Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Bagamoyo
WAKALA wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mkoani Pwani unaendelea kutekeleza miradi ya maji 35, ambayo ikikamilika itanufaisha wakazi 180,000.
Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama kutoka asilimia 80.3 ya sasa hadi kufikia asilimia 88 ifikapo Desemba 2025.
Hii ni sehemu ya juhudi za kufanikisha utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), inayolenga kuhakikisha upatikanaji wa maji vijijini unafikia asilimia 85 na mijini asilimia 95.
Hayo yalibainika wakati Naibu Waziri wa Maji, Kundo Mathew, alipokuwa akikagua miradi ya maji wilayani Bagamoyo, ikiwemo kisima cha Kitongoji cha Diagala, kijiji cha Diozile, katika ziara yake mkoani Pwani.
Kundo alisema upatikanaji wa maji mjini na vijijini mkoani Pwani umefikia asilimia 86, ukilinganisha na asilimia 59 mwaka 2021,ikiwa ni ongezeko la asilimia 20 ndani ya miaka minne.
“Tunaupongeza mkoa wa Pwani kwa kusimamia miradi ya maji kwa ufanisi. Fedha nyingi zinatumika kutekeleza miradi hii, na tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea na ajenda ya kumtua ndoo mama kichwani,” alisema Kundo.
Aliongeza kuwa kisima cha Diozile kina uwezo wa kuzalisha lita 2,500 kwa saa, sawa na lita 25,000 kwa masaa kumi, na lita 50,000 kwa siku nzima, kinatarajiwa kunufaisha wakazi zaidi ya 3,000 wa eneo hilo.
Kundo alitoa wito kwa wananchi kutunza na kulinda miundombinu ya maji na kuendelea kumuunga mkono Rais Samia katika juhudi za kusogeza huduma ya maji safi na salama kwa wananchi.
Kwa mujibu wa Meneja wa RUWASA mkoa wa Pwani, Beatrice Kasimbazi, kisima hicho chenye urefu wa mita 35 kimegharimu shilingi milioni 60 na kitaleta suluhisho kwa wakazi 3,117 waliokuwa wakitumia maji yasiyo salama.
“Kuna visima 35 na vyanzo mbadala ikiwa ni pamoja na bwawa na bomba kuu la DAWASA katika maeneo matano ya Bagamoyo ikiwa ni sehemu ya mpango mkubwa wa visima 900 vya Mama Samia unaotekelezwa nchi nzima,” alieleza Beatrice.
Aliongeza kuwa RUWASA tayari imepokea shilingi bilioni 2.4 kwa ajili ya miradi hiyo, na katika ujenzi wa visima hivyo umefikia asilimia 72.5, ambapo visima 29 tayari vinatoa huduma na visima 11 vipo katika hatua mbalimbali za ujenzi.
Kadhalika Beatrice alieleza, upatikanaji wa maji ni karibia asilimia 90 Mjini ambayo inahudumiwa na DAWASA na mamlaka za Utete na Kilindoni huku kwa upande wa Vijijini upatikanaji umefikia asilimia 80.3.
Mkazi wa Diozile Daniel Kuduru, alitoa shukrani kwa serikali kwa kusogeza huduma ya maji.
Kuduru alisema kuwa awali walilazimika kutembea kilomita 14 kwenda na kurudi kufuata maji kwenye malambo, maji ambayo hayakuwa salama kwa afya.