3.1 SUALA LA KWANZA: JE WASHIRIKI WA MUUNGANO BADO WAPO AU HAWAPO?
3.1.1 Suala hili ni la msingi kwa vile nchi ambazo zimeungana kwa baadhi ya mambo tu, inategemewa kwamba waliounganisha mambo hayo wapo, wana vikao rasmi vinavyotambuliwa na Katiba na Sheria za Nchi. Ilitegemea kuwa Washirika hao wanaamua kuongeza kupunguza mambo ya Muungano wakiwa na nguvu sawa ya uamuzi. Ilitegemea kuwa Washirika hao wana kauli sawa za maamuzi juu ya sera, uendeshaji na Sheria za Muungano. Suala ni kuwa hivi ndivyo hali ilivyo?

3.1.2 Suala hili kila mtu anaweza kuwa na maoni na fikra zake, lakini sio jibu na wala huwezi kupata jibu ndani ya Katiba, Sheria na Sera za Muungano. Sababu zinazoonyesha kuwa hakuna jibu la suali hili ni zifuatazo:

(a) Wengi wanadhani kuwa Zanzibar ipo na ni Tanganyika tu ndio haipo – lakini ukweli Zanzibar haipo katika Muungano. Wengine wanahisi Tanganyika ipo ndani ya Muungano ikivaa koti la Muungano lakini hata hilo haliko wazi kama iliomo ndani ya Muungano ni Tanganyika au nalo ni koti tu la Tanganyika.

(b) Hakuna Kikao kinachotambulika kisheria kinachozikutanisha pande mbili za Muungano.

(c) Mambo ya Muungano kiutawala na kisera yanaamuliwa na Baraza la Mawaziri la Serikali ya Muungano. Zanzibar haiwakilishwi ndani ya Baraza hilo. Rais wa Zanzibar anaingia kama Mjumbe wa Baraza la Mawaziri na sio kama upande mmoja wa chombo hicho ambao unaruhusiwa kutetea msimamo wa Zanzibar. Hivyo ndani ya Baraza Rais wa Zanzibar haiwakilishi Zanzibar kwa vile akiwa ndani ya Baraza hilo anawajibika kwa Rais wa Muungano na sio kwa mamlaka yoyote ya Zanzibar. Mawaziri ambao ni Wazanzibari nao hawawakilishi Zanzibar bali ni Mawaziri sawa na wengine ambao wanafungwa na Kanuni ya kuwajibika kwa pamoja (Collective responsibility). Hivyo lazima wakubaliane na maamuzi ya wengi na kwa vyovyote vile hawamo ndani ya Baraza kuiwakilisha Zanzibar.

(d) Inapotokea Rais wa Muungano au Makamu wa Rais anatoka Zanzibar – je, anaiwakilisha Zanzibar? Ameteuliwa na Zanzibar kama mshirika wa Muungano kuiwakilisha? Anayo haki na uwezo wa kisheria wa kutetea maslahi ya mmoja wa Washiriki ndani ya Muungano ambayo ni Zanzibar. Jibu ni kuwa Makamo wa Rais wala Rais anapotokea kutoka Zanzibar haiwakilishi Zanzibar ndani ya Muungano bali anatumia fursa yake kama Mtanzania kushika nafasi hiyo. Hapaswi na hana uwezo wala wajibu wa kutetea Zanzibar ndani ya Muungano.

(e) Katika kutunga Sheria za Muungano Zanzibar kama mshirika inawakilishwa? Takribani Sheria zote za mambo ya Muungano zinapitishwa kwa wingi wa Kura. Kwa vile idadi ya wabunge kutoka Zanzibar takriban ni robo tu ya Wabunge wa Bunge la Muungano ni wazi kuwa Zanzibar kupitia Wabunge hao haina kauli katika kutunga Sheria za Muungano. Ni mambo yale tu yaliyoainishwa katika Orodha ya Pili ya Jadweli ya Pili ya Katiba ya Muungano ndio yanayoamuliwa kwa kauli sawa. Kichekesho ni kuwa kati ya mambo hayo 8 yaliyoorodheshwa baadhi sio mambo ya Muungano.

(f) Inapotokea Zanzibar kushirikishwa kama Zanzibar katika masuala ya Muungano ni kwa njia ya SMZ kutakiwa kutoa maoni. Hata hivyo, maoni hayo ya SMZ ambayo baadhi ya wakati huandaliwa na Baraza la Mapinduzi, mara nyingi hukataliwa na hata Mkurugenzi tu wa Serikali ya Muungano au Katibu Mkuu au Waziri. Baadhi ya mifano mashuhuri ambapo maoni ya Zanzibar hayakuzingatiwa katika masuala muhimu ya Muungano ni:

(i) Katika uanzishaji wa Benki Kuu, mwaka 1965 na marekebisho ya Benki Kuu, 1995.
(ii) Uanzinshwaji wa Mamlaka ya Mapato TRA.
(iii) Katika suala la Jumuiya ya Afrika Mashariki.
(iv) Sera ya Mambo ya Nje
(v) Uraia na Uhamiaji na
(vi) Sheria ya Deep Sea Fishing Authority.

(g) Kwa upande wa pili, ingawa tunasema kuwa Tanganyika imevaa koti la Muungano lakini suala bado linabaki, kuwa Tanganyika (T/Bara) kama mshirika wa Muungano ipo. Jee Serikali ya Muungano kweli inawakilishwa na kutetea maslahi ya Tanganyika ndani ya Muungano na kwa utaratibu gani?