Kupendwa ni mtihani. Kupenda ni kujiweka katika hatari ya kutopendwa. Lakini hatari kubwa ni kutojiweka katika hatari. Kupenda si kazi, kazi ni kumpata akupendaye. Kuna methali ya Wahaya isemayo: “Mwereka wa mzazi unaomwangukia mtoto, si mwereka wa mtoto unaomwangukia mzazi.”
Mzazi anajitaabisha kukidhi mahitaji ya mtoto, lakini baadaye mtoto hajitaabishi kukidhi mahitaji ya mzazi. Kwa msingi huu kupendwa ni mtihani. Kuna mtoto mdogo aliyenunuliwa kinyago na mama yake. Siku moja alimwambia mama yake: “Nakipenda kinyago hiki lakini chenyewe hakinipendi.”
Kuna wanandoa ambao mwenzi aliyenaye si yule aliyempenda awe mwenzi wa ndoa, labda yule alichukuliwa na mwingine. Katika mazingira haya kuna kazi kumpata akupendaye. Upendo una sura mbili, kupenda na kupendwa. Mwanamuziki, Justin Kalikawe, katika moja ya nyimbo zake alisema kuwa katika msiba wa maskini kuna wana ukoo tu, katika msiba wa tajiri kuna umati wa watu. Hapa kwa baadhi ya wanaohudhuria msiba wa tajiri hapendwi mtu ila vitu. Kupendwa ni mtihani. George Eliot alisema: “Sitaki kupendwa tu, nataka niambiwe kuwa ninapendwa.” Unayempenda mwambie kuwa unampenda.
Upendo unaweza kumfanya bubu aseme. Upendo unaongea. “Upendo ni lugha ambayo kiziwi anaweza kusikia. Upendo ni wimbo ambao mlemavu wa miguu anaweza kuucheza. Upendo ni mapambazuko ambayo kipofu anaweza kuona,” alisema Ramesh Umadleat.
Kiziwi akipendwa atasikia, atajua. Kipofu akipendwa, ataona – yaani ataona kwa macho ya moyo na macho ya akili, ataelewa, atatambua. Upendo ni kama kikohozi, hakifichiki. Upendo una sifa mbili: kutoa na kupokea. Haitoshi kutoa, lazima kupokea. Unapopewa na wewe ina maana unapendwa.
Kijana alimwambia mchumba wake kuwa anampenda. Lakini aliongeza maneno haya: “Sina gari zuri kama la Yakobo na sina nyumba nzuri kama ya Yakobo.” Msichana alimwambia: “Nakupenda pia lakini niambie habari zaidi juu ya Yakobo.”
Katika kisa hiki tukisoma kilichoko nyuma ya pazia tunaweza kusema, tayari msichana alianza kumtamani Yakobo na vitu vyake. Kupendwa ni mtihani. Msichana alimuuliza mchumba wake: “Je, unanipenda?” Mchumba wake alijibu: “Ndiyo mpendwa.” Msichana alizidi kudadisi: “Unaweza kunifia?” Mvulana alijibu: “Upendo wangu ni upendo usiokufa.” Huyu mvulana hakuwa na upendo wa kweli. “Mambo mawili ambayo mtu hawezi kuficha: kwamba amelewa na kwamba yuko katika upendo,” alisema mwanasiasa Antiphanes.
Pale palipo na moto wa upendo, moto huo uchochewe, usipoe. Papa Francis katika kitabu chake ‘Furaha ya Upendo’ aliandika: “Ninakumbuka msemo wa zamani kwamba, maji yaliyotulia hayasongi mbele na hayafai kitu. Kama katika miaka ya kwanza ya ndoa hisia za upendo za wanandoa zinatulia, upendo hupoteza moto ambao unapaswa kuwa nguvu inayousukuma kwenda mbele.” Upendo ni nguvu. Upendo si nguvu tu katika ndoa hata katika mahusiano ya maadui. “Upendo ndiyo nguvu ya pekee inayoweza kumbadili adui akawa rafiki,” alisema Martin Luther King Jr.
Kuna kijana aliyehukumiwa kunyongwa. Alimchukia kila mtu, hata mama yake. Mama yake alikwenda kwa jaji na kumwomba amsamehe mtoto wake. Lakini jaji hakufanya lolote. Alisema: “Kwa nini unashughulika na kijana huyu? Hakuna unachoweza kufanya, hakupendi.” Mama alimwambia jaji: “Najua kuwa hanipendi, lakini nampenda.” Kupendwa ni mtihani.
Ukipendwa, pendeka. Ukibebwa bebeka. Ukiheshimiwa jiheshimu. Upendo uwe wa daima, unahitaji kutotegeana mitego, pawepo majadiliano kama zoezi la kupendana. Tanguliza furaha ya mwingine.