Nimesukumwa kuandika makala hii kutokana na ukweli kwamba hatuwezi kujenga taifa lenye maadili mema pasipokuwa na familia zenye maadili mema. Ustawi wa taifa unaanzia nyumbani. Kinyume chake ni kuporomoka kwa taifa kunakoanzia nyumbani.

Uhai wa taifa unategemea uhai wa familia. Tunapashwa kutambua kuwa mafanikio ni tunda la bidii. Methali ya Kichina inasema hivi, ‘Ukinieleza nitasahau’, ‘ukinionesha nitasahau’, ‘bali tukishirikiana nitaweza’.

Ni hakika wazazi na walezi wana ulazima wa kushirikiana katika malezi na makuzi ya watoto. Methali ya Kichina inaupambanua ukweli mwingine kwa kusema, ‘Hali ya nchi inaonekana nyumbani’.

Papa Yohana Paul wa II alipata kuandika hivi, ‘Namna familia inavyoenda, ndivyo taifa linavyoenda na ndivyo dunia yote inavyoenda’. Maadili mema ni uhai. Maadili mema ni uhai kwa taifa. Maadili mema ni uhai kwa familia.

Ni hakika jamii ya ulimwengu haiwezi kuukataa ukweli wa Hans Kung kwamba, ‘Pasipo maadili hakuna uhai’. Hatuwezi kuendelea kiroho, kimwili, kiuchumi, kisiasa, kijamii pasipokuwa na maadili yanayompendeza Mungu na binadamu wenzetu wanaotuzunguka. Matatizo mengi yanayoikabili jamii yetu yana chanzo chake katika tabia.

Tabia ndiyo chanzo cha matendo tunayoyaona kama kukosekana kwa uaminifu, ubadhirifu wa mali za umma, ufisadi, migororo ya ndoa, misuguano ya kijamii, ugaidi, unyanyapaa na kadhalika. Yote haya yana chimbuko lake. Mtoto anapozaliwa ni kama malaika. Hana kosa anapokuwa amezaliwa. Anakuwa mgeni aliyeleta habari njema kwenye familia. Wazazi, ndugu na jamaa hufurahi kumpokea mtoto aliyezaliwa.

Jambo gani linatokea baadhi ya watoto wanapokuwa wanabadilika? Tunapokuwa tunazungumzia maadili ya ulimwengu wa sasa kwamba yameyumba, lazima kwanza tutupie jicho letu kwenye familia zetu. Tuelewe kwamba jukumu la kujenga Taifa letu ama kulibomoa Taifa letu tunao sisi wazazi, walezi na wanajamii.

Mwandishi wa kitabu cha Mithali, ameandika kwa ufasaha kabisa kwamba “Mlee mtoto katika njia impasayo naye hataiacha hata atakapokuwa mzee’’ (Mithali 22:6). Na wahenga wetu walipata kunena ‘Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo’’. Mtoto ni malezi. Malezi bora ni ufunguo wa maisha kwa mtoto. Malezi bora ni urithi wa milele kwa mtoto.  Taifa bora la kesho linategemea malezi bora yanayotolewa na taifa bora la leo. Malezi bora ndiyo mwelekeo sahihi wa maisha ya mtoto. Kesho bora ya mtoto inajengwa na leo bora ya mzazi bora. Watoto wa leo ni raia na viongozi wa kesho, ndiyo watakaokuwa sifa au aibu kwa wazazi wao, kwa familia yao, kwa jamaa na taifa lao.

Papa Fransisko ameandika kwa ufasaha usiopingika, “Mtoto ambaye amejifunza katika familia kuwasikiliza wengine, kuzungumza kwa heshima na kueleza maoni yake pasipo kupuuza ya wengine, atakuja kuwa na nguvu ya mazungumzo na mapatano katika jamii’’.

