Kumbe, mwanadamu huyu anaweza kutumia vitambulisho hivyo isivyostahiki eti arahisishe maisha yake. Ndipo anaweza kugushi hati na akafanikiwa kudanganya akapata riziki kwa kazi asiyokuwa na ujuzi nayo. Hapo ndipo anapotumia vyeti au hati feki.

Aidha ana utambulisho sahihi (hati au cheti) kwa elimu ya darasani aliyonayo akaamua tu kwa makusudi kabisa kutumia “kalamu” ya usomi wake kujiongezea kipato kwa majina ya marehemu au watumishi waliofungwa au waliostaafu au waliofukuzwa kazi. Hapo ndipo wanapatikana “watumishi hewa”.

Huu ni mtandao unaowahusisha wengi wilayani, mkoani hadi wizarani. Hundi za mishahara ya watumishi hewa au miradi hewa zinatolewa na fedha zake zinagawanwa kwa wahusika wote wa mtandao ule. Si suala la mtu mmoja wilayani. Ni mfumo wa wizi ulioota mizizi katika Serikali. Ni kundi la wasomi wanaokula fedha hizo. Wakurugenzi wateule wa rais wana kazi kweli kupambanua wasomi walafi hawa. Kila msomi ana mbinu zake za kula fedha hizo za watumishi hewa.

Msomi huyu anawabakiza katika orodha ya watumishi (in pay roll list) na fedha zao anazikomba. Basi, kusoma elimu ya darasani na kuitumia kwa ubinafsi namna hii ndio kunaonesha kutokuelimika kwa mhusika.

Kama kila msomi wa nchi hii angalielimika akatimiza wajibu wake kwa jamii iliyomsomesha, maendeleo ya nchi yangalikuwa kamili tangu enzi za utawala wa Awamu ya Kwanza.

Fedha zote zingalitumika kama inavyopangwa katika bajeti na kuidhinishwa na Bunge mimi sidhani kama kungalikuwa na ulazima au haja ya kuwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Laiti wasomi wote wangalikubali lile Azimio la Arusha, sidhani kama wangalitokea watumishi hewa hapa nchini. Azimio la Arusha liliweka wazi, nanukuu: “Tanzania is a nation of PEASANTS and WORKERS but it is not yet a socialist country” (Tazama Nyerere: Uhuru na Ujamaa (Freedom and Socialism) uk. 233 part two, the Policy of socialism (a) ibara ile ya tatu). Kwa tafsiri yangu isiyo rasmi ni kuwa nchini Tanzania kuna watu wa makundi mawili; moja ni la WAKULIMA na la pili ni la WAFANYAKAZI. Sote tunajua wakulima kamwe hawawezi kuwa wakulima hewa. Lakini hawa wafanyakazi ndimo wanatokea hao watumishi hewa.

Enzi zile za ukoloni ulikuwepo mfumo uliojulikana wa Utumishi wa Umma na katika Mashirika ya Umma. Kulikuwa na “The Civil Service”. Humo watumishi wote waliajiriwa na ndio tunaita Sekta Rasmi. Ni watumishi wanaolipwa ujira (wage earners) kila mwisho wa mwezi. Kumbe kule kwa wakulima wao wanajiajiri wenyewe na ndio sababu wanajulikana kama Sekta Isiyokuwa Rasmi (Self Employed). Hao hawana mshahara wa kila mwezi (not wage earners), bali wanakula kile wanachovuna.

Serikali ya mkoloni ilitoa mwongozo mahsusi wa ajira katika Tanganyika. Mwongozo ule ulisema hivi nanukuu:-

It is Government’s policy that the Civil Service, should as soon as may be possible without lowering standards, be wholly recruited from among the local inhabitants of the Territory. Government therefore wishes to attract as many well qualified and suitable candidates as possible into the service… The formal qualifications set out in chapter IV in respect of the posts described including University degrees, are British qualifications…. (Tazama Appointments at the Senior Levels in the CIVILSERVICE uk. 1 ibara 2 na 5).

