Baada ya panguapangua mkoani Morogoro iliyogusa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mkuu wa Wilaya ya Malinyi na Mkurugenzi wa Maendeleo (DED) wa Wilaya ya Malinyi, nikakumbuka makala niliyoiandika takriban miaka miwili iliyopita.

Kwenye makala hiyo nilisema Charles Keenja aliongoza vizuri sana Tume ya Jiji la Dar es Salaam. Alifanya mambo mengi, makubwa na mazuri ambayo hadi leo sijaona yakitendwa na kiongozi wa Jiji. Yeye ndiye aliyeasisi shule za kata, akaleta mfumo wa usafi kwa kushirikisha kampuni binafsi. Akajenga majengo na uzio kwenye maeneo mengi. Kituo cha Mabasi Ubungo ni matokeo ya uongozi wake. Aliyafanya hayo akiwa na wakurugenzi tu. Hakuwa na diwani wala nani.

Baadaye akawania ubunge Ubungo. Akaupata. Akapelekwa kuongoza Wizara ya Kilimo na Chakula. Wengi wakatarajia atafanya aliyofanya jiji. Haikuwa kweli. Akashindwa kufurukuta. Hakuleta mabadiliko ya kupigiwa mfano. Kwanini alifeli? Keenja hakufeli kama yeye. Alifelishwa na mfumo alioukuta. Mfumo uliojikita kwenye urasimu na uliolindwa na misingi iliyowekwa tangu Uhuru ya ‘Ugumu wa kumwajibisha mtumishi’.

Nikasema leo Rais Magufuli anaweza kuona mawaziri wake kadhaa hawafai. Hawatendi kama anavyotaka. Kweli wapo wengine wanatimiza wajibu tu wa idadi, lakini wapo wanaokwama kwa sababu ya mfumo wanaokutana nao.

Rais amedhamiria kuibadili Tanzania. Kwenye mabadiliko hayo, mojawapo ni kuona mambo yakienda kwa spidi ya ‘supasoniki’. Dhamira hiyo itatimia endapo ataamua kufumua mifumo yote iliyoshindwa kuleta tija tangu Uhuru.

Bila kuifumua, tutaendelea kulia na wezi wa fedha za umma hasa kwenye halmashauri, wazembe, wasiowajibika, majizi na kila aina ya wahalifu. Tutaendelea kuwaona mawaziri, makatibu wakuu, ma-DC, ma-DED, ma-DAS, ma-RC, ma-RAS na kadhalika wakikwama.

Zawadi nyingine nzuri kati ya zawadi nyingi ambazo Rais Magufuli anawaandalia Watanzania, asisahau kutuachia zawadi ya kuufumua mfumo wa uongozi katika taifa letu.

Tuone kama kuna ulazima bado wa kuendelea kuwa na mlolongo wa vyeo kuanzia chini kabisa hadi taifa. Tujiulize, mlolongo huu unasaidia au unakwamisha maendeleo?

Rais Magufuli ajitahidi kuleta mfumo wa utendaji kazi serikalini utakaoshabihiana na ule ulioko kwenye sekta binafsi. Walioko kwenye sekta binafsi wanajua hakuna ‘kuchekeana’. Hakuna udhuru usio na ukomo au maelezo yanayojitosheleza. Sekta binafsi kumtumbua mzembe asiyezalisha ni kazi ya dakika tu.

Bila kuufumua mfumo huu wa sasa, Rais Magufuli na watakaokuja baada yake, wote watakuwa na malalamiko yanayofanana. Muhimu ni kupangua mfumo wa sasa na kuleta mfumo mpya wenye sifa na mwonekano wa utendaji kazi unaokaribiana na wa sekta binafsi.

Leo kuna mambo yanakwenda kwa sababu tuna rais anayepambana ili yaende. Haya mambo yanayokwenda, hayaendi kwa sababu ya mfumo, hapana. Yanakwenda kwa sababu yupo kiongozi mkuu na baadhi ya wasaidizi wake wakubwa walioamua mambo yaende! Mara nyingi mifumo ya aina hii huondoka pindi walioko madarakani wanapoondoka.

Kilichotokea Morogoro wiki iliyopita kinaakisi haya niliyoyasema miaka miwili iliyopita, na ambayo  kwa kweli kutokana na mapenzi yangu kwa nchi yangu nitaendelea kuyawasilisha kwa viongozi wetu.

Tunapoona DED na DC wanasuguana kwa sababu ya mradi fulani wenye ulaji, tujiulize kinachowafikisha hapo ni kitu gani? Ni fedha tu? Hapana. Shida kubwa hapa ni kuwa wote hawa wawili ni wateule wa rais.

DC anajiona kuwa ndiye ‘rais’ wa wilaya; DED anajiona ndiye ‘bwana/bibi fedha wa wilaya’. DC anatajwa kuwa na mamlaka ya mwakilishi wa rais, lakini huwezi kuwa mwakilishi wa rais kama huna nguvu ya kifedha na mamlaka; na mbaya zaidi ni kuwa wote ni wateule wa rais.

DED anapoamini kuwa DC hawezi kumtisha, au RAS anapokuwa na hakika kuwa RC hana ubavu wa kumwajibisha, hapo tusitarajie muujiza wa uwajibikaji. Ndiyo maana wapo walioliona tatizo hilo na kushauri mamlaka ya kikatiba aliyonayo rais ya kuteua wasaidizi wake yatazamwe upya ili baadhi ya uteuzi ufanywe na mamlaka nyingine zilizo chini ya rais. Kwa maneno mengine, hali ilivyo sasa ni kama wateule wote wana ‘sharubu’, maana wameteuliwa na mamlaka moja.

Kwa mfumo wa sasa, DC hana mamlaka ya kumkabili hata mtendaji wa kijiji; na ndiyo maana rungu pekee walilobaki nalo ni kuwaweka rumande viongozi wa kada hiyo na watumishi wengine wa umma.

Aina hii ya mfumo tuliyonayo ndiyo imemfanya rais wetu awe kiongozi wa kuhangaika hadi na watendaji wa vitongoji na vijiji. Ndiyo maana tunaona mabango yenye malalamiko ya wananchi mengi kila anapozuru eneo fulani. Mfumo huu ndio unaomfanya rais aonekane ndiye kiongozi anayeweza kutatua kero zote.

Ndiyo, RC ana mamlaka yake, lakini ki-ukweli hawa mara nyingi ni ceremonial tu kwa sababu hawana nguvu za kuwawajibisha baadhi ya watumishi au wateule. RC anachofanya ni ‘kukemea’ na ‘kutisha’. Ma-RC au ma-DC wachache wanaoonekana wachapakazi, wako hivyo kwa sababu tu ya jeuri na kiu ya utumishi wao kwa umma, lakini katika uhalisia hawana meno.

Kama nilivyosema hapo awali, Rais Magufuli kwa kazi nzuri anazolifanyia taifa hili lililokuwa limedharauliwa kimaendeleo, aangalie zawadi nyingine ya kuwapa Watanzania. Afumue mfumo wa uongozi uliopo sasa kwa sababu unachelewesha maendeleo. Pengine wananchi watakapomwidhinishia miaka mingine mitano hapo mwakani, atazame namna ya kukamilisha Katiba ili yote haya na mengine yenye tija kwa taifa letu yalindwe kikatiba baada ya kupata ridhaa ya Watanzania wengi.