Ualimu ni kada muhimu kweli kweli kwa maendeleo ya jamii yoyote. Taifa linaloipuuza kada hii halina mwisho mwema.

Matokeo ya kidato cha nne nchini yaliyotolewa wiki iliyopita, yamepokewa kwa mitazamo tofauti.

Shule binafsi zimeendelea kung’ara dhidi ya shule za umma. Hili ni tatizo. Duniani kote, taasisi za umma – shule, vyuo, hospitali – ndizo zinazong’ara kwenye matokeo mazuri. Zama zetu kusoma shule za Serikali ilikuwa sifa kubwa kwa mwanafunzi, mzazi au mlezi. Kusoma shule binafsi ilionekana mwanafunzi si ‘kipanga’. Leo kusoma shule ya umma inachukuliwa kuwa ni aibu! Hali hii sharti tuibadili.

Baada ya matokeo hayo, kama ilivyotarajiwa, kumekuwapo ‘hasira’ nyingi za kuhoji. Hitimisho la watawala limekuwa ‘walimu wakuu washushwe vyeo’ au ikiwezekana wafukuzwe!

Tumesikia matamko ya ‘wakubwa’ wenye msimamo huo, hasa wale ambao shule zao zimekuwa na matokeo mabaya. Haya tunayoyasikia kwenye matokeo ya shule za sekondari, ndiyo hayo hayo yanayotokea kwa matokeo ya darasa la saba.

Inawezekana wakawapo walimu wakuu walioshindwa kutekeleza wajibu wao, na hivyo kusababisha matokeo mabaya kwa wanafunzi. Hii ni sababu ndogo tu kati ya sababu nyingi kubwa na za kweli zaidi. Mwalimu Mkuu au Mkuu wa Shule mwenyewe anaweza kufanya nini kuboresha matokeo ya wanafunzi?

Juzi, nilizungumza na mwalimu mkuu wa moja ya shule ya msingi wilayani Butiama. Shule yake ina wanafunzi 1,300 lakini ina vyumba vinane tu vya madarasa!

Ukosefu wa vyumba umesababisha kuwapo kwa ‘session’ mbili. Kuna wanafunzi wanaosoma kuanzia saa 1:30 asubuhi hadi saa 6:20 mchana. Wengine wanaanza saa 6:30 hadi saa 11:30 jioni. Hawa wanaoingia mchana, wanachofanya ni kwamba asubuhi wanapelekwa wakalime mashambani ili mchana waingie madarasani. Kwa hiyo, wanapoingia mchana wanakuwa hoi bin taaban kwa uchovu na njaa!

Pili, wanafunzi hao 1,300 na walimu wao hawana vyoo vya kuwatosheleza. Kilichopo kina matundu manne yanayotumiwa na wanafunzi na walimu wao! Hii ni shule ya msingi. Bila shaka hali ni kama hii, au mbaya kuliko hii kwa shule nyingi za msingi na sekondari nchini.

Mwalimu mkuu au mkuu wa shule – wa shule ya aina hii – anapofukuzwa au kushushwa cheo kwa sababu ya kufeli kwa wanafunzi wake, anakuwa ameonewa.

Tukubali kuwa shule zetu zinakabiliwa na matatizo mengi na makubwa. Matatizo haya ni matokeo ya kile kilichoamuriwa kiwe hivyo na jamii nzima ya Watanzania – kuanzia kwa wazazi na walezi hadi kwa viongozi wa nchi.

Kama Taifa, yapo mambo ya maana tuliyoamua kuyapuuza na sasa tunafaidi matunda ya uamuzi huo. Mojawapo ya mambo hayo ni suala la uzazi wa mpango. Kuna watu wanaohoji mbona uchumi wa nchi unakua, lakini hali ya maisha ya wananchi inazidi kuwa mbaya? Mimi si mchumi, lakini akili ya kawaida inanifanya niamini kuwa kasi ya ongezeko la watu tuliyonayo haiendani na kasi ya ukuaji uchumi. 

Wananchi wanapoachwa wazae kadri wanavyojisikia, matokeo yake ndiyo haya ya kushindwa kuhimili mahitaji muhimu! Miaka ya 1970 ingawa nchi yetu ilikuwa na idadi ndogo ya watu, bado Serikali ilikuwa na wajibu wa kuhamasisha uzazi wa mpango. Vipindi vya redio, maigizo, mabango na vipeperushi vya kila aina vilisambazwa kuhamasisha aina hiyo ya uzazi. Tulifanikiwa. Leo hayo mambo hayapo. Tumeyapuuza.

Serikali kwa wakati huo yawezekana ilisisitiza uzazi wa mpango kwa sababu ilikuwa na mzigo wa kusomesha na kutoa huduma nyingine kwa wananchi bure na kwa maana hiyo iliujua uzito wa mzigo.

