Na Bashir Yakub

Wako watu bado wanalichukulia
suala la kutoa mahitaji kwa mtoto kama suala la madai ya kawaida. Wanadhani ni suala ambalo linamhusu mama mzazi na ba
basi, wao kama wao tu.
Kwa maana ni suala la kuzungumza tu na likaisha kwa maelewano yoyote yale. Kama bado una mtazamo wa aina
hii juu ya suala hili, basi unahitaji kubadilika.
Kama hautabadilika, subiri hapohapo ili sheria mpya ya mtoto ikubadilishe. Suala la mahitaji ya mtoto ni
suala ambalo lina misingi yake kisheria. Si suala ambalo umeachiwa uamue unavyotaka, kwakuwa wewe ndiye mwenye
mtoto.
Moja ya msingi wa suala hili ni kuwa hakuna kusema sina. Huwezi kutakiwa kutoa mahitaji ya mtoto ukasema sina kama si
mgonjwa asiyejiweza ama vinginevyo.
Pili, hata ukitakiwa kutoa ni wajibu kutoa kile ambacho kwa akili ya kawaida kitamwezesha mtoto kuishi kama binadamu.
Hautatoa chini ya kiwango cha ubinadamu. Ndiyo
maana nikasema suala hili siyo la kwisha kwa namna yoyote tu ambayo wewe unafikiria.
Juu ya hilo, suala la matunzo ya mtoto siyo suala la kupelekana tu ustawi wa
jamii au pengine mahakamani na kupewa amri ya kulipa tu basi. Ni kweli ustawi wa
jamii utapelekwa na mahakamani utapelekwa, ila ni kuwa haiishii tu hapo. Zipo adhabu za kisheria ambazo waweza kupata kw
kutotoa mahitaji ya mtoto.
Adhabu

Kifungu cha 51 (b) cha Sheria ya Mtoto kimetoa adhabu kwa yule anayeshindwa kutoa mahitaji kwa ajili ya mtoto kuishi na
kwa ajili ya maendeleo yake. Kifungu hiki kinatofautisha kati ya mahitaji kwa ajili ya mtoto kuishi (necessities for
survival) na mahitaji kwa ajili ya maendeleo ya mtoto (necessities for development).
Mahitaji kwa ajili ya mtoto kuishi ni kama chakula, matibabu, makazi, mavazi nk, na mahitaji kwa ajili ya
maendeleo zaidi ni elimu/shule. Ili uwe salama, yote mawili ni lazima yapatikane. Hii ni kutokana na kifungu hiki.
Aidha, kifungu kimetoa adhabu za aina tatu kwa mtu atakayeshindwa kutoa hayo mahitaji kwa mtoto.
Kwanza, ni adhabu ya faini. Kifungu hiki kinaainisha faini ya fedha taslimu isiyopungua Sh laki tano na isiyozidi Sh
milioni tano. Kwahiyo humo katikati unaweza kuambiwa kulipa Sh milioni 3,4,2, au laki 7,8,9 nk. Kumbuka hii ni faini,
si matunzo unayotakiwa kutoa. Ni penalti. Ni adhabu ya ukorofi. Kwa maana ukilipa hii bado itatolewa amri nyingine ya
kutoa mahitaji kama inavyostahili.
Pili, ni kifungo jela kisichopungua miezi sita na kisichozidi miaka mitatu. Humo katikati waweza kufungwa miezi 7,8,9,10, au
mwaka 1,2 au 3. Kumbuka kufungwa si mbadala wa kutoa mahitaji ya mtoto. Utafungwa na ukitoka huko
jukumu la kutoa mahitaji linabaki palepale.
Kifungu cha 166 cha Kanuni za Adhabu pia kimezungumzia tendo la kutotoa mahitaji ya mtoto kama kosa la jinai.
Tatu, ni adhabu ya vyote viwili, yaani kifungo pamoja na faini. Jela utakwenda na faini utatoa.
Hii nayo si mbadala wa mahitaji ya mtoto. Utatumikia adhabu zote na mahitaji ya mtoto nayo utatoa.
Kumbe si vema kulichukulia mzaha jambo hili, kwani linaweza kuathiri mustakabali wako wa maisha.

Mwisho