Imekuwa ni kawaida watu kubambikwa kesi hapa nchini. Mara nyingi matendo haya yamekuwa yakifanywa na watu wenye uwezo kifedha dhidi ya wasio na fedha pia kati ya maofisa wa polisi na raia. 

 Mtu kwa sababu ana pesa au cheo, anaweza kuamua kumfungulia yeyote mashtaka. Watu wengi wako magerezani kwa kubambikizwa kesi, hili wala si siri tena. Siseme walio mahabusu, hao nao hawana idadi. Inasikitisha mno.

 Ni wazi kuwa wengi wao wamefikia huko ama kwa kusingiziwa kosa na askari au mtu mwenye cheo au fedha. Lakini zaidi wametoka mikononi mwa askari kwa kuwa hata huyo mwenye cheo au fedha hawezi kumbambikiza mtu kesi bila kupitia kwa askari. Kwa hiyo askari ndiyo tatizo kubwa katika hili.

 

Nini maana ya kubambikwa kesi?

Kubambikizwa kesi au kumshtaki mtu kwa hila maana yake ni kumfungulia mtu kesi ya jinai bila mafanikio, na bila sababu za msingi za kufanya hivyo, mtu huyo anapata athari zozote kutokana na kumfungulia kesi hiyo. Athari ni pamoja  na kupotezewa muda, gharama, usumbufu, kudhalilishwa, kupata hasara kibiashara au kikazi kutokana na kushikiliwa na kila kitu ambacho kimekuwa kama  matokeo ya kusingiziwa kesi ni athari kwa maana hii.

 

Sababu za kubambika watu kesi

Sababu za kumuuzia mtu kesi huwa ni nyingi. Ni nyingi kutokana  na kuwa kila aliyebambikiwa kesi huwa kuna mgogoro nyuma uliosababisha  jambo hilo na migogoro kawaida inatofautiana. Pamoja  na hayo, sababu kuu za kubambikizia  mtu kesi huwa ni kwa ajili ya kumkomoa au kulipiza kisasi kutokana na chuki zilizotokana na mgogoro  kama  nilivyosema.

 

Weledi wa askari na kubambika raia kesi

Wakati mwingine askari wetu huwabambikizia watu kesi katika mazingira ya kushangaza kabisa. Askari  anaweza  kumbambikizia raia kesi kwa sababu tu raia  amehoji jambo fulani. Kwa mfano, mtu anaweza kumuuliza askari, “Nioneshe kitambulisho chako kabla hujanikamata.”

Utasikia askari akimwambia mtu, “Unajifanya mjuaji? Tutaona!” mara, “Unanifundisha kazi? Utanitambua…” na kadhalika. Eti mazingira kama hayo kwa askari wetu utakuwa tayari  ni mgogoro na mtu atapofikishwa kituoni basi ni rahisi  kupewa kesi ambayo si yake ilimradi tu askari aoneshe kuwa aliposema, “Utanitambua…” utaona  alikuwa  na uwezo wa kufanya hivyo kweli.

 

Athari za kuwabambikiza watu kesi

Kwanza upelelezi wa kesi ambayo haipo unagharimu pesa za Serikali na muda ambao kimsingi ungetumika kushughulikia kesi nyingine za watu wanaohitaji haki kiukweli. Pili, kesi hizi za kubambikizwa zinaongeza idadi ya kesi mahakamani pasi na sababu za msingi na hivyo kusababisha kesi za kweli kuendelea kuchelewa.

 Tatu, kesi hizi ni usumbufu kwa waliobambikizwa na ndugu zao na  zinaathiri nguvukazi katika Taifa kwani badala ya watu kuendelea na uzalishaji mali  hubaki kushughulikia kesi hizi zisizowahusu, na baadhi yao kufungwa kabisa na hivyo kupoteza moja kwa moja nguvukazi katika jamii.

 

Namna ya kumshtaki aliyekubambika kesi

Kushtaki ninakokuongelea hapa ni kushtaki kwa madai yaani kumdai aliyekubambikiza kesi akulipe kutokana na tendo  hilo ovu. Hivyo, hii itakuwa  ni kesi ya madai na hatua  zake  ni  hizi.