Leo, Serikali imerejea mpango wa utoaji elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne. Kinadharia, mpango huu ni mzuri kwa sababu hata watoto wa maskini sasa wana fursa ya kupata elimu hiyo. Swali la kujiuliza; je, Serikali ina ubavu wa kutoa elimu bure yenye kiwango kinachotakiwa? Jibu ni hapana. Kwanini haiwezekani? Haiwezekani kwa sababu nchi ina mambo mengi ya kufanya. Haishughulikii elimu pekee. 

Bado naona wazazi na walezi wana wajibu wa kushiriki kusaidia kuboresha hali ya elimu. Kushiriki huko si lazima kuwe kwa fedha taslimu. Wazazi wanaweza kushiriki kwa kujenga vyumba vya madarasa, nyumba za walimu na hata vyoo. Ni mambo ya aibu kwa nchi huru kuona shule yenye watoto 1,300 ikiwa na matundu manne ya vyoo ilhali wazazi, walezi na wadau wengine wakiwa wamekunja mikono kana kwamba tatizo hili haliwahusu. Kujengewa choo kwa “Hisani ya Watu wa Marekani” ni fedheha! Sehemu kama Geita ambayo dhahabu iko kila mahali kuomba msaada wa kujengewa choo ni kashfa na aibu kwetu Watanzania.

Tumeanzisha shule za kata nchi nzima. Ni uamuzi mzuri kabisa. Je, tumetafakari na kubaini umbali ambao wanafunzi wanalazimika kusafiri kwenda na kutoka shuleni? Je, tumeweza kujua wanafunzi wanaamka saa ngapi tayari kwa safari ya kwenda shuleni? Kisayansi, mlo una nafasi kubwa katika ufaulu wa mwanafunzi.

Hapa naomba nitoe mfano. Nyumbani kwangu napata shida kweli kweli kutoka kwa wanafunzi. Mimi ni mwana mazingira. Nina miembe na michungwa kwa wingi. Kipindi hiki ni msimu wa maembe. Yamezaa kweli kweli. Wanafunzi wa Kwembe na Luguruni wanachofanya ni kujihimu mapema wakiwa na mifuko kuokota maembe. Hiyo ndiyo chai yao. Wakitoka shule jioni, wengi wanakimbilia kwenye miembe kuokota na kuangua. Wanatumia mawe kupopoa. Wamevunja kioo cha ki-escudo changu ninachokiegesha chini ya mwembe. Awali, nilikasirika. Nikawa nimeazimia niwashitaki shuleni. Baadaye nikajiona nafanya jambo la kijinga. Nikaamua nikae upande wao. Nikawa mimi ndiye ninayeamka saa 10 alfajiri kupambana na makondakta wa daladala. Nikawa mimi ndiye niliyeamka bila kupewa senti ya kununulia chai. Nikawa mimi ndiye niliyeshinda darasani, na sasa natakiwa nirejee nyumbani-kutwa nzima tumbo likiwa tupu! Nikawa mimi ndiye ninayezuiwa na huyu baba kuangua au basi kuokota maembe yaliyodondoka. 

Baada ya kukaa upande wa wanafunzi, nikalazimika kuwa mpole. Nilichowaomba ni kuhakikisha hawavunji matawi ya miembe na michungwa ili kuipa fursa ya kuzaa msimu ujao waendelee kuikabili njaa! Hii ndiyo hali halisi ya watoto wetu wengi nchini.

Mtoto anayesoma katika mazingira ya aina hiyo huwezi kumlinganisha na yule anayesoma akiwa anaishi bweni shuleni au yule ambaye alfajiri anaamshwa ili akapande gari tayari kwenda shule. Mtoto wa aina hiyo ni tofauti na yule ambaye akifika shule anakuta chai nzito na mikate iliyopakwa siagi kabla ya kupata mlo wa mchana wenye sifa zote za kuitwa ‘mlo kamili’.

Mwalimu anayefundisha shule ya kata (shule ya umma), mazingira yake yanashabihiana kwa kila hali na mazingira ya wanafunzi wake na pia shule alipo. Mwalimu anayefundisha shule aina ya Feza, mwonekano wake ni wa ki-Feza! Huwezi kumlinganisha na mwalimu aliyeko Manyovu, Tandahimba, Kasesya au Mwanza-Buriga!

Shule hizi mbili zinatofautiana hata kwenye vitabu vya ziada na kiada-pamoja na vifaa vya kufundishia. Kuna maelfu kwa maelfu ya watoto wa shule za kata wanaosoma masomo ya sayansi, lakini hawajawahi kuiona wala kuitumia ‘bunsen burner’. Lakini kwa maajabu ya Mungu, wapo wanaoshinda kwa daraja la kwanza! Wakati wao wakiwa hata hawana hicho kifaa, kuna shule ambazo wanafunzi wana haki ya kukataa kutumia ‘bunsen burner’ iliyotengenezwa India! Wanataka iliyotoka England au Japan! 

