Sensa ya idadi ya watu na makazi inafanyika kuanzia Jumapili wiki hii hadi Septemba 2, huku baadhi ya Watanzania wakiendelea kuipinga hadi dodoso la dini litakapojumuishwa. Viongozi mbalimbali wa Serikali hususan Wakuu wa Mikoa na Wilaya wamekuwa wakiwaomba viongozi wa kisiasa na kidini kuwataka waumini wao washiriki kikamilifu kuhesabiwa kwa sababu ni faida yao wenyewe na taifa letu.
Wakati viongozi hao wakifanya jitihada kubwa za kuinusuru sensa hiyo inayofanyika mara moja tu kila baada ya miaka 10, hii ikiwa ni ya tano tangu Uhuru uliopatikana Desemba 9, 1961, baadhi ya wafuasi wa dini ya Kiislamu wameendelea kuwahamasisha waumini wenzao waisusie kama dodoso hilo la dini halitawekwa.
Tayari kazi hiyo imeripotiwa kufanyika katika mikoa ya Singida, Kilimanjaro, Kaskazini Pemba, Mjini Magharibi na kadhalika na kuna sehemu nyingine vimesambazwa hadi vipeperushi vya kuwataka Waislamu nchini wakatae kuhesabiwa.
Nakumbuka mtu wa kwanza kuwataka hadharani Waislamu wasishiriki sensa hiyo ni Amiri Mkuu wa Jumuiya ya Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Mussa Kundecha, siku chache baada ya Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa, kuwasilisha hotuba ya bajeti ya Serikali ya mwaka 2012/2013 mjini Dodoma Juni 14, mwaka huu.
Kundecha alikerwa na kauli ya Serikali kwamba hadi wakati huo, maandalizi ya sensa yalikuwa yanakwenda vizuri na utekelezaji wake uligharimu Sh. bilioni 23.6 ikiwa ni asilimia 95. Uzinduzi wa uhamasishaji kwa wananchi, umefanyika Ijumaa iliyopita kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja Dar es Salaam na mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu, Mizengo Kayanza Pinda.
“Tunasikitika (kusema) kuwa hatutashiriki sensa hadi mapendekezo yetu yatakapofanyiwa kazi. Tunataka idadi halisi ya Waislamu ili nasi tujue tunawasaidiaje kimaendeleo na kidini,” alisema Sheikh Kundecha alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini.
Kiongozi wa pili mwandamizi wa Kiislamu kupinga jambo hilo alikuwa Katibu Mkuu wa Taasisi hiyo, Sheikh Ponda Issa Ponda, hapo Juni 21 mwaka huu aliposisitiza kuwa msimamo wa kutoshiriki sensa hiyo uko palepale. Yeye alikwenda mbali zaidi kwa kusema Serikali inawahujumu Waislamu kwa kutoa takwimu za uongo kuhusu idadi yao, ili waonekane wachache lakini hakuainisha jambo hilo linafanyika namna gani au kwa njia zipi.
Sitaki watu wakimbilie imani yangu kwamba ninapinga matakwa haya kwa sababu ni Mkristo, hoja ambayo hata ikijengewa maneno matamu namna gani, itabaki kuwa haina msingi wala maana yoyote. Mwaka 2001 aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambaye sasa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, aliwakemea Waislamu wenzake kwa tabia yao ya kuingilia imani za kiroho za watu wengine.
Katika kufanya hivyo, Kikwete aliwanyooshea kidole Waislamu walioandamana jijini Dar es Salaam, kupinga adhabu ya kufungwa jela mwaka mmoja kwa Khamis Dibagula, ile ambayo alipewa baada ya kutiwa hatiani kwa kwenda kwenye mkutano wa Injili mjini Morogoro na kupiga kelele akisema “Yesu si Mungu”.
Kikwete ni Mwislamu kwa asilimia 100 kuanzia yeye mwenyewe, ukoo wake na hata familia yake, lakini hakubaliani na kuingiza imani binafsi za kidini mahali pasipotakiwa. Ndiyo maana tangu awakemee miaka 11 iliyopita, hakuna Mwislamu yeyote wakiwamo masheikh, maimamu na wanazuoni wengine – aliyewahi kumjibu chochote wala popote, hivyo naamini wameshindwa kwa sababu tu alizungumza ukweli ambao hata iweje hauwezi kugeuzwa vinginevyo.
