Wiki iliyopita, mchambuzi na mwandishi wa masuala ya uhusiano wa kimataifa na kikanda anazungumzia Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC), akisema Umoja huu wa sasa ni ulaghai mtupu. Alichambua akisema kama baada ya miaka 50 ya Uhuru, Wakenya siyo wamoja; Wauganda siyo wamoja na Wanyarwanda wa Burundi na Rwanda si wamoja watawezaje kuwa wamoja na Watanzania? Huu ni uongo ambao unatakiwa uzikwe wakati mwasisi wa mradi huu, Alhaj Ali Hassan Mwinyi bado yu hai. Tuendeleze ushirikiano wa kibiashara lakini kusema hilo haliwezekani bila shirikisho ni utapeli. Kama nchi za Afrika zinafanya biashara na nchi za Ulaya na Marekani bila ya shirikisho sioni kwa nini ishindikane Tanzania, Uganda, Kenya, Rwanda na Burudni kufanya biashara kati yao bila ya shirikisho. Fauka ya hilo hivyo ndiyo ilivyokuwa tangu 1884 (tangu ukoloni hadi leo) huu ulazima wa shirikisho unatoka wapi? Sasa endelea…
Pili, ubinafsishaji wa mashirika ya umma pamoja na mikataba yote iliyosimamiwa na Mheshimiwa Benjamin William Mkapa chini ya mwavuli wa utandawazi ipitiwe upya wakati yeye aliyeasisi yupo hai.
Tatu, Sera ya Kilimo Kwanza, kadhalika ifutwe wakati muasisi wake, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, yu hai. Serikali ya Awamu ya Tano isiruhusu nchi iingie kwenye maangamizi kwa ajili ya kuhifadhi nyuso za marais wastaafu na waasisi wa baadhi ya sera ambazo zimethibitika kuwa ni haribifu; huko hakutakuwa ni kuwaenzi viongozi hao bali ni kuwaumbua.
Kama Mwalimu Nyerere alikosolewa kwa kufutwa sera zake wakati yu hai, tena sera ambazo hazikuhatarisha uhuru wetu; itakuwa ni kosa lisilomithilika kuacha kufuta hizi sera ambao tayari zimeanza kuvuruga amani yetu na zipo mbioni kuliweka Taifa kwenye minyororo ya ukoloni mamboleo milele.
Milele kwa vipi? Kutokana na ugunduzi wa silaha ziitwazo “drones” yaani ndege za vita ambazo hazitaji marubani, basi huu mfumo (concept) wa kupigania uhuru sasa umekomeshwa; kwa sababu huweza kufanya vita za ukombozi wakati adui yako kajificha kilometa 10,000 kutoka uwanja wa vita lakini anakuporomoshea mabomu kama kawaida. Hivyo basi kwa kuwapa ardhi yetu waja kama inavyotokea sasa, tunajifunga sisi na vizazi vyetu vijavyo kwenye ukoloni ambao hatutakuwa na jinsi ya kujikomboa.
Taifa linapouza au kukodisha ardhi, basi hapo kinachouzwa au kuwekwa rehani in uhuru wa taifa hilo, kwa sababu ardhi na uhuru ni pande mbili za sarafu moja; vitu hivi viwili haviwezi kutenganishwa katika maisha ya Taifa lolote.
Waafrika wasifanye makosa ya kunukuu sera na mifumo ya umiliki ardhi wa mataifa yanayoitwa yaliyoendelea au ya viwanda kwa kuwa kwenye nchi hizo ardhi ni uhuru, ndiyo, lakini si uhai; watu wao walio wengi hawajikimu kwa kupitia kilimo.
Kwa mfano, nchi za Umoja wa Ulaya, zinazojumuisha mataifa 28, yenye ukubwa wa eneo la mraba wa zaidi ya kilometa milioni 4 na jumla ya watu wapatao milioni 503 zina wakulima takribani 13,000,000 tu; wakati Marekani yenye watu karibu milioni 322 hivi sasa, ina wakulima 2,000,000.
Lakini kuonesha umuhimu wa kilimo katika taifa: hawa wakulima milioni 13 wa Umoja wa Ulaya, ambao wananchangia asilimia 1.6 tu kwenye pato la Umoja huo (gross domestic product- GDP) wanapewa bure (si mkopo) zaidi ya asilimia 47 ya bajeti ya Umoja huo kila mwaka.
