Wazazi wengi wanaishia tu kwenye hatua ya kuzaa, hawaendelei na hatua ya kulea. Hapo tulio wengi tunachemka. Methali ya Kiswahili yatuambia hivi; ‘Kulea mimba si kazi, kazi ni kulea mwana’.

 Wapo wazazi wanaojiita ni wazazi lakini hawatambui wajibu wao kama wazazi. Uozo wa kimaadili tunaouona katika jamii yetu unaonesha uhalisia wa familia zetu. Kwa tunayoyaona yakitendeka kwenye jamii yetu tusiwalaumu watoto wetu, tusiilaumu Serikali, tusiwalaumu viongozi wa dini badala yake tujilaumu sisi wazazi, walezi na wanajamii wote kwa kushindwa kuhimili jukumu letu la malezi.

Kizazi cha leo kimekosa ushirikiano wa malezi. Kila mmoja anajiona mlezi anayestahili kutunukiwa tuzo ya ‘Nobel’. Hakika tunahitaji kuhurumiwa. Wazazi na walezi ndiyo chanzo cha kuporomoka kwa maadili katika jamii yetu. Tubadilike, methali ya Kiafrika inauthibitisha ukweli huu ninaousema kwamba, ‘Kuporomoka kwa taifa kunaanzia nyumbani.

Wazazi na walezi tumechangia kwa sehemu kubwa kuyumbisha misimamo na ndoto za watoto wetu kuyeyuka. Ni watoto wangapi wananyimwa haki yao ya msingi ya kusoma? Ni watoto wangapi wanafanyiwa ukatili na wazazi wao ama walezi wao?

 Ni wengi kwa hakika. Wazazi wameaminishwa na Mwenyezi Mungu kuwalea, kuwalisha na kuwatunza watoto wao kwa afya bora na malezi safi. Kwa jinsi hiyo wazazi watadaiwa kutoa hesabu ya jukumu lao hili kubwa mbele ya kiti cha enzi cha Mwenyezi Mungu, ikiwa kweli waliwalinda na kuwafunda watoto wao na kuwalea kwa maadili yanayompendeza Mwenyezi Mungu.

 Wazazi wana jukumu la kuishi maisha ya mfano bora ili na watoto wao waishi maisha ya mfano bora katika jamii. Kama nilivyodokeza hapo awali ni kwamba tukumbuke ipo siku sisi wazazi na walezi tutasimama mbele ya kiti cha enzi cha Mungu.

 Tutajibu nini? Tuliowatelekeza watoto wetu tutajibu nini? Tuliozikimbia familia zetu kwa kukwepa majukumu yetu ya ubaba na umama tutajibu nini? Tunaofurahia anasa za dunia na wakati huo huo watoto wetu wanapata mlo mmoja kwa siku tutajibu nini?

Tulio na watoto wanaojiita ombaomba kwenye miji yetu tutajibu nini? Sijui tutajibu nini, na tena sijui tutajibu nini. Mwandishi wa Kijapani Mineko Iwasaki anasema, “Choma mwili kisu utapona, lakini jeruhi moyo na jeraha lake litaishi maisha yote”.

Watoto wengi wana majeraha. Wana majeraha ya kukosa malezi bora kutoka kwa wazazi na walezi wao. Wana majeraha ya kukosa upendo kutoka kwa wazazi na walezi wao. Wana majeraha ya kukosa msamaha kutoka kwa wazazi na walezi wao. Wana majeraha ya kukosa ushauri kutoka kwa wazazi na walezi wao.

Wamejeruhiwa na kujeruhika. Mshairi wa Kijerumani Wolfgang Von Goethe alipata kutuasa kwa busara hii, “Nina uwezo mkubwa mno wa kuyafanya maisha yawe ya uchungu au ya furaha. Nina uwezo wa kuwa chombo cha maumivu makali au chombo cha kuvutia, naweza kunyanyasa au kutia hamasa, kuumiza au kuponya. Kama tukiwatendea watu kadiri walivyo, tunawafanya wanakuwa wabaya zaidi. Kama tukiwatendea watu kama wanavyopaswa wawe tunawasaidia kuwa namna wanavyoweza kuwa”.

 Tuwalee watoto wetu kwa imani ya dini zetu. Wamtambue Mwenyezi Mungu. Wampende Mwenyezi Mungu. Wamuheshimu Mwenyezi Mungu. Malezi ya mtoto pasipo imani ni kama suruali isiyo na zipu. Kuna profesa aliyekuwa anawafundisha wanafunzi, siku moja akamwambia mwanafunzi mmoja, “Una habari kwamba hakuna Mungu”. Mwanafunzi akabisha, profesa akamwambia mwanafunzi; Tazama nje, unaona nini? Mwanafunzi akasema, naona miti, watu, nyasi na wanyama. Profesa akasema, “Unaona! Hakuna Mungu”. Je, umemuona “Mungu?” Mwanafunzi akasema hapana sijamuona Mungu huko nje.

 Mwanafunzi mwingine, akasema ngoja profesa mimi nimuulize maswali huyo mwanafunzi mwenzangu. Akaanza kumuuliza mwanafunzi mwenzake maswali. “Ukimtazama profesa unaona nini?” Mwanafunzi mwenzake akasema, “Naona nywele, ngozi, viatu, saa na simu ya mkononi.” 

Akaulizwa tena, je, unaona akili ya profesa? Mwanafunzi mwenzake akajibu akasema, “Hapana siioni akili ya profesa’’. Mwenzake akamuuliza tena; je, tunaweza kusema profesa hana akili? Profesa baada ya kusikia hivyo akaja juu. Akaambia hivi, “Kama vile ambavyo hatuoni akili ya profesa lakini tunaamini anayo. Ndivyo mambo yalivyo kwa Mungu. Hatumuoni lakini yupo”

 Tunaishi kwa imani na si kwa kuona. Tunajifunza nini kutokana na hadithi hii. Mwanafunzi huyu alikuwa ameaminishwa na wazazi wake kwamba kuna Mungu aliyeumba vinavyoonekana na visivyoonekana. Wazazi na walezi wa siku hizi wamejiaminisha kwamba wao peke yao wanaweza kuwalea watoto wao pasipo kupata msaada wowote ule kutoka kwa Mwenyezi  Mungu.

Ukweli ni kwamba wazazi na walezi wa aina hii hawana msaada wowote ule kwa watoto wao zaidi ya kuwapoteza watoto wao katika ulimwengu wa giza. 

Natamatisha makala hii kwa maneno haya; mtoto ni malezi, malezi ni wimbo, uimbe. Malezi ni mchezo, ucheze. Malezi ni changamoto, ikabili. Malezi ni ndoto, ielewe. Malezi ni sadaka, itoe. Malezi ni upendo, ufaidi. Malezi ni lengo, lifikie. Malezi ni njia, ipite. Malezi ni mti, upande. Malezi ni gharama, igharamie. Malezi ni msalaba, ubebe.