Mojawapo ya habari zilizobeba uzito katika gazeti hili ni ile inayohusu uchakachuaji wa mbolea, ambao umekuwa ukichangia kudhoofisha juhudi za wakulima katika kujiondolea umaskini.

Tayari Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika imefanya ukaguzi maalumu na kubaini kampuni za udhibiti, uuzaji na usambazaji wa mbolea zinazofanya madudu hayo.

 

Kampuni hizo zimetajwa kuwa ni ile ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (FST) pamoja na Staco, Apex na Yara zinazouza na kusambaza mbolea kwa wakulima nchini.

Ripoti maalumu iliyowasilishwa na Dk. Susan Ikera kwa Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima, imeambatanisha vielelezo vya mbolea feki zilizokutwa kwenye maghala ya kampuni hizo.

 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, baadhi ya mbolea zimegundulika kuwa chini ya kiwango kutokana na kuchakachuliwa kwa kuchanganywa na saruji, nyingine zimechanganywa na chumvi.

 

Hali hiyo imesababisha wakulima wengi wa mazao mbalimbali yakiwamo ya tumbaku, pamba na mahindi katika maeneo mengi nchini kupata hasara ya mavuno duni kutokana na matumizi ya mbolea hizo.

 

Baada ya kupata ripoti hiyo na maelezo ya nyongeza, Naibu Waziri Malima ameapa kuchukua hatua za kuhakikisha kampuni husika zinafutiwa leseni za kufanya biashara ya udhibiti, uuzaji na usambazaji wa mbolea nchini.

 

Kimsingi hatua ambazo Naibu Waziri huyo ameahidi kuchukua dhidi ya kampuni hizo zinatia matumaini kwani zinaonesha jinsi asivyopenda kuona na kusikia watu wachache wanakuwa bilionea kwa kuwafanya wakulima maskini kuwa maskini wa kutupwa.

 

Lakini sisi JAMHURI tunakwenda mbali zaidi ya hapo. Tunaona kuna haja ya wamiliki na viongozi wa kampuni hizo kuchukuliwa hatua za kufikishwa mahakamani kujibu mashitaka ya kukiuka masharti ya leseni zao na kuhujumu wakulima ambao ndiyo tegemeo kubwa la ukuaji wa uchumi wa Taifa letu.

 

Hatua ya kuzifutia kampuni hizo leseni pekee haitoshi kwa kuwa tayari zimeshawaliza wakulima kwa takriban miaka 20 sasa, na hata Serikali yenyewe imeshalizwa kwa kuuziwa mbolea feki (bila kujua) kama sehemu ya ruzuku ya pembejeo kwa wakulima.

 

Kwa mantiki hiyo, pamoja na hatua ya kuzipiga kampuni hizo marufuku ya kufanya biashara hizo nchini, Serikali ihakikishe inazifungulia mashitaka mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.

 

Pamoja na hatua hizo, JAMHURI itafurahi kuona na kusikia kampuni zilizobainika kuchakachua mbolea pia zinawajibika kwa kuwalipa wakulima fidia ya hasara waliyoipata kwa kipindi walichotumia mbolea hizo feki.