JUHUDI MAHSUSI ZA SMT NA ZA SMZ
2.7 SMZ peke yake ama kwa kushirikiana na Serikali ya Muungano, zimechukua hatua kadhaa za kutafuta ufumbuzi wa Kero za Muungano. Kwa upande wa SMZ, miongoni mwa hatua ilizochukua na ambazo zinajulikana ni
pamoja na kuunda Kamati mbali mbali. Miongoni mwa Kamati zilizoundwa na SMZ kushughulikia Kero za Muungano kati ya mwaka 1990 na 2003 ni pamoja na ziufatazo:

(a) Kamati ya Baraza la Mapinduzi (Kamati ya Amina) ya 1992.

(b) Kamati ya Rais ya Kupambanua na Kasoro za Muungano (Kamati ya Shamhuna, 1997).

(c) Kamati ya Rais Kuchambua Ripoti ya Kisanga (Kamati ya Salim Juma).

(d) Kamati ya Rais ya Kuandaa Mapendekezo ya SMZ juu ya Kero za Muungano. (Kamati ya Ramia, 2000).

(e) Kamati ya BLM juu ya Sera ya Mambo ya Nje.

(f) Kamati ya Rais ya Wataalamu juu ya Kero za Muungano (2001).

(g) Kamati ya BLM ya Jamuiya ya Afrika Mashariki.

(h) Kamati ya Mafuta

(i) Kamati ya Madeni baina ya SMZ na SMT.

(j) Kamati ya Suala la Exchusive Economic Zone (EEZ)
(k) Kamati ya Masuala ya Fedha na Benki Kuu.

(l) Kamati ya Rais ya Masuala ya Simu – (1996 – 1999)

SMZ pia imewahi kuajiri mtaalamu wa mambo ya fedha, Dr. Courtrey Blackman na Mtaalam wa masuala ya mafuta.

2.8 Mbali ya baadhi ya Kamati hizo za SMZ peke yake, SMT na SMZ zimeunda Tume, Kamati na Kuajiri Wataalamu mbali mbali ili kutafuta suluhisho la Kero mbali mbali za Muungano. Miongoni mwa Tume na Kamati hizo ni kama zifuatazo:

(a) Kamati ya Mtei
(b) Tume ya Nyalali
(c) Kamati ya Shellukindo
(d) Kamati ya Bomani
(e) Kamati ya Shellukindo 2, ya kuandaa Muafaka juu ya Mambo ya Muungano baina ya SMZ na SMT.
(f) Kamati ya Harmonisation.
(g) Kamati ya Masuala ya Simu (Kamati ya Kusila)

Aidha SMZ na SMT zimefanya vikao vya pamoja visivyopungua 80 katika ngazi mbali mbali ili kuzungumzia Kero za Muungano. Aidha Serikali hizi mbili mwaka 1994 ziliomba msaada wa IMF ili kuzishauri kuhusiana na Benki Kuu, mgawano wa Misaada na uhusiano wa kifedha (intergovernmental fiscal relationship).

2.9 Mbali ya juhudi zote hizo, tarehe 14 Novemba, 2000 wakati Rais Benjamin Mkapa alipokuwa akizundua Bunge aliahidi kuzipatia ufumbuzi Kero za Muungano ndani ya siku 60!! Tokea ahadi ilipotolewa hadi leo ni siku 1620 – yaani siku 60 zimepita mara 27.

2.10 Pamoja na hatua zote hizo zilizoambatana na masikitiko ya Viongozi wa juu, manung’uniko ya wananchi wa pande zote mbili juu ya uendeshaji wa Muungano na ahadi nzito za viongozi wa juu wa Serikali za kuondoa kasoro za Muungano – lakini bado Kero au Kasoro hizo zipo pale pale au zimezidi zaidi.

Cha kusikitisha zaidi kuwa baadhi ya Kero zilizozungumzwa mwaka 1984 katika vikao vya pamoja ndizo Kero hizo hizo zilizozungumzwa katika Ripoti ya Shellukindo ya 1992 na katika Muafaka baina ya SMZ na SMT wa mwaka 1994 na ndizo hizo hizo zilizozungumzwa katika Ripoti ya Kamati ya Wataalamu ya SMZ ya 2001.

Suala muhimu ni kuwa ni kwa nini juhudi zote hizo zimeshindwa? Jibu langu ni kuwa Muungano una Kasoro za maumbile, za kuzaliwa nazo!!

2.11 Suala muhimu ni kuwa ni vipi tutaweza kuzibaini Kasoro hizo za Maumbile katika Muungano? Jibu ni kuwa baadhi ya kasoro hizo hazitaki utaalamu kuziona. Hata hivyo kwa sababu kasoro nyingi za Muungano ziko wazi na zimeshazungumzwa mara nyingi, wengi wamezizoea na kuona kwamba kasoro ni sehemu ya Muungano.

Lakini tunaposogea mbele zaidi na kujiuliza ni kwa nini Kero za Msingi Muungano zimeshindwa kupatiwa ufumbuzi pamoja na juhudi na ahadi nzito za viongozi, nadhani jibu si kuwa Kero hizo zimezoeleka au kuwa ni sehemu ya Muungano. Tunapaswa tujiulize zaidi nini kiini cha tatizo. Wengi wana maoni kuwa kiini cha tatizo ni mfumo wa Serikali mbili. Ingawa mfumo huo kweli umechangia, lakini hilo bado ni jibu rahisi kwa suala zito (gumu) – “it is an oversimplified answer to a very complicated question”.

2.12 Kwa maoni yangu, tatizo la msingi ni kuwa kila uhusiano baina ya watu una Kanuni za msingi zinazoongoza uhusiano huo (“basic principles” au “grundnorm” za uhusiano). Aidha kuna mipaka ya uhusiano (parameters). Nyenzo za uhusiano kama vile nyaraka na sera lazima ziwe na uwezo wa kujibu maswali ya msingi kuhusiana na uhusiano huo.

2.13 Katika Muungano wa Tanzania, Zanzibar na Tanganyika ziliungana kwa baadhi ya mambo tu na sio mambo yote na ndio maana kuna orodha ya mambo ya Muungano. Aidha ibara ya 64 ya Katiba ya Muungano inaeleza wazi kuwa Bunge halina mamlaka ya Kutunga Sheria kwa mambo ya Zanzibar yasiyokuwa ya Muungano.

Hivyo ilitarajiwa kwamba, kwa vile pande hizi zimeungana kwa baadhi ya mambo tu Kanuni ya msingi ni kuwa pande hizo lazima ziwe na kauli sawa kuhusiana na Mambo ya Muungano katika Sera, Utawala na katika kuyatungia Sheria. Aidha ziwe na kauli sawa katika kuongeza na kupunguza mambo ya Muungano na Katiba iweke bayana jambo hilo.

Katika Muungano wa Kikatiba au wa kisiasa, Katiba au Mkataba wa Muungano, Sheria na Sera za Muungano ndio nyenzo kuu. Iwapo nyenzo hizo zinashindwa kutoa majibu kwa masuala ya msingi kuhusiana na Muungano ni kielelezo tosha kuwa Muungano huo una kasoro za maumbile. Kasoro hizo ni pamoja na kutokuwa na Kanuni za Msingi na kutokuwepo Mipaka katika Waraka huu tutaeleza Masuali ya Msingi ambayo hayana Majibu katika Katiba, Sheria na Sera za Muungano.

3.0 MASUALA YASIYO NA MAJIBU