2.0 JUHUDI ZA KUONDOA KERO ZA MUUNGANO
2.1 Katika kutekeleza shughuli za Muungano matatizo kadhaa yamejitokeza ambayo yamepelekea kuwepo zinazoitwa Kero za Muungano.

Tatizo la siku za mwanzo kabisa la Muungano lilijitokeza mwaka 1965 wakati jambo jipya la Muungano lilipoongezwa katika orodha ya mambo ya Muungano; inaonyesha bila ya makubaliano baina ya Serikali hizi mbili. Mawasiliano yaliopo katika kumbukumbu baina ya Waziri wa Fedha wa Zanzibar na Waziri wa Fedha wa Serikali ya Muungano yanaonyesha kuwa mawazo ya Serikali ya Zanzibar katika uundaji wa Benki Kuu hayakusikilizwa.

Baada ya muelekeo wa kuwa na Shirikisho la Afrika Mashariki kufifia, nchi za Afrika Mashariki zikitanguliwa na Uganda zilichukua hatua za kuanzisha Benki Kuu zao hata kabla ya kuivunja rasmi Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki. Katika hali hiyo ndipo Serikali ya Muungano ilipochukua hatua za haraka za kuanzisha Benki Kuu ya Tanzania bila ya maafikiano rasmi na Zanzibar na hivyo kupelekea Zanzibar kukosa haki zake katika Bodi ya Sarafu na ndani ya Benki Kuu ya Tanzania.

Kutokana na hatua hiyo Rais wa Zanzibar Sheikh Abeid Amani Karumed aliunda Kamati ya watu 12 ikiongozwa na mtaalamu wa Masuala ya Benki Bw. E. Ebert ili kuishauri Serikali juu ya kuanzisha Benki ya Serikali ya Zanzibar. Kamati hiyo iliwasilisha ripoti yake mwishoni wa mwaka 1965. Ripoti hiyo pamoja na mambo mengine ilipendekeza kuwa Benki hiyo iwe ndio Benki ya Serikali na itumike kusimamia hesabu za (Accounts) Serikali.

Kamati ilipendekeza hadi ifikapo July, 1966 ‘accounts’ zote za Serikali ziwe zimehamishiwa Benki hiyo. Hapondipo ilipoanzishwa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) ambayo iliendelea kuwa ndio Benki ya SMZ hadi mwaka 2001 wakati Benki Kuu ya Tanzania ilipoanza rasmi kuwa Benki inayotumiwa na Serikali ya Zanzibar. Hivyo pamoja na kuwepo Benki Kuu kama chombo cha Muungano lakini kuanzia awamu ya kwanza hadi ya Tano za Serikali ya Zanzibar, haikutumia Benki hiyo. Serikali ya Muungano ilikuwa siku zote ikililalamikia jambo hilo.

2.2 Wakati wa Awamu ya Pili ya Serikali ya Zanzibar, matatizo ya Muungano yalijitokeza zaidi. Rais Aboud Jumbe alionekana dhahiri kutoridhishwa hata kidogo na mwenendo wa Muungano. Mbali ya kutafuta mtaalamu wa Sheria kutoka Ghana, Bw. Bashir Swanzi ili kujenga Hoja ya kukiukwa kwa Katiba ya Muungano na kupendekeza hatua za kisheria za kuondoa kasoro hizo, hatua iliyopelekea kuanguka kwake katika Uongozi, lakini yeye binafsi alichukizwa sana na mambo ya Muungano yanavyoendeshwa bila ya kufuata Katiba na ‘sprit’ ya Muungano. Katika moja ya mawasiliano yake ya kiserikali ya tarehe 23 Oktoba, 1983 aliwahi kuandika yafuatayo:

“Kosa moja ambalo linaendelea kufanywa ni lile la kudhani kwamba kuimarisha Muungano kuna maana moja na kuhaulisha shughuli zisizokuwa za Muungano ziwe za Muungano na kwamba Chama na Serikali ya Muungano wanaweza kufanya hivyo – bila ya kuzingatia Katiba wala hisia au matakwa ya Zanzibar.

Dhana hizo ni ama ni za kupotosha kusudi kwa sababu wanazozielewa wenyewe wafanyao hivyo, au ni kukataa kuelewa Katiba. Vyovyote vile ilivyo ni mashaka.

Kisheria shughuli yoyote isiyo ya Muungano haiwezi kufanywa iwe ya Muungano bila ya ridhaa ya Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Tanganyika au na Serikali ya Muungano kwa niaba ya Tanzania Bara. Mpango wa Serikali ya Muungano kuwakilisha pia Tanzania Bara umeleta fadhaa na wasiwasi wa kutosha katika miaka kadhaa, hasa ya hivi karibuni.

