Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inapenda kufahamisha Umma kwamba, Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imeondoa hitajio la Visa kwa raia wa Tanzania wanaoingia DRC kuanzia tarehe 20, Machi, 2025.

Baada ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) mwezi Julai 2022, tarehe 2 Septemba 2023, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliondoa utaratibu wa malipo ya visa kwa raia wa DRC kwa matarajio ya nchi ya DRC pia kufuta utaratibu wa kutoza malipo ya visa kwa msingi wa kuungana mkono (reciprocity).

Serikali ya Jamhuri ya Tanzania inaamini kuwa uamuzi huu wa Serikali ya DRC ni hatua nzuri katika kuimarisha mtangamano na utakuwa na manufaa, ikizingatiwa kuna mwingiliano mkubwa wa wananchi wa nchi hizi mbili katika masuala mbalimbali ya kijamii na kibiashara. Vilevile, kuondolewa kwa hitajio la Visa kutachochea ukuaji wa uwekezaji, biashara na kupunguza gharama.

Hatua hii ni moja ya mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na  Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia na ujirani mwema kwa vitendo, na ni ishara ya Tanzania kuzingatia miongozo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, pamoja na Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA).