Wiki iliyopita katika mfululizo wa makala hii tuliishia pale mwandishi aliposema ni nani amewaandalia haya mazingira? Ni mimi au wewe?
Ni yule au wao wenyewe? Jibu ni si yule wala wale, si yeye. Ni mimi na wewe, kwa nini ni mimi na wewe? Malezi bora ndiyo yanayowaandaa watoto kifikra na kitabia.
Maisha ya mtoto wako na msingi uliompa leo ndio utakaowezesha maisha bora ya mama na baba bora wa kesho, baba na mama wema wanaandaliwa leo. Dunia ya leo ina wazazi wengi, lakini wazazi na walezi bora ni wachache.
Kwa maneno mengine tunaweza kusema hivi, dunia ina wazazi kuliko walezi. Papa Yohana wa XXIII alipata kuandika hivi: “Ni rahisi kwa baba kuwa na watoto kuliko watoto kuwa na baba wa kweli.”
Wapo wazazi ambao kazi yao ni kufurahia tendo la ndoa tu pasipo kutambua gharama zake kwa baadaye. Kuna kuzaa na kulea. Kuzaa ni hatua nyingine na kulea ni hatua pia.
Hizo zote ni hatua muhimu za kumwandaa mtoto ili akue katika mazingira mazuri. Wazazi wengi wanaishia tu kwenye hatua ya kuzaa, hawaendelei na hatua inayofuata ambayo ni kulea.
Hapo tulio wengi tunachemka, kuna methali ya Kiswahili inayosema: “Kulea mimba si kazi, kazi ni kulea mwana.” Wapo wazazi wanaojiita ni wazazi lakini hawatambui majukumu yao kama wazazi.
Uozo wa kimaadili unaoonekana katika jamii yetu unaonyesha uhalisia wa familia zetu. Kwa tunayoyaona yakitendeka kwenye jamii yetu tusiwalaumu watoto wetu, tusiilaumu serikali, tusiwalaumu viongozi wa dini, badala yake tujilaumu sisi wazazi.
Kizazi cha leo kimekosa ushirikiano wa malezi. Kila mmoja anajiona mlezi anayestahili kutunukiwa tuzo ya Nobel. Hakika tunahitaji kuhurumiwa. Wazazi na walezi ndio chanzo cha kuporomoka kwa maadili katika jamii yetu, tubadilike.
Wazazi na walezi tumechangia kwa sehemu kubwa kuyumbisha misimamo na ndoto za watoto wetu kuyeyuka. Ni watoto wangapi wananyimwa haki yao ya msingi ya kusoma, ni watoto wangapi wanafanyiwa ukatili na wazazi wao ama walezi wao?
Kwa hakika ni wengi, wazazi wanalo jukumu la Kimungu la kuwalea, kuwalisha na kuwatunza watoto wao kwa afya bora na malezi safi, kwa jinsi hiyo wazazi watadaiwa kutoa hesabu ya jukumu lao hilo kubwa mbele ya kiti cha enzi cha Mwenyezi Mungu.
Wazazi wana jukumu la kuishi maisha ya mfano bora ili watoto waishi maisha ya mfano bora katika jamii. Kama nilivyosema hapo awali, tukumbuke ipo siku sisi wazazi na walezi tutasimama mbele ya kiti cha enzi cha Mungu, tutajibu nini?
Tuliowatelekeza watoto wetu tutajibu nini? tuliozikimbia familia zetu kwa kukwepa majukumu yetu ya ubaba na umama tutajibu nini? Tunaofurahia anasa za dunia na wakati huo watoto wetu wanapata mlo mmoja kwa siku tutajibu nini?
Tulio na watoto wanaojiita ombaomba kwenye miji yetu, tutajibu nini? Mwandishi wa kijapanI, Mineko Iwasaki, anasema: “Uchome mwili kisu utapona, lakini jeruhi moyo na jeraha lake litaishi maisha yote.”
Watoto wengi wana majeraha! Wana majeraha ya kukosa malezi bora kutoka kwa wazazi na walezi wao, majeraha ya kukosa upendo kutoka kwa wazazi na walezi wao.
Watoto hao wana majeraha ya kukosa msamaha kutoka kwa wazazi na walezi wao. Wana majeraha ya kukosa ushauri kutoka kwa wazazi na walezi wao.