(a) Kwanza inategemea unataka akulipe shilingi ngapi. Kuanzia shilingi moja mpaka milioni tano utakwenda Mahakama ya Mwanzo. Ukifika hapo mahakamani utaeleza shida yako pale na watakusaidia kufungua kesi hiyo. Aidha, kuanzia milioni tano na kuendelea  Mahakama unayotakiwa kufungua kesi ni ya wilaya na Mahakama Kuu. Napo ukifika  mahakamani utaelekezwa utaratibu wa kufungua kesi lakini kwa Mahakama hizi ni vema ukamuona mwanasheria kabla ya kwenda mahakamani.

(b) Kwa ajili ya kufungua shauri  hilo utaratibu ni mwepesi kihivyo na bila  shaka  baada ya kufanya hayo utakuwa umefungua kesi ya kulipwa kutokana na kubambikizwa.

 

Mambo unayotakiwa kujiandaa nayo ili ushinde kesi ya kubambikizwa

(a) Kwanza hakikisha unatunza makaratasi yote yanayohusu ile kesi ya jinai uliyofunguliwa kwa kubambikizwa. Makaratasi (documents) hayo ndiyo yatakayotumika kuonesha kuwa kweli kesi ya jinai dhidi yako ilifunguliwa.

(b) Zingatia sana kuwa kubambikizwa kesi ni pale tu unapofunguliwa mashtaka polisi bila kujali mashtaka hayo yamefika mahakamani au hapana. Kitendo cha kufikishwa polisi kwamba umetenda kosa fulani wakati si  kweli tayari umebambikizwa kesi. 

(c) Pia kama ulibambikizwa kesi ikafika mpaka mahakamani na ukaachiwa huru, hakikisha unapata nakala ya hukumu inayoonesha kuwa uliachiwa huru kwa kuwa itakuwa ushahidi kuwa kesi haikuwa ya kweli na ndiyo maana Mahakama iliitupilia mbali.

(d) Tatu, jiandae kuonesha kuwa aliyekufungulia kesi alifanya hivyo bila sababu za msingi. Yaani ionekane wazi kuwa hapakuwa na sababu zozote za msingi za kufanya hivyo yaani kukufungulia mashtaka kama hayo.

(e) Pia andaa ushahidi au mashahidi ili kuonesha ni kwa kiasi gani uliathirika kutokana na kubambikizwa kesi ili uweze kupata pesa ulizoomba kulipwa. Kuathirika au kupata madhara kunakoongelewa hapa siyo lazima ziwe athari za kimwili tu. Zipo athari kama mtu kuharibiwa hadhi yake katika jamii, athari ya kumharibia mtu sifa njema katika jamii, na athari za kumpotezea mtu mali pamoja na muda kutokana na kesi hiyo.

Aidha, athari ya mali na muda inatokana na mtu kuacha kufanya shughuli zake na kuanza kushughulikia kesi hiyo ya uongo. Katika kufanya hivyo ni rahisi mtu kufukuzwa kazi au kupoteza kazi yake kwa namna yoyote ile ikiwa ni pamoja na kumharibia mtu mipango yake mbalimbali ambayo ingeweza kumwingizia kipato. Haya yote yanahesabika ni athari ambapo mtu aliyesababisha atatakiwa kuyafidia. Na hizo athari si lazima zitokee zote. Hata ikitokea moja kati ya hizi inatakiwa kufidiwa. 

(f) Jambo jingine la muhimu na la mwisho katika kufungua shauri la kubambikizwa kesi, ni kuwa lazima mashtaka aliyosingiziwa mtu yawe ni ya jinai. Yaani ulisingiziwa kutenda jinai kama kuiba, kubaka, kupiga, kutapeli, kutukana, kusingiziwa kumiliki silaha na kadhalika.

 

Kuhusu sheria za Ardhi, Mirathi, Ndoa Kampuni n.k. tembelea: sheriayakub.blogspot.com