Mwaka 2014 Marekani ilitoa kwa wakulima wake dola bilioni 149 ambayo ni sawa na dola 1,200 kwa kila kaya nchini humo. Lakini wakati huo huo hizi nchi za Ulaya, Marekani na taasisi zao kama Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Ulimwengu zinawashurutisha viongozi wa Afrika na Dunia Tatu wafute misaada yote kwa wakulima wao.
Tena pamoja na vitisho vya kusitisha mikopo kama amri yao hiyo haitazingatiwa. Jamani, iwapo kutowapatia misaada wakulima ni jambo bora kulikoni hao wenyewe hawafanyi hivyo? Huku ni kuwaona viongozi wa Afrika mazumbukuku.
Dai la kuwa nchi za Afrika zinadaiwa si hoja yenye mashiko; Marekani inaongoza ulimwengu kwa kudaiwa, hivi sasa deni lipo kwenye dola trilioni 18. Hizo nchi za Ulaya zote zina madeni mpaka kwenye kope za macho yao; mbona hiyo haiwafanyi wao waache kusaidia wakulima wao?
Watu wenye mitazamo finyu wanaweza kusema “… Oooh! na sisi Afrika tunaweza kuwafanya watu wachache wahodhi ardhi yote (kama Ulaya na Marekani) na kuwaruhusu wao walime chakula kitakachotosheleza mahitaji ya nchi nzima”. Hilo ni jepesi sana kufanyika.
Lakini swali muhimu litakuwa hili: je, wakulima hao wachache watagawa hicho chakula bure kwa wanaoporwa ardhi yao? Kwa sababu wananchi watakaonyang’anywa mwajiri wao – ambaye ni ardhi – watabaki hawana kazi wala ruzuku kutoka serikalini, hivyo hawatakuwa na kipato chochote cha kuwawezesha kununua chakula kitakacholimwa na wachache watakaokuwa sasa wameidhinishwa, kisheria, kuhatamia karibu ardhi yote nchini. Je, wenye kuporwa ardhi tunategemea waishi vipi!
Hizo nchi zilizoendelea ambazo zinaiga bila tafakari zina vyanzo vya ajira vya kutosha pamoja na kitu kinachoitwa ruzuku zinazotolewa na serikali (social security benefits), yaani fedha ambazo Serikali zinagawa bure kila mwezi, kwa wananchi wote wasiokuwa na ardhi na wasiobahatika kuajiriwa; wakati huduma hizo Afrika hazipo, sasa mfumo huu tunategemea utawezaje kufanya kazi?
Kweli nyingine ambayo pia ni muhimu sana viongozi wa Afrika kuizingatia ni kwamba tatizo linalokabili ulimwengu hivi sasa si aidha upungufu wa chakula au udhaifu wa teknologia ya kilimo, bali ugawaji mbaya wa chakula kilichopo.
Hivyo huu wendawazimu wa kilimo cha (GMO – Genetically Modified Organism) unaosambazwa Afrika kwa madai ya kuongeza mavuno ya kilimo ni mwendelezo wa kuwaona viongozi Waafrika mambumbumbu.
Hivi sasa dunia ina watu karibu bilioni 7.2 na ulimwengu una chakula cha kuweza kutosheleza kikamilifu mahitaji ya watu bilioni 11.3; lakini kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Umoja wa Mataifa (UN), watu 21,000 wanakufa kila siku kwa njaa na magonjwa yanayosabishwa na njaa; ambayo ni sawa na kifo cha mtu mmoja kila sekunde 4. Ulazima wa kuongeza uzalishaji kupitia kilimo cha GMO unatoka wapi?
Miaka ya 1960 bara la Afrika lilikuwa linazalisha mazao ya vyakula vya ziada (food surplus) kwa kiasi cha asilimia 7.5 kila mwaka; hawakutumia teknologia ya GMO!
Na tena Waafrika walikuwa kwenye kilele cha kuwapiga vita hawa wakoloni na mabeberu ambao leo tunasujudia na kuwaita waje kuleta ukame wa ardhi kama ilivyokuwa zama za kikoloni.
