Awali ya yote, nianze mada hii kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai aliotujaalia, mimi na wewe, kuweza kuwa hai hadi sasa.
Naamini uhai tulio nao ni kwa neema ya Mungu maana wengi walitamani tuwe nao lakini haikuwezekana. Hivyo ni vema tena ni haki tukamshukuru Mwenyezi Mungu.
Nchi yetu imebahatika kuwa na rasilimali nyingi za maliasili – ardhi na udongo wenye rutuba, maji, misitu, wanyamapori, samaki, madini na rasilimali watu.
Tanzania Bara inalo eneo la hekta milioni 89. Taifa kuweza kuwa na eneo kama hilo ni bahati ya aina yake. Isitoshe, Tanzania imejaaliwa kuwa na ukanda wa bahari wenye urefu wa takribani kilometa 800 – kuanzia kusini mpakani na Msumbiji hadi kaskazini mpakani na Kenya.
Rasilimali zote hizo na nyingine ambazo sikuzitaja zinatujengea fursa nyingi kuweza kujiletea maendeleo. Kwa upande mwingine tujiulize tunaposema maendeleo kwa Tanzania na watu wake tunamaanisha nini? Je, ni kweli tukae tukisubiri nchi zilizoendelea zije kutuletea maendeleo tunayoyataka? Je, dhamira ya “Uhuru na Kujitegemea” maana yake nini?
Kwa bahati mbaya wapo baadhi yetu wanaosema “bila misaada kutoka nje hatuwezi kuendelea”. Kama hivyo ndivyo, najiuliza hao wanaotakiwa kuja kutusaidia na ambao wameendelea je, nani aliwasaidia wakafikia hapo walipo? Kama hakuna aliyewasaidia walifanyanje wakajipatia maendeleo waliyoyafikia?
Vilevile, kama sisi ni binadamu kama wao na tumekuja duniani kwa njia ile ile ya kuzaliwa na mwanamke, tukanyonya matiti hadi tukakua na hatimaye kuweza kufanya kazi za kujiletea maendeleo; iweje wao waendelee na sisi tuzidi kujiona wanyonge kila kukicha? Ni kweli kazi ya kujiletea maendeleo si lelemama. Inahitaji kufikiri, kuwapo hekima/busara na kufanya kazi kwa bidii.
Nchi zilizoendelea zimeyaweza hayo; kwanza kwa kuhakikisha watu wake wanapewa elimu katika nyanja zote za maisha. Pili, wakafikiri ipasavyo, wakakuza vipaji vyao na hatimaye wakaanzisha viwanda badala ya kutegemea rasilimali ardhi kama njia pekee ya kumudu maisha. Hivyo, elimu, viwanda na usimamizi thabiti vikawa kichocheo cha maendeleo waliyonayo.
Vilevile, nchi zilizoendelea watu wake walihangaika sana, wakafanya kazi kwa bidii na wengine katika kuhangaika kwao ili wawe na maisha bora zaidi iliwalazimu kuja hadi Bara la Afrika wakachukua nguvukazi. Kutoka Afrika walichukuliwa watumwa kwenda kufanya kazi katika mashamba na viwanda. Hawakupelekwa huko kwa minajili ya kustarehe, bali kama nguvukazi. Wakachukua rasilimali nyingine kama mazao ya misitu, kilimo na madini.
Kusema kweli, maendeleo yataletwa na mtu au jamii yenyewe na kama ni kusaidiwa hilo liwe moja ya matokeo ya juhudi zake katika harakati za kujiletea maendeleo. Haiingii akilini kwamba tukae tubweteke tukisubiri misaada. Itakuwa ni ajabu tukifanya hivyo na jamii duniani haitatuelewa. Badala ya kutegemea misaada ya nje tunatakiwa tukazane, tujizatiti kweli kweli na tufanye kazi kwa bidii na nguvu zote. Tukifanya hivyo Mwenyezi Mungu ataziona juhudi zetu na atatusaidia tusonge mbele.
Kama kuna rafiki yetu atakayeziona juhudi zetu na anayo nia ya kweli kutusaidia, basi milango iwe wazi na awe huru kutusaidia. Haifai kuwa ombaomba wakati uwezo wa kujiletea maendeleo tunao. Kama ni teknolojia zinafahamika, kama ni ardhi tunayo, rasilimali watu ipo tena ni nguvukazi ya kutosha, baadhi ya Watanzania ni wataalamu wenye uzoefu – sasa ni kuchapa kazi kwa kuutumia ujuzi wetu katika fani mbalimbali kwa faida ya wote.
Ndiyo maana tunasema elimu ipewe mkazo, afya zetu ziimarike na miundombinu iwe imara na mengineyo ikiwamo amani, upendo na kuthaminiana kama Watanzania wenye nia moja ya kufanya kazi kwa nguvu na kujiletea maendeleo. Kwa kufanya hivyo, tutasonga mbele. Hata Serikali ya Awamu ya Tano inataka kuinua maisha ya Watanzania kwa kufanya kazi kwa bidii, kubana matumizi na kuona Tanzania inaingia kwenye uchumi wa viwanda.
Hakuna siri, Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli imeingia madarakani katika hali isiyowaridhisha Watanzania. Kumekuwapo malalamiko mengi kwamba nchi inatafunwa, mafisadi kibao, ujangili, dawa za kulevya, rushwa kila mahali na viongozi kutowajibika. Pamoja na CCM kurejea madarani, tunamshukuru Mwenyezi Mungu ametuinulia Rais ambaye anafanya kazi na kupambana na maovu; na anataka Taifa lirejee kwenye msingi wa awali wa kuwatumikia Watanzania kwa uadilifu na weledi.