Hata kingekuwa Chama au Serikali ya Muungano vingeweza Kikatiba kufanya hivyo, na haviwezi , basi lingelikuwa ni kosa la uadilifu na pia la kisiasa kufanya hivyo, bila ya ridhaa na makubaliano ya pande zote mbili za Muungano, wala hicho kisingekuwa kitendo cha kuimarisha, bali cha kudhoofisha na hata kupotosha dhamiri na maana ya Muungano.

Najua baadhi wana mashaka na kimya changu na wangependa kujua msimamo wangu juu ya suala hili la masahihisho ya Katiba. Msimamo haunihusu kwa sasa, jambo la msingi ni kwamba lazima Katiba ziheshimiwe, maadili yafatwe na dhamiri ya Muungano ihifadhiwe. Dhamiri lazima siku zote ibaki kuwa ni zao la nidhamu ya hali ya juu kabisa.

Muungano au Umoja hauwezi kuimarishwa kwa upande mmoja kutwaa madaraka ambayo ni ya pande mbili za umoja huo. Ikiwa wote tutatekeleza wajibu wetu kwa dhati, haki haitakuwa mbali kuonekana na kila upande utakuwa na utaridhika na haki yake. Huko ndiko kuimarisha Muungano”.

Hii ni ushahidi wa wazi kuwa pamoja na viongozi wakuu wa Muungano kuupenda Muungano lakini waliona kasoro za wazi za utekelezaji wa Muungano zaidi ya miaka 20 iliyopita.

2.3 Katika Awamu ya Tatu na Nne mbali ya mambo ya Muungano kuongezeka, juhudi za kusawazisha kasoro za Muungano ziliendelea. Njia kubwa iliyotumika ilikuwa ile ya vikao vya pamoja baina ya Serikali ya Muungano na Zanzibar. Vikao hivyo vikiongozwa na Waziri Mkuu na Waziri Kiongozi.

2.4 Katika Awamu ya Tano, kama tutavyoona hapo baadae, Serikali ilichukua hatua nyingi zaidi kuliko awamu yoyote kushughulikia kasoro za Muungano. Dr. Salmin Amour hakuwa akificha hisia zake za kutoridhishwa na utekelezaji wa Muungano. Miongoni mwa mambo aliyoyawekea msimamo wazi wa kutaka kuwe na uwazi na masawazisho ni masuala ya uchumi, kupunguzwa mambo ya Muungano yasiyo ya lazima na suala la Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kuna taaarifa za kuaminika kuwa wiki chache kabla ya kutiwa saini Mkataba wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, Rais Salmin Amour alimuandikia Waraka maalum Rais Benjamin Mkapa, kueleza msimamo na mtazamo wa Zanzibar juu ya uwakilishi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Jambo ambalo nina hakika ni kuwa Waraka huo wa kurasa 10 wenye maoni na mtazamo wa Zanzibar haukushughulikiwa hadi leo!!

2.5 Awamu ya Sita ya Serikali ya Zanzibar inajulikana wazi kwa msimamo wake juu ya suala la uchimbaji wa mafuta – msimamo ambao iliurithi kutoka Awamu ya Tano. Mbali ya suala hilo, iliunda Kamati ya Wataalamu katika siku za mwanzo za kuingia madarakani. Kamati ilichambua kasoro za Muungano na kupendekeza mambo ya kubaki katika Muungano, mambo ya kupunguzwa, mambo ya kuongezwa na utaratibu wa kuendesha masuala ya Muungano kisera, kiutawala na katika kutunga Sheria za Muungano.

Miongoni mwa mapendekezo mahsusi ya Kamati ilikuwa ni pamoja na kuwa Bunge la Tanzanzia liwe na sehemu mbili – ‘Lower house’ itayoshughulikia mambo yasiyo ya Muungano ya Tanzania Bara na ambapo Wabunge wa Zanzibar hawatoshiriki na “Upper House” ambayo itashughulikia mambo ya Muungano tu na itakuwa na uwakilishi sawa baina ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Aidha Kamati ilirudia mapendekezo ya Bomani ya kuwa na Baraza la Taifa (Council of State) ingawa kwa muundo tofauti. Baraza hilo kazi yake ni kushughulikia mambo ya Muungano kisera na kiutawala. Kamati iliwasilisha Ripoti yake Serikalini mwezi March, 2001. Kwa kadri ya ninavyoelewa hakuna hata moja katika mapendekezo ya Kamati, na ambayo yalikubaliwa na Serikali lililofanyiwa kazi. Eneo jengine lilofanyiwa kazi na Awamu ya Sita ni masuala ya fedha – Benki Kuu na Tume ya Pamoja ya Fedha.

2.6 Maelezo hayo yanathibitisha mambo mawili:-
(a) Muungano una kasoro za msingi
(b) Juhudi za kuondoa kasoro hizo zinazofanywa na viongozi wa SMZ hazijawa na mafanikio ya maana