Vilimo vinavyonyang’anya wakulima ardhi leo vina mlengo wa kulisha matumbo ya nje ya Afrika pamoja na kujaza petroli au dizeli kwenye matangi ya magari; hivi ni vilimo vinavyolima njaa si shibe kwa bara letu. Kudai kuwa wageni wanaruhusiwa kuwekeza kwenye ardhi ili Afrika ijitosheleze katika mahitaji ya chakula ni utapeli, tena kulingana na madhara yatokanayo ni utapeli wa kihaini.
Mwaka 2009 makampuni ya Saudi Arabia yalianza kusafirisha kwao chakula ambacho makampuni hayo yanalima nchini Ethiopia wakati Waethiopia milioni tano wanategemea misaada kutoka World Food Programme; huo ndiyo ufisadi wa kisaliti.
Mwaka 1984, wakati Michael Burke wa televisheni ya BBC London aliporusha picha za Waethiopia waliokuwa wanakufa kwa njaa kwa wingi kama nzi, wiki hiyo hiyo matikiti yaliyolimwa Ethiopia yalikuwa yanauzwa kwenye soko la Covent Garden jijini London.
Mtu anaweza kusema kuwa lakini matikiti yasingeweza kuzuia watu kufa kwa njaa; hiyo itakuwa kweli, lakini huko kutakuwa kukosa kuipata mantiki yangu. Ninachokisema ni kuwa ardhi ambayo ingaliweza kutumika kulima mazao ya chakula, ilichukuliwa na kilimo cha mazao ya anasa (matikiti) kwa ajili ya kuuza nje.
Hiyo ndiyo hatari ambayo wananchi karibu wote wa Afrika wanakabiriana nayo karne hii kupitia hizi sera potofu za kuruhusu wageni “kuwekeza” kwenye ardhi; hatari ya Waafrika kwenda kulala na njaa, pengine hata kufa kwa njaa wakati ardhi na maji yao yanatumika kulima mazao ya chakula cha kulisha raia wa nje au mazao ya anasa kama maua na nishati inavyotokea Ethiopia na kwingineko.
Viongozi wanaounga mkono hizi sera duni wanaweza kujitetea kwa madai ya kuwapo kwa ardhi ya ziada ambayo haitumiki; na kuwahimiza wananchi wao wahame sehemu wanazoishi kuwapisha maharamia wanaoitwa wawekezaji kwenye ardhi.
Swali la msingi ni hili: hizo sehemu ambazo Serikali zinaamini zipo wazi na ambazo wananchi wanaweza kuhamia, kwa nini wasipewe hao “wawekezaji”, ili kuepusha zahama ya kuvuruga maisha na kutenganisha jamii kwa kuwahamisha watu ambao wametulia kwenye sehemu hizo maisha yao yote? Na sababu kuu ni moja: sehemu hizo (ambazo watu tayari wanaishi) zina rutuba ya kutosha; vyanzo vya maji vya kudumu pamoja na miundombinu; na ndiyo sababu wawekezaji wanazitaka.
Lakini, iwapo mambo haya matatu ni muhimu kwa wawekezaji, basi ni muhimu zaidi kwa wananchi wetu, yamkini ndiyo sababu walichagua kufungua maskani zao sehemu hizo. Na kwa nchi kama Tanzania, ndiyo sababu Serikali iliwaweka sehemu hizo, kwa wale waliohamishiwa wakati wa vijiji vya miaka ya 1970.
Baadhi ya watu wanaweza wakadhani kuwa nchi za Afrika nazo pia zinaweza zikajenga viwanda kama ilivyotokea kwenye hizo nchi zinazoitwa za viwanda, vitakavyoweza kuajiri wanaonyang’anywa ardhi.
Hilo linawezekana, lakini utaratibu usiokuwa wa kitapeli ni kujenga hivyo viwanda kwanza, vitakavyotoa ajira zitakazowavuta (kwa hiyari) wakulima wadogo kwenda kufanya kazi viwandani kwa sababu mapato yao yatakuwa ni mazuri zaidi kuliko kuwa wakulima wadogo wa kujitegemea.
Hivyo ndivyo viongozi wa hizo nchi zinazoitwa za viwanda au zilizoendela walivyofanya. Kujaribu kufanya kinyume chake ni ufisadi na utapeli wa kisaliti.
Harid Mkali ni mtunzi wa vitabu na mwandishi wa habari, anaishi London, Uingereza. Simu: +447979881555, barua pepe: [email protected] na tovuti: www.haridmkali.com.