Na Mwamvua Mwinyi,JamhuriMedia,Pwani
Mkuu wa mkoa wa Pwani ,alhaj Abubakari Kunenge,ameeleza mkoa hauridhiki na hali ya usafiri wilayani Mafia, kwani wananchi wa wilaya hiyo bado wanachangamoto kubwa ya kupata kivuko kitakachojibu kero ya usafiri waliyonayo.
Aidha wilaya hiyo,inakabiliwa na changamoto ya muda mrefu ya ushuru wa bidhaa kwenye bandari ndogo ya Nyamisati na Mafia ,unaowatesa wananchi na wafanyabiashara wa pande hizo.
Akizungumza katika kikao cha bodi ya barabara, cha mkoa , Kunenge alieleza muda mwingi wananchi wanakosa usafiri na vivuko Kuwa kwenye matengenezo na kusababisha abiria kukwama.
Alimweleza Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) ,kuwasiliana na Wakala wa ufundi na umeme (TEMESA) ,ili kueleza mpango wao wa kivuko kinachotengenezwa ,gharama zake halisi na uwezo wa kivuko ,kisha washirikishwe wananchi na viongozi wa wilaya pasipo kuweka usiri.
Ameeleza ,wakati wanaufungua mkoa kwa miundombinu mbalimbali ya barabara,reli, kuna haja ya kupata ufumbuzi wa muda mrefu kutatua changamoto ya usafiri hasa wa njia ya maji.
Hata hivyo Kunenge,aliwataka Mamlaka ya Bandari Tanzania ( TPA )kuja mpango wao na waweze kuzungumza na mkoa .
“Tunafahamu Serikali inafanya jitihada kubwa ya kutatua changamoto ya usafiri Mafia ,Lakini Serikali ya mkoa hatujaridhika na utatuzi wa kero hii,
“Haiwezekani TEMESA Leo mnakuja na mpango wenu, na kusema kivuko mnakuja kukileta Cha zaidi ya Bilioni 9 wakati hamjashirikisha mkoa,wilaya Wala wananchi “
Niwaombe TEMESA msifanye usiri katika hili , wananchi wanapaswa kushirikishwa ili nao watoe maoni Yao kujua endapo kivuko hicho kitawafaa” amesema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mafia Juma Salum alieleza ,kilio cha usafiri wa uhakika ni mtihani mkubwa kwa wana Mafia.
Ameeleza,sasa ni siku ya tatu wasafiri wa Mafia wamekwama Nyamisati kutokana na kukwama kwa usafiri.
Salum alifafanua licha ya hilo,pia ni takriban miezi mitano sasa kivuko cha MV Kilindoni kinadaiwa kuwa katika matengenezo suala ambalo linakatisha tamaa katika maendeleo ya Mafia.
“Kivuko hiki hakijibu tatizo la usafiri Mafia, tunatakiwa kupata uhakika wa usafiri wa kuingia Nyamisati na Kutoka Mafia,kuwe na mpango wa muda mrefu,kwa shida hizo kunasababisha wananchi kuhitaji huduma ya kivuko cha binafsi kilichokuwepo zamani ili kiwasaidie “alisema Juma Salum.
Awali Meneja wakala wa ufundi na umeme, TEMESA Mkoa , Mhandisi Rehana Juma ameeleza ,vivuko vya Mv Kilindoni inafanyiwa marekebisho ya kimatengenezo kwa gharama ya zaidi ya milioni 294 ,ipo katika hatua ya mwisho ya matengenezo na Sasa imefikia asilimia 85 ,tayari kwa majaribio ili iingie majini kuanza safari zake.
Kutokana na matengenezo ya mara kwa mara ya vivuko vilivyopo,Wizara husika na TAMESA imeamua kuanza mchakato wa kununua kivuko kipya ili kupunguza adha ya ongezeko la wasafiri wa pande zote mbili Nyamisati na Mafia itakayokuwa na uwezo wa kubeba Tani 120 na watu 500,chenye gharama zaidi ya Bilioni 9.