Wakati kuna shule ambazo walimu wake wanaoneshana umahiri kwa kubadili magari, huko vijijini na pengine mijini kuna walimu ambao hata hiyo pikipiki ni kitu cha anasa kabisa kwao! Wakati walimu wengine wakiishi kwenye nyumba zenye kila kitu, wapo walimu wetu ambao nyumba zao zimeezekwa kwa makuti. Wananyeshewa. Wanashirikiana na mifugo kwenye maji.

Katika mazingira ya aina hiyo, ambayo pengine wanafunzi wa madarasa mawili (mfano la tano na la sita) husomea kwenye chumba kimoja kwa wakati mmoja wakiwa wamepeana migongo, ni dhambi kumwajibisha mwalimu mkuu au mkuu wa shule kwa matokeo mabaya.

Hapa tunapaswa kuangalia mazingira ya walimu, wanafunzi na vitendea kazi katika shule husika.

Lakini zipo shule ambazo licha ya kuwa na walimu wa kutosha, vifaa na mazingira mazuri; bado matokeo katika shule zao ni mabaya. Hapo tunapaswa kwenda mbali kubaini chanzo cha tatizo.

Sidhani kuna shule inaweza kufanikiwa kuwa na wanafunzi weledi bila kuwapo msaada wa  wazazi na walezi. Zamani zile, mtoto alikuwa ni zao la umma. Kila mzazi au mlezi alikuwa na wajibu wa kuhakikisha yeyote anayeitwa mtoto au mwanafunzi anaenenda katika misingi inayotakiwa kijamii.

Kwa mfano, mzazi alipopita mtaani akawakuta wanafunzi wametega kwenda shule, mzazi huyo aliwajibika kuwahoji na ikiwezekana kuwakamata watoto hao na kuwashitaki shuleni au katika mamlaka nyingine. Mzazi alipokuta genge la watoto wakishiriki vitendo visivyokuwa vya kimaadili, alihakikisha anapambana na hali hiyo akilenga kujenga ustawi wa mtoto, jamii na Taifa kwa jumla. Mtoto alichukuliwa kuwa ni rasilimali ya Taifa kwa hiyo kufaulu au kufeli kwake kungekuwa ni kufaulu au kufeli kwa Taifa!

Leo wazazi hawana muda na watoto. Kila mzazi kawa mkali mithili ya pilipili. Hakuna mtu mzima anayemrudi mwanafunzi. Walimu wanaogopa kuwaadhibu wanafunzi kwa sababu kufanya hivyo maana yake ni kumwambia mwalimu awe tayari kupigwa, tena mbele ya hadhara.

Wapo wazazi na walezi walioondoka na kwenda shuleni, ama kuwatukana au kuwapiga walimu waliowaadhibu au kuwasema ‘vibaya’ watoto wao. Hapa naomba Mahakama inisamehe – kuna mzazi mkoani Tanga amefikishwa mahakamani akituhumiwa kumuua kondakta aliyedai nauli. Mwanafunzi alikaidi (inavyodaiwa) kulipa nauli, kondakta akapambana naye, mwanafunzi akaenda kushitaki kwa baba, kilichofuata ni mauti kwa kondakta!

Katika mazingira ya aina hiyo – ya walimu kutukanwa na kupigwa – ni mwalimu yupi atakayekuwa tayari kuhangaika na mwanafunzi? Je, si kweli kuwa walimu wengi sasa wameamua kurejesha mikono nyuma na kuwaacha wanafunzi wafanye wanavyotaka? Je, si kweli kuwa kwenye hizo shule zenye matokeo mabaya kuna wanafunzi wanaofauli kwa daraja la kwanza, la pili au la tatu? Wao wanafanya miujiza gani hadi wafaulu? Kwa hao, ukichunguza utabaini kuwa wazazi au walezi wanawapa ushirikiano wa kutosha walimu.

Ufaulu wa wanafunzi haupo darasani au shuleni pekee. Mitaani na nyumbani ni sehemu zinazoweza kusaidia sana au kuwaangusha kabisa wanafunzi. Je, wazazi tunajua watoto wetu wanafanya nini wawapo nyumbani? Wanajisomea au wanashinda kwenye ‘vibanda umiza’ kuangalia sinema? Je, tunajua fedha tunazowapa zinaishia kwenye ‘kubeti?’Je, wanapotazama TV nyumbani, wanatazama na kusikiliza taarifa za habari au wanashindia na kukesha kwenye stesheni za bongo fleva na sinema za Nigeria?

Yapo mengi ya kuyasema hapa. Itoshe tu kusema kuwaadhibu walimu kwa matokeo mabaya ya wanafunzi, ni kuwaonea. Tatizo la ufaulu ni tatizo la jamii nzima – kuanzia kwa wanafunzi wenyewe-wazazi/walezi-walimu hadi watunga na wasimamia sera. Tujisahihishe.