1.0 UTANGULIZI
Tokea kuasisiwa hapo Aprili 26, 1964 Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao ndiyo uliozaa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania umekuwa na sifa mbili kuu.

Sifa moja ni ile ya kuwa nyenzo au kitambulisho cha umoja wa kitaifa Tanzania, na hivyo wale wanaojinadi kwa uzalendo na hisia za umoja wa kitaifa wamekuwa wakijinasibisha na kuupenda mno Muungano na kuahidi kuulinda kwa gharama zozote. Mapenzi haya ya Muungano yamesababisha hata Katiba ya Jamhuri ya Muungano kuwa na kifungu mahsusi cha kuwataka Viongozi wa Kitaifa (Rais wa Jamhuri ya Muungano, Makamo wa Rais, Waziri Mkuu na Rais wa Zanziba) kula kiapo cha kuulinda Muungano kabla ya kuanza kazi zao (Kifungu cha Katiba ya Muungano).

Aidha, Sheria ya Vyama vya Siasa inakiondolea sifa ya kutosajiliwa chama chochote cha siasa ambacho Katiba yake au sera zake ni za kutaka kuvunja Muungano. Hii ni kusema kwamba Katiba na Sheria zetu zinakataza wananchi kuwa na mawazo ya kuvunja Muungano. Huu ni ulinzi na mapenzi makubwa kwa Muungano.

Sifa ya pili ni kuwa Muungano umekuwa ni kitu kinachotambuliwa na kukubaliwa na wale ‘WANAOUPENDA’ na “WASIOUPENDA” kwamba una kasoro nyingi – lugha ya siku hizi huitwa KERO za MUUNGANO. Fedha, wataalamu na muda mwingi umetumika katika kutafuta suluhisho la kasoro au kero hizo, lakini mafanikio yamekuwa madogo mno (kama yapo). Kuna wanaosema kuwa Kasoro au Kero za Muungano zimekuwa zikiongezeka badala ya kupungua. Wanaosema hivyo mimi nawaunga mkono.

Naamini yeyote atayetafakari kwa makini atawaunga mkono. Hivyo, suala la msingi ni kwa nini kipenzi hiki cha Taifa la Jamhuri ya Muungano kinachoitwa MUUNGANO ambacho sote tunakubali kuwa kinaumwa tokea uchanga wake hadi leo, miaka 41 tokea kizaliwe, kimeshindwa kupatiwa dawa pamoja na Tanzania kuwa na mabingwa wa dawa za kisiasa na pamoja na juhudi kubwa za mabingwa hao bado MUUNGANO unaumwa zaidi. Wapo wanaodai kuwa dawa ipo na inajulikana, lakini pengine inaonekana ni chungu sana kupewa kipenzi hicho cha Watanzania!

1.2 Ni maoni yangu kwamba MUUNGANO una kasoro za msingi za kimaumbile. Kasoro hizo ni miongoni mwa sababu za MUUNGANO kuwa na KERO sugu. Kasoro hizo za maumbile ni kuwapo kwa masuala ya msingi ya kikatiba ambayo hayana majibu ama kutoka ndani ya Katiba, Sheria, Sera na hata kutoka kwa watendaji.

1.3 Katika Waraka huu nitajaribu kueleza juhudi mbalimbali za kuondoa Kero za Muungano ambazo zimeshindwa kuondoa Kero hizo. Juhudi hizo na kushindwa kwake ni kielelezo cha kuwepo kwa kasoro za maumbile katika Muungano. Aidha nitaeleza baadhi ya Masuala yasiyo na Majibu katika Muungano. Maswali hayo ni kielelezo cha kasoro za maumbile na ni miongoni mwa sababu za kushindwa kupatiwa dawa KERO za Muungano. Kwa kuelewa mambo hayo mawili pengine itatusaidia sote kwa pamoja kutoa mapendekezo ya kusawazisha KERO za Muungano.