Hatari
(vii) Uraia
(viii) Uhamiaji
(ix) Mikopo ya Nje
(x) Biashara
(xi) Utumishi katika Serikali ya Muungano
(xii) Kodi ya Mapato
(xiii) Forodha (Ushuru)
(xiv) Kodi ya Bidhaa (exercise)
(xv) Bandari
(xvi) Usafirishaji wa Anga
(xvii) Posta
(xviii) Simu
(xix) Sarafu
(xx) Mabenki
(xxi) Fedha za Kigeni
(xxii) Leseni za Viwanda
(xxiii) Takwimu
(xxiv) Elimu ya Juu
(xxv) Mafuta yasiyosafishwa
(xxvi) Gesi asilia
(xxvii) Baraza la Mitihani
(xxviii) Usafiri wa Anga
(xxix) Utafiti
(xxx) Mahakama ya Rufaa
(xxxi) Usajili na Shughuli za Vyama vya Siasa

3.2.3 Pamoja na Orodha hiyo jadweli ya Pili, Orodha ya Pili inaeleza kwamba, Bunge lilipotaka kubadili masuala yanayohusiana na Mamlaka ya Serikali ya Zanzibar na suala la Mahakama Kuu ya Zanzibar – lazima yakubaliwe na theluthi mbili ya Wabunge wa Tanzania Bara na theluthi mbili ya Wabunge wa Zanzibar. Suala hapa ni kuwa kwani hayo ni mambo ya Muungano?

3.2.4 Dalili ya pili inaonyesha kwamba Mambo ya Muungano hayajulikani ni mangapi ni kuwa yapo mambo yanayofanywa kimuungano pamoja na kwamba si ya Muungano (kama vile Bima – inayosimamiwa na Kamishna ya Bima). Aidha yapo mambo ya Muungano ambayo hayasimamiwi kimuungano kama vile Takwimu (isipokuwa sensa ya Idadi Watu), Bandari na Leseni za Viwanda.

3.2.5 Dalili ya tatu ni kuwa Bunge limekuwa likitunga Sheria na kuzifanya za Muungano hata kwa mambo ambayo hayamo katika orodha ya Muungano. Mfano ni Sheria ya Proceeds of Crimes Act ya 1991.

3.2.6 Dalili ya nne ni kuwa kuna baadhi ya maeneo ambayo Serikali zenyewe (pamoja na Wanasheria Wakuu) hazikubaliani kama ni ya Muungano au si ya Muungano. Maeneo hayo ni kama vile “Deep Sea Fishing Authority”, na Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora. Aidha suala la Ushirikiano wa Kimataifa.

3.2.7 Dalili ya Tano ni kuwa hata kwa yale mambo ambayo yamo katika Orodha ya Mambo ya Muungano, mengi hayana tafsiri na hivyo hayajulikani mipaka yake. Mifano ni kama vile Elimu ya Juu (inaanzia wapi inaishia wapi?), Usalama (Jee ni ule wa hata kuweka “watchman”) jee Serikali ya Zanzibar haina siri zake peke yake ambazo hazipaswi kujulikana na Serikali ya Muungano na hivyo kuwa na taratibu zake za usalama? Mikopo ya Nje, Biashara za Nje. Posta na Simu jee ni miundo mbinu au udhibiti (regulatory aspect).

3.2.8 Dalili au hoja ya Sita ni kuwa jee mambo yasiyo ya Muungano ya Tanzania Bara pekee nayo ni ya Muungano au si ya Muungano? Hili linaonekana kama suali la kijinga mno, lakini ndio suali gumu hata kwa wanaojiona werevu mno. Hakuna ubishi kuwa jambo lisipokuwa la Muungano Zanzibar inaweza kulisimamia wenyewe, lakini kuna matatizo kwa upande wa Tanzania Bara.

3.2.9 Baadhi ni kama yafuatayo:
(i) Bajeti: Zipo baadhi ya Taasisi za Muungano ambazo zinafanya kazi za Muungano na sizizo za Muungano – kwa mfano Bunge linatunga Sheria na kusimamia mambo ya Muungano na yasiyo ya Muungano. Vivyo hivyo kwa ‘Executive’ na Judiciary ya Muungano. Hivi gharama zake zitoke wapi? Kwa sasa Bunge na Executive inajulikana kuwa ni za Muungano, hivyo igharamiwe na Mfuko wa Muungano?

(ii) Taasisi zisizo za Muungano ndizo zinazoiwakilisha Zanzibar nje kwa jina la Tanzania mfano Kilimo, Kazi, Utalii na hata Tanzania Football Federation. Hivyo suala linakuja ni wakati gani taasisi ya Tanzania Bara isiyokuwa ya Muungano inakuwa sio ya Muungano?

3.2.10 Majibu ya maswali yote hayo hayamo katika Katiba wala Sheria zetu wakati ni mambo ya msingi na ndio uti wa mgongo wa Muungano.