Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani

Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Alhaji Nuhu Mruma, amehimiza ktika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadan ni muhimu kwa Watanzania kuendelea kushikamana, kuwa wamoja, na kujali yatima, hasa wale walio na mahitaji maalum.

Amesema hayo wakati aliposhiriki iftar iliyoandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, ikiwa ni sehemu ya kusherehekea mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Alieleza iftar hiyo imewaleta pamoja watu mbalimbali, wakiwemo watoto yatima kutoka vituo mbalimbali vya kulelea watoto.

Alhaj Mruma, ambaye alikuwapo kama mwakilishi wa Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zuber, alisema kuwa kilichofanyika katika Mkoa wa Pwani ni muendelezo wa kile alichofanya Mheshimiwa Rais katika tukio la Machi 4, Ikulu, akieleza kuwa juhudi hizi ni za kupongezwa na kuigwa.

“Katika kipindi hiki cha Ramadhani, ni muhimu kwa Watanzania kuendelea kuungana na makundi maalum ikiwemo watoto yatima kutoka vituo vya kulelea watoto”

“Tumetoka mbali, lakini bado tunahitaji kuhakikisha kuwa tunawahudumia na kuwa na upendo wa dhati kwao,” alisema Alhaji Mruma huku akisisitiza umuhimu wa kufanya ibada kwa utulivu na amani.

Alhaji Mruma alipongeza viongozi wa BAKWATA Mkoa wa Pwani kwa kuungana na kusaidia makundi yanayostahiki, akisema kuwa juhudi zao ni za kipekee na zinahitajika zaidi katika jamii yetu.

Aliongeza , BAKWATA inaendelea kukemea mmomonyoko wa maadili ili kujenga jamii yenye uadilifu na inayokataa rushwa na maasi.

Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Hamis Mtupa, aliunga mkono hatua ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani na kusema kuwa ni jambo la kuigwa.

Alisema kuwa aina hii ya iftar ni ya kipekee kwa sababu imegusa wahitaji hasa watoto yatima, na kuwa ni mfano mzuri kwa wengine wanaolenga kufuturisha.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, aliwahakikishia wageni na wakazi wa Mkoa wa Pwani kuwa futari hiyo iliyotayarishwa na Rais ilikuwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha kuwa watu mbalimbali, wakiwemo watoto yatima, wanapata fursa ya kushiriki katika sherehe za Ramadhani.

Hafla hiyo iliambatana na dua maalum kwa ajili ya kumuombea Rais Samia Suluhu Hassan.