Ni kawaida kwa mwanamke aliyepevuka kupata hedhi ya kila mwezi katika mzunguko wake kutokana na mabadiliko ya homoni, ambapo mfuko wa uzazi unatengeneza ukuta mpya kwa ajili ya mapokezi ya utungishwaji wa mimba.

Kwa kipindi hicho mwanamke anapitia siku kadhaa za utokwaji wa damu kupitia uke. Idadi ya siku hizi imetofautiana kati ya mwanamke mmoja na mwingine, kulingana na mfumo wa  vichocheo wa kila mwanamke.

Wengi wamezoea kupata hedhi kwa kipindi cha siku tatu, nne na wengine hata siku tano. Lakini hedhi inayopitiliza zaidi ya kipindi hiki inaashiria tatizo la kiafya ambalo mwanamke hapaswi kulifumbia macho.

Ifahamike kuwa, hata mzunguko wa kawaida wa hedhi unachangia upungufu wa damu, hivyo katika hedhi iliyopitiliza mwanamke anapoteza kiasi kikubwa cha damu kwenye kila mzunguko kuliko kawaida, ikiambatana na maumivu yanayoweza kumfanya mwanamke ashindwe kuendelea na shughuli zake za kila siku.

Ni muhimu kumuona daktari haraka ikiwa mwanamke anapitia hali hiyo na kupatiwa tiba stahiki.

Pedi kujaa damu ndani ya muda mfupi, hivyo kulazimika kubadili pedi kila saa, na wengine hulazimika kuvaa pedi zaidi ya moja ili kukikabili kiasi kikubwa cha damu kinachotoka, ni dalili kuwa mwanamke hayupo kwenye hedhi ya kawaida.

Lakini pia dalili nyingine ni kama vile kupata hedhi zaidi ya wiki moja, damu inayotoka kuambatana na mabonge madogo madogo ambayo yamesababishwa na damu kuganda. Pia dalili za anemia kama vile uchovu uliopitiliza na matatizo katika upumuaji.

Mwanamke anashauriwa kumuona daktari kama anapitia dalili hizi au pia kama mwanamke anapata hedhi mara mbili kwa mzunguko mmoja.

Sababu zinazochangia hedhi kupitiliza ni nyingi, likiwamo tatizo la kiafya linaloathiri utendaji kazi wa mayai ya uzazi. Japo kwa lugha ya Kiswahili halijapatiwa jina sahihi, lakini kwa Kiingereza linajulikana kama polycystic ovary syndrome (PCOS).

Tatizo hili linasababisha kuyumba kwa mzunguko wa hedhi kati ya mwezi mmoja na mwingine, na hedhi inapokuja inakuwa ni ya muda mrefu kuliko kawaida.

Lakini pia maambukizi kwenye mfumo wa uzazi wa mwanamke, mathalani kwenye mfuko wa uzazi, kwenye mirija ya uzazi na hata maambukizi kwenye mayai ya uzazi, nayo yanasababisha hedhi kupita kiasi. Hedhi iliyopitiliza pia inaweza kusababishwa na uvimbe kwenye mfuko wa uzazi.

Uvimbe huo hauashirii saratani, lakini ukiwa mkubwa unasababisha hedhi iliyozidi kawaida. Baadhi ya njia zinazotumika kwenye uzazi wa mpango pia zinachangia kwa kiasi kikubwa hedhi kupitiliza.

Baadhi ya njia hizi si rafiki kwa afya ya mwanamke na pamoja na utendaji kazi wake, zinakwenda kuvuruga mfumo wa uzazi wa mwanamke; mathalani vipandikizi vinavyowekwa kwenye mfuko wa uzazi ili kuzuia utungishwaji wa mimba.

Kipandikizi hiki kinasababisha hedhi iliyopitiliza kwa mwanamke kwa kipindi cha miezi mitatu hadi miezi sita tangu kuwekwa. Saratani ya mfuko wa uzazi pia inachangia hedhi iliyopitiliza.

Pia, matatizo yanayotokea wakati wa ujauzito yanachangia tatizo hilo, mathalani kuharibika kwa mimba na mimba kutungwa nje ya mfuko wa uzazi.

Mimba inapoharibika mwanamke hutokwa damu kwa kiasi kikubwa katika mzunguko wake wa hedhi, na hali hii inaweza kudumu kwa muda wa miezi kadhaa hadi hedhi kurudi katika hali ya kawaida.

Pia mimba inapotungwa nje ya mfuko wa uzazi, inasababisha maumivu makali na kutokwa damu kusiko kawaida. Baadhi ya magonjwa ya damu ya kurithi yanahusishwa kuwa chanzo cha tatizo hili.

Lakini pia kuna baadhi ya dawa ambazo mara nyingi hutumika kutuliza maumivu madogo madogo mwilini na hasa kupunguza maumivu ya majeraha yanayotoa damu.

Baadhi ya dawa hizo ni kama vile acetaminophen, ibuprofen na aspirin. Matumizi ya dawa hizo kwa muda mrefu yanasababisha hedhi iliyopita kiasi kutokana na utendaji kazi wake.

Magonjwa ya figo ni tatizo la kiafya linalochangia hedhi kupitiliza. Aidha, ifahamike kuwa, hedhi iliyopitiliza, kwa kiasi kikubwa inatokana na mabadiliko ya homoni mwilini ambapo yai la uzazi linapasuka endapo halijafanya urutubishwaji ndani ya muda husika.

Wakati wa mabadiliko hayo ya homoni, watu ambao wapo hatarini zaidi kupata tatizo la hedhi iliyopitiliza ni wanawake wenye umri mkubwa, ambao wanakaribia kukosa uwezo wa kuzaa.

Kwa kawaida wanawake wenye umri wa kuanzia miaka 60 wanapoteza uwezo wa kushika mimba na kwa wakati huo, mabadiliko makubwa ya mfumo wa homoni yanatokea katika miili yao.

Kupata hedhi kulikopitiliza kunaambatana na matatizo mengi ya kiafya yakiwamo ugonjwa wa anemia inayosababisha upunguvu wa madini ya chuma mwilini.

Ulaji wa vyakula vyenye ukosefu wa madini ya chuma ndicho chanzo kikuu cha anemia, lakini hedhi iliyopitiliza inasababisha kwa kiasi kikubwa anemia. Mgonjwa anapitia dalili chache kama vile uchovu, na ngozi kupauka na kubadilika rangi.