Familia ni kitalu cha haki, amani na upatanisho. Familia bora hujenga jamii bora. Ndiyo maana tunathubutu kusema kwamba umaarufu wa jamii unatokana na familia zilizo safi. ‘Familia ni jumuiya ya msingi; ndicho chanzo cha uhai mpya wa binadamu; ndicho kituo cha kwanza ambamo mtu anaweza kupata maendeleo ya kiroho, kimaadili na kimwili kwa ukamilifu.’

Ni tafakuri iliyotolewa na Baraza la Maaskofu Wakatoliki wa Tanzania kupitia ujumbe wao wa kwaresma wa mwaka 2010. Familia imara ni msingi wa taifa bora la nchi. Pasipo familia taifa halitakuwapo. Familia ni shule ya malezi na makuzi bora. Familia ni shule ya kusamehe na kusamehewa, kupenda na kupendwa. Familia ni mbingu ndogo ya wanafamilia ambapo watoto na wazazi wanaishi maisha ya kimapendo, kindugu na kirafiki. Familia ni hospitali ya kwanza iliyo karibu zaidi na wagonjwa.

Padre Festo Mkenda SJ anasema, upendo wa baba na mama ni mfano bora kwa watoto. Uhusiano ulio imara wa taifa na wenye kujaa baraka unajengwa kwanza kwenye ngazi ya kifamilia. Ni ukweli kwamba kama familia hazielewani ni hakika hata taifa halitaelewana. Methali ya Kijerumani yatujuza; “Upendo huanzia nyumbani.’’ 

Mchungaji A. W. Tower alipata kunena haya; “Malezi bora kwa mtoto ni lulu kwa ulimwengu.” Kesho bora ya mtoto inajengwa na leo bora ya mzazi bora. Methali ya Kiswahili inatukumbusha maneno haya, “Samaki mkunje angali mbichi.” Itakuwa ni biashara isiyolipa kumkunja samaki akiwa mkavu. Atavunjika, na utapata hasara ambayo pengine hukutarajia kuipata.

Nakubaliana na Frederick Douglass kusema, “Ni rahisi sana kujenga watoto imara kuliko kukarabati watu wazima waliovunjika.” Mzazi au mlezi unatakiwa uwe mlezi saa ishirini na nne. Unatakiwa uwe mlezi siku saba za wiki. Unatakiwa uwe mlezi siku 30 za mwezi. Unatakiwa uwe mlezi siku 365 za mwaka. Malezi hayana likizo. Malezi ni utumishi. Malezi bora ndiyo yanayowaandaa watoto kifikra na kitabia. 

Tafakari kesho ya mtoto wako umeiandaaje? Jielewe kwamba wewe ni mzazi na mlezi. Chukua nafasi yako kama mzazi. Malezi ni kulea na kujilea. Mzazi au mlezi unapomlea mtoto wako usisahau na wewe kujilea. Maisha unayoishi wewe mzazi yana maana kubwa sana kwa wanao kuliko maneno unayowaambia.

Padre Anton wa Padua aliyeishi karne ya 14, kila alipokuwa akianza mahubiri alikuwa anawaambia waumini wake maneno haya, “Matendo yanaongea zaidi kuliko maneno.’’ Maneno yanafutika lakini matendo hayafutiki.

David Oyedepo amepata kuandika haya, “Wazazi wanapaswa kuwaongoza watoto wao kwa wao wenyewe kuwa mfano bora kwa matendo yao, kwa kuwa watoto huiga kile kinachofanywa na wazazi wao’’. Watoto ni waigaji wakubwa wa mambo. Maisha unayoishi yana mfano gani kwa watoto wako?

Mwanafalsafa Tolmons alipata kuandika hivi; “Katika maisha unayoishi unaweza kuonesha sura ya Mungu au sura ya shetani.’’ Kazini kwako unaweza kuonesha sura ya shetani au sura Mungu. Kwenye familia yako unaweza kuonesha sura ya shetani au sura ya Mungu. Kwa majirani zako unaweza kuonesha sura ya shetani au sura ya Mungu. 

