Jiji la Dar es Salaam, na bila shaka majiji na miji mingine, hali ya ustaarabu mitaani imerejea. Mitaa inapitika na thamani kwa waenda kwa miguu imerejeshwa.
Bahati nzuri Watanzania wengi ni waelewa. Wapo waliodhani mpango wa kuwaondoa wamachinga katika maeneo yasiyostahili usingefanyika kwa utulivu.
Tunashukuru wengi walielewa, hivyo hapakuwapo vuta nikuvute mbaya. Hii ina maana Watanzania wakipangwa, wanapangika. Shida ni kwa wapangaji wenyewe!
Mara nyingi watu wastaarabu wamelalamika mno kuhusu uchafu, taswira ya hovyo na ya aibu ya miji na majiji yetu kutokana na kadhia hii ya biashara holela kila mahali.
Tuliokosoa hali hii tulifanya hivyo kwa kuamini kuwa Watanzania hatujafikia hatua ya kuishi kama mahayawani au watu tusiostaarabika. Haiwezekani tuishi kana kwamba ni viumbe tuliokosa akili ya kutambua jema na baya.
Juzi nilikuwa mjini Iringa – kuna kitu cha ajabu kinaendelea kwa muda mrefu. Nacho ni biashara ya majeneza. Barabara kuu ya kuingia na kutoka Iringa upande wa kusini imepambwa majeneza. Unakwepa jeneza unaingia hotelini.
Unakwepa jeneza unaingia duka la nyama kununua kitoweo. Unaingia kwa kinyozi wanaingia watu wanauliza bei ya majeneza!
Kwa hulka ya binadamu, hii si biashara ya kuitia wateja. Ni biashara inayohitaji staha fulani, lakini si kuipanga kana kwamba ni samani au mapambo.
Tena haifai majeneza kupangwa kwenye malango ya mapokezi hospitalini. Kuna wagonjwa wakishaona ‘hiyo kitu’ wanakata pumzi. Hawa wanahitaji kutengewa maeneo maalumu wafanye biashara zao.
Hali hiyo ndiyo iliyoikumba mitaa ya miji yote nchini kwa kupanga na kuuza bidhaa katika maeneo yasiyostahili. Tusipoanza leo kusafisha hali hii, hakuna atakayeweza kuirekebisha miaka mitano au 10 ijayo.
Lakini pia siyo sifa nchi kuwa na utitiri wa wamachinga kwa kigezo kuwa wanajiajiri. Sharti watunga sera na wananchi wote wenye mapenzi mema waketi na wainuke wakiwa na majibu ya kuondokana na huu uchuuzi.
Siyo sifa kuwa na idadi kubwa ya wachuuzi hata kama tungelipamba hili jambo kwa maneno ya dhahabu. Bahati mbaya bidhaa zinazochuuzwa ni za nje. Hakuna bidhaa za Tanzania. Huu ni utumwa wa kiuchumi.
Wanasiasa na wasomi walete majawabu ya ajira nchini. Waachane na majibu mepesi ya kuhalalisha umachinga na uendeshaji bodaboda kama tiba ya ajira.
Hauwezi kujenga uchumi wa watu na wa nchi kwa kuwahimiza waendeshe bodaboda au wauze sidiria na njiti za meno mitaani.
Nilikwisha kushauri, twende Misri tuone kinachofanywa – kuanzia kwenye umachinga hadi kwenye kilimo. Vijana wa Misri wenye shahada wanalima.
Serikali imewawekea mazingira mazuri mno. Twende tujifunze kwao. Hapa kwetu kilimo kimegeuzwa na kuonekana ni kazi ya wasiosoma!
Sasa wamachinga tumewaondoa mitaani. Mapambano hayawezi kwisha kirahisi namna hiyo. Watu hawa hawana ajira. Ninashauri: Serikali Kuu ishirikiane na Serikali za Mitaa kuandaa maeneo ya kudumu kwa kundi hili la Watanzania, maana tumeliunda na sharti lihudumiwe sasa.
Kwa mfano, serikali inaweza kwenda Manzese, ikaainisha nyumba 100. Ikalipa fidia nono kwa wenye nyumba wakahama.
Nyumba zikaondolewa na kukajengwa majengo makubwa ya ghorofa kadhaa kisha wakawekwa wamachinga. Unakuwa na ghorofa la nguo za kina mama, kina baba; unakuwa na ghorofa kwa nguo za watoto pekee, unakuwa na ghorofa kwa vifaa vya urembo tu, n.k. Tufanye hivyo Temeke, Tandale, Mbezi Louis, Kunduchi, nk.
Hayo hayo yafanywe katika miji yote mikubwa kama Mwanza, Mbeya, Arusha, Moshi, Dodoma, Iringa n.k.
Tukishamaliza, umachinga urasimishwe kwa madaraja. Walipe kodi. Hii sifa ya kuwa watu wanyonge hawalipi kodi na badala yake wanaolipa ni watu wachache sana, ni ya kinyonyaji. Matajiri wengi wamepenya humo kwa sababu wanajua hakuna kodi. Hauwezi kuwa na mtaji wa Sh milioni 200 halafu unalipa kodi ya Sh elfu 20 pekee kwa mwaka. Huo ni unyonyaji.
Jingine, ninashauri wanasiasa waache kuvuruga taratibu za nchi kwa sababu na matamanio yao ya kisiasa.
Kuna njia nzuri za kuwasaidia wanyonge bila kuvunja sheria za halmashauri na za nchi. Kitendo cha kuamuru wamachinga waachwe wafanye biashara popote wanapotaka bila bughudha kilikuwa cha kuvuruga na pengine kuifanya nchi isitawalike.
Ni zigo analoachiwa anayefuata. Rais wa sasa analaumiwa kwa ‘rumbesa’ iliyoandaliwa na mtangulizi wake. Lakini kama tangu awali tungesimamia utengaji wa maeneo kwa ajili ya wamachinga, haya manung’uniko ya hapa na pale yasingekuwapo.
Tuwe na siasa za kuvutia kura bila kuathiri utawala wa nchi. Na hapo ndipo unapoona umuhimu wa kuwa na Katiba inayozuia amri na maagizo hatarishi kama haya ya watu kufanya chochote wanachotaka kufanya popote.
Pamoja na kuafiki suala la kuwaondoa wamachinga, inasikitisha kuona hata wale walio nje ya miji na ambao hawaleti kero yoyote, nao wanaondolewa. Hapana. Wenye mamlaka wasivuke mipaka ya utu. Maeneo kama Luguruni kuna sababu gani kuwaondoa hawa watu?
Mwisho, tuombe mamlaka husika zisione kuwaondoa wamachinga kuwa ndiyo kazi imekwisha! Kazi bado wanayo, tena kubwa – kuhakikisha wanawapatia maeneo ya kuendeshea shughuli zao. Wasichekelee na kuanza kujipongeza baada ya kuwaweka kando.
Wasipoandaliwa mazingira, kero za uhalifu watakazoleta zitatufanya tuseme heri kero walizosababisha wakiwa wamevamia maeneo yasiyostahili.
Mara zote mamlaka zijitahidi kupata majibu ya kudumu kadiri inavyowezekana ili kuinusuru amani yetu. Katika hili Rais Samia asikatishwe tamaa wala kuandamwa, maana si yeye aliyeliunda. Hatuna budi kuishi kistaarabu.