Kwa tafsiri yangu isiyokuwa rasmi ni hivi: “Ni sera ya Serikali kwamba katika utumishi wa umma, bila kuathiri ubora wake, ajira zote zitolewe kwa wananchi. Serikali imetoa vivutio kwa wenye sifa zitakiwazo kuajiriwa katika utumishi wa umma. Sifa hitajika zimetolewa katika mwongozo huu katika sura ile ya IV ya kijitabu hiki. Humo kumeoneshwa aina za kazi (types of posts), mishahara, na wajibu zake. Hatimaye mwongozo ule ulisema vigezo vya elimu ni pamoja na shahada za Chuo Kikuu zenye hadhi ya Kiingereza (British qualifications) yaani Vyuo Vikuu vya Uingereza).

Angalizo hapa: Wakoloni walithamini zaidi vyeti vya Uingereza kuliko vile vya nchi nyinginezo zozote zile.

Sasa kwa mwongozo ule ulioitwa “Appointments at the Senior Levels in the civil Servivce” ulifuatwa kikamilifu kabla ya Uhuru na mpaka miaka michache baada ya Uhuru. Baada ya hapo ndipo wanasiasa wakaingizwa kwenye utumishi wa umma. Hapo ndipo, utaratibu ukavurugwa na hali ya utumishi wa umma ikabadilika. Sifa hazikufuatwa na ule uzoefu au seniority havikufuatwa tena.

Nathubutu kusema kuanzia hapo, basi taratibu na kanuni za Civil Service zikaborongwa. Leo hii tunapolia na watumishi hewa ni kule kuacha mila na kanuni za utumishi wa umma unavyotakiwa kuwa katika Serikali. Ni lazima utaratibu ule urudishwe katika utumishi wa umma. Hapo nidhamu ya kazi itakuwapo.

Wateule wote wa rais wakazanie kufuata na kuendeleza mila na kanuni za utumishi serikalini. Ni sifa moja ya utawala bora. Kama wanasiasa hawaingilii kazi za kitawala za Wakurugenzi, ma-RAS na ma-Katibu Wakuu kama ma-“Accounting Officers” ni wazi kabisa watumishi hewa hawatapatikana tena. Na wasomi wakielimika, vyeti fekie havitakuwapo ndipo vilaza hawataajiriwa katika utumishi wa umma.

Mimi naitakia Serikali hii ya Rais John Magufuli- ya Awamu ya Tano – mafanikio katika kurudisha nidhamu na maadili ya kazi katika utumishi wa umma na katika mashirika ya umma. Huu siyo UDIKTETA, bali ni kufufua mila na desturi za utumishi katika Taifa hili.

Wale wote waliozoea kupata bila kutoka jasho na nje ya utaratibu wa kiserikali lazima wataona ugumu ku-comply na sheria na kanuni za utumishi. Hapo sioni ajabu wakilalamika kuwa wanagandamizwa- basi wanaita UDIKTETA wa Rais Magufuli.

Lakini, daktari anayemtibu aliyevunjika mfupa akiwa na huruma hatanyoosha mifupa iliyoachana na kuifungia ule mhogo tuitao POP (Plaster of Paris). Hivyo kila mara pale daktari yule atakapojaribu kunyoosha mifupa iliyovunjika ili kuilinganisha na kuiweka sawa ipate kuungana, mhusika aliyevunjika atalalama kweli kwa maumivu makali anayopata.

Sote tunajua mifupa ile itaunga na yule aliyevunjika atapona na kuweza kutumia tena kiungo chake hicho. Hapo daktari yule hakuwa mkatili na wala hakuwa mdikteta, bali ni mtaalamu anayejua wajibu wa kazi yake na anaitenda kwa weledi kuponya mgonjwa.

Siyo lugha ya watu walioelimika kuita viongozi madikteta. Hapo ndipo narudia swali langu nani MSOMI na nani MWELIMIKA katika nchi yetu hii? Msomaji naomba unisaidie kujibu sahihi.

 

>>TAMATI>>