Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt.Batilda Burian amesema suala la kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga sio jukumu la wizara ya Afya pekee hivyo ni muhimu kila sekta kuweka mikakati ya pamoja.
Balozi Burian amebainisha hayo mkoani Tabora katika ufunguzi wa kikao cha watalaam wa Afya Kanda ya Magharibi inayounda mikoa Tabora ,Katavi na Kigoma cha kujadili mikakati ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga katika kanda hiyo.
“Maelekezo ya Wizara ya Afya ni kuhakikisha kila halmashauri inaweka mikakati ya kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga hivyo suala hili ni mtambuka sio tu la Wizara ya Afya ni la sekta zote ,sisi viongozi ni kuhakikisha kuwa tunasimamia masuala haya ya Afya ya msingi na afya ya uzazi na watoto ili vifo hivi vipungue .
“Sababu zinazochangia vifo ni kutokana na kupoteza damu nyingi kabla ya kujifungua na baada ya kujifungua ,sasa tunafanyaje watu wa kilimo wanafanyaje,katika bustani zao wanakuwa na mbogamboga ,rozela inayosaidia kuongeza damu”amesema.
Katika hatua nyingine mkuu huyo wa mkoa ameagiza vituo vyote vya kutolea huduma katika mkoan wa Tabora vyenye TV kuweka jumbe zenye maudhui ya Afya ili mwananchi anaposubiri kupatiwa huduma anapata ujumbe sahihi wa Afya badala ya kusikiliza muziki .
Kuhusu takwimu za vifo vitokanavyo na uzazi katika Kanda ya Magharibi yenye mikoa ya Tabora, Kigoma na Katavi kwa miaka mitatu mfululizo Balozi Dkt.Burian amesema Mwaka 2019 akina mama wajawazito 210 walipoteza maisha; ambapo, Kigoma vilikuwa vifo 100, Tabora 62 na Katavi 48.
Mwaka 2020 akina mama 235 walipoteza Maisha; ambapo Kigoma vilikuwa vifo 119, Tabora 58 na Katavi 58, na Mwaka 2021 akina mama 174 walipoteza Maisha; ambapo Kigoma vilikuwa vifo 75, Tabora vifo 58 na Katavi vifo 41.
Ametaja sababu kubwa zilizosababisha vifo vya wajawazito ni pamoja na Kutokwa damu nyingi baada ya kujifungua,Kifafa cha mimba, Kupasuka mfuko wa Uzazi,Kutokwa na damu nyingi kabla ya kujifungua, Upungufu mkubwa wa damu,Uambukizo wakati na baada ya kujifungua huku hali ya vifo Mwaka 2020 vitokanavyo na uzazi kitaifa vilikuwa 1,640 na Mwaka 2021 vilikuwa 1,588.
Takwimu za vifo vya watoto wachanga kuanzia siku 0-28 katika Kanda ya Magharibi kwa mwaka 2021 ni watoto wachanga 2,539 walipoteza maisha; ambapo Kigoma vilikuwa ni vifo 1,026, Tabora vifo 954, na Katavi vifo 559 kushindwa kupumua, watoto kuzaliwa njiti,uambukizi kwa watoto wachanga,na kuzaliwa na uzito pungufu.
Katika kiwango cha mimba za utotoni kanda ya Magharibi Balozi.Dkt.Burian amesema Mkoa wa Katavi ni asilimia 25.2, Tabora asilimia 17 na Kigoma asilimia 11.9 na hudhurio la kwanza la wajawazito chini ya wiki kumi na mbili kwa mkoa wa Tabora ni silimia 34.4, Katavi asilimia 41 na Kigoma asilimia 54.9 na kiwango cha utumiaji wa njia za kisasa za uzazi wa mpango kwa mkoa wa Katavi ni asilimia 41,Kigoma asilimia 46.4,na Tabora ni asilimia 60.1.
Hivyo,Mkuu huyo wa Mkoa ametoa maagizo ya Kuongeza uwajibikaji katika usimamizi na utekelezaji wa mipango mikakati itakayoandaliwa ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga, kudhibiti mimba na ndoa za utotoni, elimu ya Afya itolewe kwenye jamii kupitia njia mbalimbali za mikusanyiko ya watu, mashuleni, makanisani na misikitini, vyombo vya habari na wanaowapa mimba watoto wa shule sheria ichukue mkondo wake ili kudhibiti vitendo hivyo.
Maagizo mengine ni Mikoa ihakikishe Halmashauri zinakusanya damu ili vituo vya kutolea huduma za Afya hasa Hospitali na Vituo vya Afya viweze kuwa na damu ya kutosha kwa ajili ya kuokoa maisha ya wajawazito na watoto chini miaka mitano na wagonjwa wengine.
Afisa Programu Wizara ya Afya,Idara ya Afya ya Uzazi ,Mama na Mtoto Jackline Ndanshau amesema lengo la kikao hicho kilichoandaliwa na Wizara ya Afya ni kujadili mikakati ya kupunguza vifo vya uzazi na watoto wachanga na kupokea taarifa ya mwaka mzima .
Mganga Mkuu Mkoa wa Kigoma Dkt.Jesca Lebba amehimiza umuhimu wa ushirikishwaji katika ngazi mbalimbali za uongozi kujadili kupunguza vifo vya mama na mtoto.