Anataka rasilimali za Taifa ziwanufaishe wengi kuliko kuporwa na kunufaisha wachache. Sheria zifanye kazi na kila kiongozi katika nafasi yake awajibike. Je, kwa kufanya hivyo anakosea nini? Vilevile, hakuna mahali amesema hatutaki misaada, bali anasisitiza kuwa kama ni misaada yenye masharti yasiyoendana na utu wetu; mfano kututaka tuingize masuala ya ushoga katika sera na sheria zetu, bora misaada ya aina hiyo wakakaa nayo. Lakini kama ni rafiki wa kweli na ameona juhudi zetu na yuko tayari kutuunga mkono, basi afanye hivyo nasi tutamshukuru kwa kutujali.
Baadhi wanasema kuwa Rais amekuwa dikteta – sielewi kivipi. Kama tunasema kuna hali kama hiyo sawa, hata hivyo ukiwapo udikteta kidogo kwenye familia fulani, lakini wanafamilia wakapata riziki na wakaishi maisha mazuri ni bora ikawa hivyo kuliko kuwa na familia ambayo kila mtu anafanya anavyotaka, lakini mwisho wa yote maisha yao yakawa ya hovyo. Natambua kuwa binadamu hatutaki kubanwa. Tunataka kufanya tupendavyo, lakini kwa hali Taifa letu tulipokuwa tumefika mtakubaliana nami kwamba tulihitaji kiongozi wa juu wa kutusaidia turudi kwenye mbio sahihi za kuliletea maendeleo Taifa letu na watu wake.
Tunahitaji Taifa lenye maadali mema na matumizi sahihi ya rasilimali. Watanzania wanataka kuona huduma za kijamii zinakuwa bora – elimu bora na si bora elimu; huduma za afya zikiimarika; tunapata maji ya kutosheleza mahitaji; miundombinu; kilimo kinakuwa chenye tija; na mazingira yanahifadhiwa kwa faida yetu na vizazi vijavyo.
Baadhi ya Wanzania wanasema demokrasia inadhoofishwa, sawa! Lakini dhana ya kuwapo demokrasia bila ya kuwapo dhamira ya kweli ya kuwaletea maendeleo endelevu Watanzania ni sawa na kutokuwapo demokrasia. Wengine wanasema ni vigumu kwa malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano kutimia maana imezungukwa na kikundi cha watu wachache (elite group), lakini chenye nguvu kisiasa, kiuchumi na hata kisheria.
Ninapopata fursa ya kutembea mitaani nasikia baadhi ya wadau wa siasa wakisema; ukitazama kusini utakutana na ufisadi; ugeukie kaskazini unakumbana na ujangili; ukigeukia mashariki huko usiseme rushwa imejaa; uende magharibi unabambwa na biashara kubwa za hao watunga sera na wafanya uamuzi na mwisho ukikimbilia katikati unajikuta umezungukwa na ubinafsi na kutokuwajibika. Wana wasi wasi kwamba jitihada anazozifanya Rais wetu zitagonga mwamba. Kuna mawazo kuwa ni sawa na mbio za sakafuni ambazo mwisho wake ni ukingoni.
Kuna wengine tunasema kazi anayofanya Rais ni ngumu, lakini anafanya hayo yote akitutakia maisha bora hivyo tumwombee asitetereke katika kuyatimiza malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano. Akaze buti, asonge mbele kama ni kupasua majipu, basi afanye hivyo kwa busara na hekima bila ya kumwonea yeyote na asihofu wala kumwogopa binadamu bali amhofu na kumwogopa Mungu aliye asili ya uhai wake.
Tuzidi kumwomba Mwenyezi Mungu ampatie busara na afanye kazi zake kwa hekima kubwa shetani asimshinde. Ninayoyasikia mitaani ni dalili ya baadhi wetu kukata tama, lakini tujipe moyo tumuunge mkono.
Tangu miaka ya 1970 na 1980 Tanzania imekuwa ikipata misaada, lakini hali za Watanzania wengi kiuchumi, kijamii na kimazingira ni duni. Kiwango cha umaskini ni kikubwa. Ndiyo maana tulihitaji mabadiliko ili tuweze kuanza ukurasa mpya wa kujiletea maendeleo bila kuwategemea wahisani.
Tunahitaji kufanya kazi kwa nguvu zetu zote. Tusibweteke kwamba misaada itakuja, bali tukazane kujiletea maendeleo sisi wenyewe.
Nchi zilizoendelea zilikazana na haikuwa rahisi. Wengi waliumia kwa ajili ya kupata maendeleo. Walithubutu, wakafanikiwa. Kwa nini sisi tushindwe? Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alisema ili tuendelee tunahitaji Watu, Ardhi, Siasa Safi na Uongozi Bora. Pengine inawezekana tumeyumba katika safari yetu zaidi ya miaka 50 kama Taifa huru kutokana na kulegalega katika siasa zetu na uongozi. Watu na ardhi vipo. Kinachotakiwa ni kuimarisha siasa na uongozi Bora kwa misingi ya kuwaletea mafanikio wengi ambao bado wanajiona ni maskini wakati Taifa lao limesheheni rasilimali.
Tunahitaji siasa na uongozi unaoweka maslahi ya nchi mbele. Naamini kwa msimamo wa Serikali ya Awamu ya Tano “HAPA KAZI TU” na masuala ya MAADILI na UWAJIBIKAJI yakaingizwa katika Katiba, hakuna shaka tutafanikisha azma ya kujiletea maendeleo.
Tumwombe Mwenyezi Mungu atusaidie tuweze kutimiza wajibu wetu na tufanye kazi kwa bidii na maarifa. Uamuzi utakaofanywa na viongozi wetu uwe wenye busara na hekima kwa faida ya Watanzania wote.