Mkutano wa Rais John Magufuli na wafanyabiashara ni miongoni mwa uamuzi wa busara uliosaidia kurejesha imani ya kundi hilo kwa serikali.
Kulishatanda hofu kwamba wafanyabiashara ni kama vile watu wasiotakiwa, jambo ambalo si rahisi kutokea katika serikali yoyote makini.
Nchi inahitaji fedha ili iweze kujiendesha. Kuna miradi mingi na mikubwa mno ambayo yote inahitaji fedha kuitekeleza. Fedha za kutekeleza kazi hiyo zinatoka kwenye makundi yote ya uzalishaji – wafanyabiashara wakiwa na mchango mkubwa.
Tumeona matokeo kwenye mkutano wa rais na wafanyabiashara wa kada mbalimbali, pia wafanyabiashara wa madini. Kote huko kumeanza kuonekana matokeo yenye kuleta tija. Nyoyo za wafanyabiashara na wawekezaji zimeanza kutulia.
Hata hivyo, bado kuna matatizo makubwa kwenye kada nyingine. Matumaini ya wengi ni kumuona rais akiendelea kukutana na kada kama vile wakulima na kadhalika.
Nimeona jambo moja niliseme kabla mambo hayajaenda mrama. Kada ya kilimo, hasa upande wa kampuni za uzalishaji na usambazaji wa mbegu nchini inaelekea shimoni. Sidhani kama Waziri wa Kilimo ambaye hana muda mrefu katika kiti hicho anajua kinachoendelea Arusha na Moshi.
Nimezuru baadhi ya kampuni za uzalishaji wa mbegu na kujionea hali mbaya inayowakabili wawekezaji kwenye nyanja hii.
Leo naomba nitoe mfano mmoja wa Kampuni ya Balton Tanzania Limited. Kampuni hii ipo hapa nchini tangu mwanzoni mwa miaka ya 1960. Inajihusisha na utafiti wa mbegu, kilimo cha umwagiliaji na utengenezaji wa viuatilifu. Imetoa mchango mkubwa kwenye uchumi wa taifa letu. Imekuwa msaada mkubwa kwa wakulima. Imekuwa ikifanya utafiti wa mbegu za mazao mbalimbali.
Kuna habari mbaya kwamba Balton Tanzania Limited wanafunga kazi zao hapa nchini. Wameshafungasha virango. Wanapiga mnada mali zao, yakiwamo maghala. Wanaiacha Tanzania waliyoitumikia kwa miaka takriban 60. Hii si habari nzuri.
Wanaondoka nchini, lakini hawaendi mbali. Wamehamishia shughuli zao zote Nairobi, Kenya. Wanasema kama kuna sababu ya kuendelea kuwahudumia Watanzania, basi uungwana huo wataufanya wakitokea katika ofisi zao za Nairobi.
Hili si jambo dogo la kufumbia macho. Ni habari mbaya kwa wakulima na wanufaika wote wa sekta ya kilimo nchini.
Nini kinawaondoa nchini? Siyo siri kwamba kinachowaondoa nchini ni ubabe wa baadhi ya wanasiasa wenye mihemko wanaoamini kuwa kuongoza ni kunyanyasa.
Masuala ya mbegu ni ya kisayansi ndiyo maana kabla ya zao fulani kupandwa mahali fulani kitu kinachofanywa awali kabisa ni kupima udongo na hali ya hewa ya sehemu husika. Inaelezwa kuwa wakulima fulani walinunua mbegu za Balton na kwenda kusiha. Zile mbegu, ama hazikuota, au ziliota kwa shida shida. Wakulima wakalalamika. Mwanasiasa mmoja kijana akaibuka na kutoa amri ya kukamatwa kwa viongozi wa Balton. Hakutaka kuuliza na kupewa sababu za kisayansi za kwanini mbegu zimegoma kuota.
Wanasema wazi kuwa wanaondoka kwa sababu ya bughudha, kudhalilishwa na kuwekwa mahabusu bila sababu za msingi. Wanapinga kuonewa na kudhalilishwa. Wanaona mazingira ya kuendelea kufanya shughuli zao hapa nchini si rafiki. Mali zao zilizoko Kisongo na Dar es Salaam wanaziuza. Wanaondoka.
Kina Balton wanaokumbwa na hali hiyo ni wengi nchini kote. Hali kama hii iko Moshi na maeneo yote ambako wadau wa mbegu na viuatilifu wanaendesha shughuli zao. Ubabe ulioelezwa na Rais Magufuli kwa upande wa TRA hauko huko pekee, bali umeenea kwa kada zote, hasa kwa wanasiasa.
Mazingira ya aina hii hayana mbolea kwa uchumi wa taifa letu. Ni kweli kwamba umekuwapo ujanja ujanja mwingi kwenye maeneo mengi ya uzalishaji na biashara.
Lakini hiyo haimaanishi kuwa maeneo yote ‘yameoza’ au yanahitaji nguvu za kipolisi kukabiliana na ubovu uliopo. Udhaifu mwingine unaoonekana katika maeneo mengi ni matokeo ya mfumo wetu mbovu tuliokuwa nao. Mamlaka hazikutekeleza wajibu wao.
Tunapaswa kufungua ukurasa mpya wa mazungumzo na maridhiano badala ya ubabe na maguvu. Tunapaswa kuwa na viongozi wakweli wanaoripoti taarifa zilizo za kweli kwa wakubwa wao. Viongozi wakuu wanapopewa taarifa za upotoshaji ni hatari kubwa kwa wanaosingiziwa.
Kwa hili la kampuni zilizo katika sekta ya kilimo hatuna budi kulitazama kwa jicho la hadhari, maana kilimo ndiyo uhai wa Watanzania walio wengi. Tukianza kuwavuruga wadau hawa tutakuwa tunawakwamisha maelfu kwa maelfu ya Watanzania wanaotegemea kilimo kama njia ya kuyamudu maisha yao.