DAR ES SALAAM

Na Pawa Lufunga 

Aprili 13, 1922, mtoto wa kiume alizaliwa kaskazini mashariki mwa Tanzania.

Wazazi na ndugu zake hawakujua mtoto yule mdogo angekuja kuwa nani kwa taifa na duniani.

Simulizi zinasema wazazi wake wakampa jina la Kambarage, ingawa kwa asili ni jina la kike.

Baada ya elimu ya kiwango alichoweza na kufundisha shule kadhaa za sekondari ikiwamo Shule ya Mtakatifu Maria, Tabora na baadaye Shule ya Mtakatifu Francis (Pugu), Dar es Salaam akafahamika kwa jina la Mwalimu.

Alipojiunga na harakati za kisiasa, uwezo wake uliwatisha watawala wa kikoloni waliomtaka achague ama kuendelea na ualimu au siasa.

Duru za kihistoria zinadai kuwa Mwalimu Nyerere amewahi kunukuliwa akisema alikuwa Mwalimu kwa kuchagua lakini mwanasiasa kwa bahati mbaya.

Akaacha kazi ya ualimu na kuanza mapambano ya kudai Tanganyika huru, ambapo licha ya kupitia maumivu na madhila mbalimbali kama ambavyo wakosoaji wa watawala hupitia, Mwalimu Nyerere akaibuka shujaa baada ya Tanganyika kupata Uhuru Desemba 9, 1961.

Kwa kushirikiana na mwanamapinduzi Mzee Abeid Amani Karume, wakaiunganisha Tanganyika na Zanzibar Aprili 26, 1964 na Oktoba mwaka huo, ‘Tanzania’ ikaingia rasmi katika historia ya dunia na Mwalimu kuwa Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mwalimu akaanza kujenga jamii kwa nguvu bila unafiki wala kujilimbikizia mali kutokana na nafasi aliyokuwa nayo.

Akajizatiti katika kujenga jamii isiyo na matabaka, jamii ya Tanzania ambayo watu wote ni sawa; isiyokuwa na matajiri na maskini, kwa kuwa wote walipaswa kunufaika na utajiri wa nchi yao bila kujali itikadi, dini, kabila, kanda wala ukoo.

Katika kuyatekeleza hayo, Mwalimu alipiga vita rushwa kwa nguvu na kwa wazi bila woga, alikomesha migawanyiko ya kikanda, kabila, dini na vyama na ili wote wanufaike na rasilimali za taifa, huduma muhimu za jamii ikiwamo elimu, zikatolewa bure kwa ngazi zote.

Mwalimu alisimamia misingi ya utu, uadilifu na uchapakazi huku masilahi ya umma yakiwa mbele kuliko matakwa binafsi na familia au jamaa zake wa karibu.

Akajenga miundombinu ya barabara, taasisi za serikali na kusisitiza miongozo mbalimbali iliyotafsiri mwelekeo wa taifa kwa wakati huo na wa baadaye bila kuathiri masilahi ya kizazi chochote.

Katika kutekeleza hilo, Mwalimu amewahi kunukuliwa akisema haikumpendeza kuchimba madini ya Tanzania na kuyauza Ulaya kwa mikataba aliyoiita ya kinyonyaji, akidai madini ni utajiri wa bure, zawadi ya Mwenyezi Mungu kwa Watanzania, hivyo kuyauza kwa hasara ni laana.

Kwamba kizazi kijacho kikisoma na kujua maovu hayo, kingelaani hata makaburi ya waliohusika. 

Mawazo haya ni uzalendo mkubwa na ucha Mungu wa hali ya juu katika uongozi wa umma, sifa ambazo viongozi wengi duniani wanazikosa.

Baadaye Mwalimu akaasisi misingi ya demokrasia kwa kuhamasisha na kusimamia mfumo wa vyama vingi vya siasa, akitoa kauli tata kwa chama chake, CCM, mara kadhaa, kuwa kisipojikita katika kutatua kero za wananchi, kuna siku kitaondoka madarakani. 

Hata haya ni mawazo ya kidemokrasia na imani ya kweli katika utekelezwaji wa demokrasia.

“CCM siyo baba wala mama yangu, ikiwa itaacha misingi tuliyoianzishia, nitaiacha.

“Chama cha siasa ambacho hakitatii maoni ya wananchi ipo siku kitalia na asiwepo wa kukifuta machozi,” sehemu ya kauli tata za Mwalimu Nyerere zilizoashiria alivyokuwa muumini wa demokrasia ya kweli inayojengwa katika mamlaka ya wananchi wenyewe na si kikundi cha koo fulani tu au chama fulani pekee kuamua nani awe kiongozi na nani atangazwe kushindwa uchaguzi.

Baada ya mengi mazuri aliyoyatenda Mwalimu Nyerere, hatimaye Oktoba 14, 1999, Tanzania, Afrika na dunia ilipigwa butwaa!

Ndiyo, ni simanzi baada ya aliyekuwa Rais wa Tanzania wa wakati huo, Benjamin Mkapa, kuutangazia umma kuwa Mwalimu Nyerere amefariki dunia. Mwisho wa Mwalimu ukawa hapo.

Tangu wakati huo, yapata miaka 22 sasa, siku hiyo imebaki kuwa muhimu kwa Tanzania wakiadhimisha kumbukizi ya mema na juhudi za Mwalimu katika ujenzi wa taifa na jamii ya Tanzania na juhudi zake za kuiona Afrika moja na dunia yenye watu wanaoishi kwa haki, utu na usawa.

Kwa hakika kuitaja pekee siku hii; kupumzika siku hii na viongozi kutoa hotuba tamu bila kuyaishi mema yake kwa vitendo, ni kejeli na dhihaka kwa Mwalimu.

Kama ukanda huu, ikiwamo, Tanzania ikiwa yenye kuumizana kwa tofauti za kisiasa na tamaa za madaraka, jamii aliyoiasisi Mwalimu Nyerere ikiwa ya wala rushwa, watoza gharama kwa watoto wa maskini katika huduma muhimu ikiwamo elimu, hatutakuwa na sababu ya kutaja jina la Mwalimu na kupumzika siku ya kifo chake.

Ni hekima ya kawaida tu kwa Watanzania wote kila mmoja kwa nafasi yake, viongozi na wananchi yatupasa kuendelea kuenzi tunu muhimu tulizoachiwa na mzee wetu huyu na hata tukilitaja jina lake katika siku yake muhimu baraka tutapata na si laana.

Katika kuadhimisha siku hii, hatuna budi kutafakari mwenendo wa demokrasia ya nchi yetu, hali ya rushwa katika jamii zetu, aina ya mikataba tunayoingia na mataifa ya nje katika uvunaji na matumizi ya rasilimali za nchi yetu, dhamira na dira ya watawala na jinsi wanavyojipambanua katika utatuzi wa kero za wananchi na uwezo wao katika kusikiliza maoni ya wananchi.

Hii isiwe siku ya kutaja jina la Mwalimu pekee na wanasiasa kutoa hotuba ndefu zenye kumsifia huku jamii ikilia, kero zikiwa lukuki na misingi aliyoiasisi katika kukabiliana na hayo ikiwa kando, hapo tutalaaniwa na jina lake kwani katika ulimwengu wa roho, ipo nguvu katika jina. 

Mwili wa Mwalimu ulikufa lakini nafsi ihai, inaishi, tumuenzi Mwalimu Nyerere.