Inategemea maisha yako unayoishi yanawakilishwa na matendo ya aina gani. Vivyo hivyo, katika maisha unayoishi unaweza kuwa chachu ya mabadiliko ama ukawa mhanga wa mabadiliko. Tupembue tuone. Ufisadi ni sura ya shetani. Rushwa ni sura ya shetani. Uchu wa madaraka ni sura ya shetani. Uchawi ni sura ya shetani. Uchoyo ni sura ya shetani. Umbea ni sura ya shetani. Udini ni sura ya shetani. Biashara haramu kama ya dawa za kulevya ni sura ya shetani. Wizi wa pembe za ndovu na meno ya tembo ni sura ya shetani. Ukahaba ni sura ya shetani.

Kwa upande mwingine pia tuone Mungu anawakilishwa na sura ya namna gani. Sura ya Mungu ni sura ya uadilifu na uaminifu. Sura ya Mungu ni sura ya upendo. Sura ya Mungu ni sura ya amani. Sura ya Mungu ni sura ya mshikamano. Sura ya Mungu ni sura ya unyenyekevu na huruma. Leo unaposoma makala hii amua unapenda maisha yako yawakilishwe na sura ya nani, sura ya Mungu au shetani? Ulimwengu na watu wake unalia kwamba maadili yameporomoka. Kwa uhalisia wake ni kweli maadili yameporomoka. Lakini kwa nini maadili yameporomoka? Nani wa kulaumiwa katika hili? Ni mtoto au mzazi? Ni viongozi wa dini au mzazi? Ni viongozi wa serikali au mzazi? Nani wa kulaumiwa? 

Kwa hakika mimi na wewe hatuwezi kukwepa kulijibu swali hili. Chanzo cha maadili kuporomoka katika jamii yetu ni nini? Ni ukweli usiohitaji hoja kwamba wanaoharibu ulimwengu kwa matendo yao maovu hawajatokea vichakani wala kuzaliwa na wanyama, bali wametokea kwenye familia zetu. Wengi tunaishi nao, ni ndugu zetu. Lakini kwa nini wamegeuka kuwa magaidi? Kwa nini wamegeuka kuwa mashoga? Kwa nini wamegeuka kuwa mafisadi? Kwa nini wamegeuka kuwa malaya wa kuuza miili yao? Ni kwa nini? Tena ni kwa nini? Nani amewaandalia haya mazingira? Ni mimi? Ni wewe? Ni yule? Ni wao wenyewe? Ni nani?

Jibu ni hili; siyo yule, siyo wale, siyo yeye. Ni mimi na wewe. Kwa nini ni mimi na wewe? Malezi bora ndiyo yanayowaandaa watoto kifikra na kitabia, maisha ya mtoto wako na msingi uliompa leo ndiyo utakaowezesha maisha bora ya mama na baba bora wa baadaye. Baba mwema na mama mwema wanaandaliwa leo.

Dunia ya leo ina wazazi wengi, lakini wazazi na walezi bora ni wachache. Kwa maneno mengine tunaweza kusema hivi; dunia ya leo ina wazazi wengi wa kuzaa na si wazazi wengi wa kuzaa na kulea. 

Papa Yohana wa XXIII alipata kuandika hivi, “Ni rahisi kwa baba kuwa na watoto kuliko watoto kuwa na baba wa kweli”. Ni kweli, wababa wa kweli ni wachache. Wababa wa kutoa mbegu ni wengi, lakini wababa wa kulea ni wachache. Wababa wa kuzaa ni wengi lakini wababa wa kuandaa kesho njema ya mtoto ni wachache. 

Wapo wazazi ambao kazi yao ni kufurahia tendo la ndoa tu pasipo kutambua gharama zake kwa baadaye. Kuna kuzaa na kulea. Kuzaa ni hatua nyingine na kulea ni hatua nyingine. Zote ni hatua muhimu za kumwandaa mtoto ili akue katika mazingira mazuri.

 

>>ITAENDELEA