Edgar Aggaba, mwanasheria wa Emmanuel Okwi, nyota wa soka wa kimataifa kutoka Uganda, hakufika Dar es Salaam kusimamia kesi ya mchezaji huyo wakati Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ilipojadili mkataba na usajili wake katika klabu ya Yanga.

Akiwa Uganda, Aggaba amesema kwamba hadhani kwamba ilikuwa muhimu kwake kuja Dar es Salaam, Tanzania, baada ya kuipima kesi hiyo na kuona kuwa ni rahisi na kwamba Okwi mwenyewe angeweza kujitetea kuondoka Yanga kabla ya kusajiliwa Simba.

Amesema Yanga imechemsha kwa kukiuka mkabata wake na katika hilo, anasisitiza; “Yanga haina wa kumlaumu zaidi ya uongozi wao kukosa umakini na kuwa na jeuri.”

Wakati Yanga ilijipanga kwenda kwenye rufaa hiyo ikiwa na mwanasheria wake, Sam Mapande, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati Ndogo za Klabu hiyo, Simba iliyomsajili Okwi kwa mara ya pili ikampa mchezaji mwanasheria maarufu Dk. Damas Daniel Ndumbaro.

Hoja za Mapande kukata rufaa ya kutomwachia Okwi ni kupata haki yao ambayo wameshindwa kuipata katika TFF kwa kuwa maadili yaliyotolewa na FIFA yamekiukwa.

Yanga ilimdai Okwi kiasi cha dola 500,000 za Marekani (sawa na Sh. 900 milioni) baada ya mchezaji huyo kuvunja mkataba huo na klabu hiyo. Gharama hizo zilipanda kufuatia mchezaji huyo kuamua kujiunga na Wekundu wa Msimbazi Simba Sports Club, lakini awali Yanga walikuwa wanamdai mchezji huyo dola 200,000 za Marekani (sawa na Sh. 340 milioni).

Ni hivi; Dar es Salaam Young Africans (Yanga), yenye makao yake makuu katika mitaa ya Jangwani na Twiga jijini Dar es Salaam, ilimsajili Okwi katika sakata lake la kisheria na timu ya Etoile du Sahel ya Tunisia Desemba 2013 na kucheza mechi 11 tu za Ligi Kuu Bara. Lakini kuelekea mwishoni mwa ligi kwa mara nyingine Okwi aliingia katika mgogoro na klabu ya Yanga kwa kushinikiza amaliziwe pesa zake zote za usajili.

Lakini uongozi wa klabu hiyo umefunga safari ya kwenda Geneva, Uswisi kwenye Mahakama ya Soka (CAS) iliyo chini ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA). Hata hivyo, Yanga ina haki kufanya hivyo.

Inachokifanya Yanga kwa sasa ni kujaribu kuwatuliza mashabiki wake. Inafanya kazi ya kutuliza hasira za wanachama wake wanaoelezwa kuwa ni wengi ikilinganishwa na timu nyingine Tanzania hususani Simba – mtani wake wa jadi. Yote hayo ni kutafuta amani klabuni.

Imekwenda huko kudai haki ya kummliki au kumdai mamilioni mwanasoka Emmanuel Okwi, raia wa Uganda, baada ya kuvunja mkataba wake na kuhamia Simba ghafla, lakini akiwa amewahi tarehe ya mwisho kabla ya kufungwa kwa dirisha kubwa la usajili, mapema mwezi huu.

Kama nilivyosema awali, Yanga ina haki, lakini kwa inachokifanya ni kujisumbua tu kwa sababu Kamati ya Rufani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) iliangalia uhalali wa mchezaji na mkataba wake Yanga, na kugundua upungufu na kumwacha nyota huyo kama mchezaji huru.

Wakati wanafikia uamuzi huo, tayari Simba ilikuwa imemsajili Okwi na ameanza kuitumikia klabu hiyo ya Msimbazi, ambayo sasa inaelezwa kuwa imekamilisha safu yake ya ushambuliaji kwa kuwa Amisi Tambwe, Kiongera wakali kama wa Manchester United ya England yenye Falcao, Van Persie na Rooney.

Dk. Ndumbaro hakuwa na kazi kubwa kupangua hoja za Yanga, kwani alianza kuwasilisha barua za mawasiliano kati ya Okwi na Yanga ambao mwisho wa siku kamati ikaona kuwa mchezaji huyo alikwisha kuondolewa Yanga. Sasa Yanga inahaha CAS kwa kitu gani?

Dk. Ndumbaro aliwamaliza zaidi Yanga katika hoja zifuatazo:-

    1. Klabu inaposhindwa kumlipa mchezaji wake mshahara kwa miezi mitatu mfululizo, ambapo Yanga imedhihirika kushindwa kufanya hivyo kwa Okwi kwa miezi mitano mfululizo.
    2. Kukosekana kwa huduma muhimu za kijamii kama (Bima, matibabu na malazi) ambapo pia Yanga imekiuka hili baada ya kushindwa kumlipia pango la nyumba mchezaji wake pamoja na kushindwa kumlipa kiasi cha dola 50,000 za Marekani (sawa na Sh. 80 milioni).
    3. Yanga iliomba kuvunjwa mkataba wa Okwi bila ya kumpatia  nakala ya barua, yeye akafanya juhudi ya kuzipata barua hizo na kukubaliana na hilo kwa barua pia, maana yake hakuwa tena na mkataba na Yanga.
    4. Msisitizo bila ya kusema kiasi gani, Okwi naye anaidai Yanga fidia ya kukiuka mkataba ambao tayari umevunjika. Dk Ndumbaro ameitaka Yanga kumlipa mteja wake jumla ya Sh. 111.8 milioni.

Vigezo vingine vinavyompa uhuru Okwi kuwa huru na kujiunga na timu yoyote ni pamoja na vifuatavyo na vinatambulika kisheria.

    1. Klabu itakapotamka kisheria kuwa imefilisika, ambapo Yanga haijatamka hilo, lakini ni kigezo kinachomruhusu mchezaji kuwa huru.
    2. Pale ambapo mchezaji anaweza kununua mkataba wake wote uliobakia na timu husika.
    3. Endapo mchezaji hatatumika kwa kiwango cha asilimia 10 katika mechi za michuano ya kishindani ndani ya msimu mzima. Hili lina utata kwani Yanga waliweza kumtumia kwa mechi 11 tu za msimu uliopita na ndipo misukosuko ya madai ya mshambuliaji huyo yalipoanza.

Kufuatia na vigezo vya FIFA na vipengele vya taratibu hizo alizozitumia Dk. Ndumbaro, ni dhahiri kuwa Yanga inajaribu kuwapoza tu mashabiki wake.