Mikataba yote ya kimataifa huongozwa na wajibu wa aina mbili. Wajibu ulioandikwa (express obligation) na wajibu ambao haukuandikwa (implied obligation).
Wajibu ulioandikwa ni masharti yote ya mkataba yaliyo katika maandishi ambayo wahusika husoma na kuridhia, wakati wajibu usioandikwa ni masharti ya mkataba ambayo hayakuandikwa katika mkataba lakini yapo kwa asili au yapo kwa kuwa tayari yalishasemwa na sheria na hivyo si lazima kuyaandika katika mkataba.
Mathalani, mfanyakazi wako wa duka hawezi kukuibia halafu akasema kwenye mkataba wangu wa ajira hakuna sharti la uaminifu. La hasha, uaminifu ni sharti la asili ‘implied obligation’ kwa hiyo liandikwe au lisiandikwe bado lipo tu.
Kwenye mikataba ya kimataifa kama ile ya kwetu na kampuni za madini, masharti yafuatayo ni ya asili na hayahitaji kuwa yameandikwa ili kuyatekeleza;
Wajibu wa kuandika taarifa zote muhimu kuhusu shughuli inayotekelezwa katika mkataba (Implied covenant to disclose all necessary information over the subject matter).
Wajibu wa kutekeleza na kutenda kwa nia njema (Implied covenant to act in good faith and fair dealing).
Wajibu wa kila mhusika katika mkataba kuwa mkweli. Hili huwa ni katazo la udanganyifu (Fraud).
Haya yawe yameandikwa kwenye mkataba au hayakuandikwa, yakikiukwa tafsiri yake ni kukiuka masharti ya mkataba.
Matendo kama kulaghai kuhusu uzito wa madini yanayochukuliwa, kulaghai kuwa unachukua dhahabu huku ukijua unachukua zaidi ya dhahabu, kulaghai kuhusu bei, kutotoa taarifa sahihi za kipi unapata na kipi hupati, nk ni kukiuka wajibu na masharti ya mkataba, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Na ikiwa wamekiuka mkataba kwa misingi hiyo, basi Tanzania inaweza kufanya yafuatayo;
Kuendelea na mkataba lakini kwa sharti la kurudisha kile chote kilichopotea kwa muda wote (specific performance).
Kutoendelea na mkataba na kudai fidia, hasara tuliyopata, pamoja na riba zake kwa kipindi chote (breach of contract).
Ndugu zangu, wajibu wa kutekeleza na kutenda kwa nia njema (implied covenant to act in good faith and fair dealing), kuwa mwaminifu na kutoa taarifa sahihi katika utekelezaji mikataba ni matakwa ya lazima duniani kote.
Sheria ya biashara ya Amerika Uniform Commercial Code vifungu vya 1-12 habari hii imeelezwa kwa upana.
Sheria ya biashara ya Ufaransa na Ujerumani The German Civil Code (BGB) na Civil Code of France zimeeleza vitu hivi.
Pia Mahakama Kuu ya Uingereza katika kesi ya Yam Seng PTE vs International Trade Co. Ltd (2013) EWHC 111 (QB), iliamua kuwa masuala ya uaminifu na kutoa taarifa sahihi katika kutekeleza mikataba ni wajibu ambao upo hata kama haukuandikwa kwenye mkataba.
Hali kadhalika, Sheria yetu ya Mikataba, Sura ya 345 vifungu vya 18 na 13 vimeyafanya masuala ya udanganyifu na kutoa taarifa zisizo sahihi kama mambo ambayo ni makosa na yanayobatilisha mkataba.
Kamati ya Profesa Mruma imebaini upotevu wa bilioni 829.4 x Miezi 12 kwa miaka 18= Trilioni 829.4. Hizi ni pesa nyingi mno. Tunayo kesi nzuri ya madai na uhakika wa kurejesha fedha tulizopoteza. Ni vema muda huu pamoja na mambo mengine, nguvu nyingi ikatumika kuona ni namna gani tunapata hii fedha. Makosa yapo na yametendwa na hilo halina shaka. Iko wapi haja kuhofu, hakika haipo.
Yumkini haitakuwa rahisi kutokana na aina ya mabepari ambao tunashughulika nao. Ni mabepari hatari wenye mtandao mkubwa wa kisiasa na nchi wafadhili pamoja na taasisi kubwa kama IMF, WB, UN nk.
Hata hivyo, tumeshasema hii ni vita na vita sharti ipiganwe ili waliosiginwa wawe huru. Tunaweza kuumia kwa muda ila mwisho wa maumivu hayo itakuwa ni neema kubwa na ya milele.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu mbariki Rais kwa pamoja tushinde vita hii.
Kuhusu sheria za ardhi, mirathi, kampuni, ndoa n.k, tembelea SHERIA YAKUB BLOG.