Nashukuru kwamba baadhi ya viongozi wengine wa Kiislamu nchini akiwamo Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Issa bin Shaaban Simba, wamewataka Waislamu wasiihusishe sensa na mambo ya dini. Katika hali hiyo, juhudi zote zinazofanywa na baadhi ya Waislamu za kuwaunga mkono Kundecha na Ponda haliingii akilini.
Suala la kutaka kujua idadi ya wafuasi wa dini au imani yoyote haiwezi kusubiri sensa ya Serikali. Hiyo ina sehemu zake ambazo zipo siku zote, hivyo inaweza kupatikana wakati wowote na mahali popote. Mathalani, haiwezekani Wizara ya Elimu isubiri sensa ili kufahamu idadi ya wahadhiri vyuoni, walimu na wanafunzi wa shule na taasisi mbalimbali za umma na binafsi na bila kuwepo haiwezi kujua.
Nakubali dhamira njema ya Sheikh Kundecha na wenzake ya kutaka kufahamu idadi ya Waislamu nchini, ili waweze kuwasaidiwa kimaendeleo na kidini, lakini sikubaliani na mpango wowote wa kutaka wawatambue kwa kutumia sensa ya Serikali ya watu na makazi na si kwa njia nyinginezo.
Wakati wapagani, kwa mfano, wanaweza kutambuana kwa kupitia ibada zao kwenye mapango, baharini, ziwani, mitoni, chini ya miti pamoja na sehemu nyingine zinazotumika kufanyia matambiko yao ya kuomba mizimu wakitoa hadi makafara ya wanyama, mazao ya kilimo na kadhalika, watu wenye imani nyingine nao hutambuliwa kwa namna zao.
Hao ni pamoja na Wakristo wanaotambuana kimadhehebu kwa jinsi wanavyosali au Waislamu wanavyoswali na mavazi yao; Wahindu kwa alama walizonazo na kwenda kwao mahekaluni, katika masinagogi na sehemu nyingine. Wapo pia Masingasinga, Wabaha’i na wafuasi wa madhehebu kama Baps Swaminarayani, Shri Swaminarayani na kadhalika.
Katika hali hiyo, wote wanaotaka kujua idadi ya waumini wao nchini watawapata katika sehemu za ibada zao. Haiwezekani washinikize kupata takwimu hizo kupitia sensa ya watu na makazi kwa sababu haihusiki na dini yoyote. Natambua, kwa mfano, kwamba waumini wa madhehebu ya Kikristo yakiwamo ya Kilutheri, Katoliki, Wasabato, Waanglikana, Wapentekoste na mengineyo hutambuana makanisani mwao na si kupitia shughuli yoyote ya serikali wala taasisi nyingine.
Ndiyo maana utakuta kila kanisa lina utaratibu maalum wa kuwatambua ili kujua idadi yao, kazi inayofanywa ili kuweka vizuri mipango yake ikiwamo ya upanuzi wa makanisa, viti vya kukalia pamoja na mahitaji mengine, na pia yanafanya hivyo ili kuwasaidia waumini wake katika masuala ya dini na maendeleo ya kidunia.
Huko utakuta wameunda jumuiya, kwaya za Injili au vikundi vingine vyenye majina yake kama Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) kuanzia kwenye vigango vyao, mitaa yao, sharika zao, parokia zao, majimbo yao, dayosisi zao na sehemu nyingine.
Aidha, waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), kwa mfano, kila mmoja ana kadi yake ya ahadi anayojaza mwenyewe kila mwaka ili pamoja na mambo mengine, kumtambulisha rasmi usharikani kwake, na pili huandikishwa kwenye kitabu kinachotunzwa ofisini kwa Mwinjilisti wa Mtaa au Mchungaji wa Usharika wake.
Pamoja na mfumo huo wa uhakika, kila ibada inayofanyika waumini wake huhesabiwa na kumbukumbu zao hutunzwa kwa kuonyesha idadi halisi ya wanaume, wanawake na watoto. Hiyo inawezesha kufahamu kila wiki, kila mwezi na kila mwaka kwamba wangapi waliosali, hali inayofanikisha kujua kama mtaa husika, usharika, jimbo, dayosisi au kanisa nchi nzima linaongeza idadi ya waumini ama linarudi nyuma.
Katika hali hiyo, hakuna mashaka kwamba haina tija kuendelea kung’ang’ania watu waisusie sensa inayofanyika Jumapili wiki hii. Sensa hii ni kwa ajili ya maendeleo yetu kama Watanzania na haina uhusiano wowote wa kuridhisha nafsi zetu kiimani.
Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa Simu Na. 0659 220 220 na 0762 633 244