Awali ya yote nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema na wingi wa neema, lakini pia kutupatia uwezo na nguvu kusimamia na kutumia rasilimali zilizopo kwa faida ya kizazi hiki na kijacho.

Tanzania imejaliwa kupata rasilimali na vivutio vya kipekee duniani. Kidunia ukitaja hifadhi za Mlima Kilimanjaro, Serengeti, Ngorongoro au visiwa vya Zanzibar itafahamika unamaanisha Tanzania.

Tanzania imejaliwa misitu ya asili yenye thamani kubwa duniani mfano, Hifadhi ya Misitu Asilia (Nature Forest Reserve) zaidi ya 12, hasa kwenye Milima ya Tao la Mashariki (Eastern Arc Mountains). Misitu hiyo ni muhimu kuhifadhi makazi ya bioanuwai na vyanzo vya mito mikubwa nchini (i.e. Kagera, Kilombero, Kihansi, Mara, Pangani, Wami, Ruaha, Ruvu, Ruvuma, Zigi na kadhalika). Vilevile, taifa letu limebahatika kuwa na madini aina mbalimbali na vito vya thamani (germ stones).

Isitoshe, kuna rasilimali samaki za kutosha kwenye maji baridi na maji chumvi bila kusahau ardhi ya kutosha na rasilimali watu zaidi ya milioni 50. Haya yote ni hazina kubwa katika Tanzania. Je, rasilimali hizi tunazitumia vipi kujiletea maendeleo sisi na vizazi vitakavyofuata?

Julai 31 na Agosti 1, 2019 Taasisi ya Uongozi kupitia Jukwaa la Maendeleo Endelevu (Green Growth Platform) liliandaa kongamano jijini Dodoma lililohusu utunzaji na usimamizi imara wa misitu kwa upatikanaji endelevu wa maji kwa matumizi ya nyumbani na shughuli za kiuchumi.

Mada nne zilitolewa zikifuatiwa na majadiliano kupitia jopo la wataalamu watano waliobobea katika masuala ya rasilimali misitu na maji. Baadaye kukawapo mjadala, maoni, majumuisho na kisha kutembelea Msitu Chenene na chanzo cha maji Mzakwe.

Wadau walijifunza uhusiano kati ya Msitu Chenene na Mzakwe na kushauri nini kifanyike ili kuhakikisha upatikanaji wa maji katika Jiji la Dodoma unakuwa endelevu.

Kongamano lilifunguliwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, na kuhudhuriwa na Waziri wa Nchi – Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), George Mkuchika; Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano, George Simbachawene na Dk. Benilith Mahenge ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.

Asilimia 88 ya waliokusudiwa kuhudhuria walifika. Walengwa walikuwa ni maofisa waandamizi kutoka sekta za umma na binafsi – wakiwamo viongozi wa taasisi na mashirika, wakuu wa mikoa ya Katavi, Mbeya na Ruvuma na wakuu wa wilaya za Bahi, Kilolo, Mufindi, Namtumbo na Rufiji. Kabla ya ufunguzi, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Profesa Joseph Semboja, alitoa maelezo ya utangulizi na kumshukuru Makamu wa Rais kwa kukubali kuwa Mlezi wa Jukwaa la Maendeleo Endelevu.

Kimsingi kongamano lilikuwa la mafanikio ya kutosha kutokana na majadiliano ya kina na matokeo ya kutembelea Msitu Chenene na rasilimali maji Mzakwe. Baadhi ya waliostahili kuhudhuria hawakufanya hivyo kutokana na kukabiliwa na majukumu mengine au kushiriki kwenye kongamano/semina nyingine.

Kwa miaka mingi imekuwapo hali ya sekta/taasisi kupanga na kutekeleza shughuli zake bila kushirikisha wadau ipasavyo. Tunajifungia ofisini na kukosa kujua nini matokeo kwa sekta nyingine kutokana na shughuli tunazozifanya hasa kwa taasisi au sekta zinazotegemea matumizi ya rasilimali ardhi na vilivyopo juu/chini yake (inadequate cross-sectoral linkages).

Mfano, sekta kama kilimo, mifugo, maji, misitu, wanyamapori, uvuvi, umwagiliaji, madini, miundombinu, viwanda, nishati, vijiji na ardhi. Kutokana na kutokuwapo uratibu madhubuti kuhusu shughuli za kila sekta/taasisi, matokeo ya utendaji na/au utekelezaji wa kazi za kila siku kisekta/taasisi; yamekuwa na changamoto kadhaa kutokana na kutoratibiwa shughuli za kisekta/taasisi ipasavyo.

Uzoefu unaonyesha kuwa kufanya kazi kisekta/taasisi bila kuhusisha wadau kikamilifu tumekuwa tukitumia fedha/muda kutekeleza shughuli zinazoshabihiana (duplication of efforts), lakini bila kukusudia tunajikuta tunasababisha madhara kwa sekta nyingine.

Mathalani, kupoteza misitu kutokana na kilimo cha kuhamahama (shifting cultivation); kuchunga mifugo kiholela maeneo yaliyohifadhiwa kisheria; kufyeka na kuchoma misitu na masuala ya nishati ya kupikia kusababisha misitu kuharibika kutokana na matumizi makubwa ya mkaa na kadhalika.

Kila sekta/taasisi kufanya kivyake (operating in silos/boxes) mfano, misitu, nishati, kilimo na mifugo na nyinginezo, ni matokeo ya kutokuwapo chombo madhubuti cha KURATIBU shughuli za kisekta ili kuondoa changamoto katika matumizi ya rasilimali zetu kwa faida ya wote.

Misitu inatoweka kwa kasi kubwa kutokana na shughuli za sekta nyingine na kwa miaka mingi kumekuwapo ushirikishwaji hafifu wakati wa kutunga sera au kutayarisha mikakati ya kutekeleza shughuli za kisekta/taasisi, hivyo kukosa nguvu ya kupata matokeo chanya.

Huenda rasilimali maji zinaathirika kwa njia hiyo hiyo. Serikali kupitia Sera ya Uchumi wa Viwanda imefanya sahihi kuweka kituo kimoja cha kuratibu shughuli za wawekezaji wa ndani na kutoka nje (Tanzania Investment Centre – TIC).

Sasa taifa linahitaji kituo kama hicho kuratibu shughuli za kisekta/kitaasisi kwa masuala ya makongamano, semina na mikutano inayohitaji ushiriki wa wadau ili kuondoa mkanganyiko kwa shughuli zinazofanana kutekelezwa wakati mmoja wakati wadau ni wale wale. Ni kama kugombania watakaoshiriki.

Kukiwapo chombo cha kuratibu shughuli hizo itakuwa rahisi kupunguza gharama na kupata matokeo chanya na kuongezeka ushirikiano kati ya sekta/taasisi hasa zenye shughuli za kutumia rasilimali asilia. Ili tufanye vizuri zaidi tunahitaji uratibu sahihi na chombo hicho kitahakikisha tunafanikiwa vizuri.

Nimwombe Rais Magufuli, kwa manufaa yetu sote, aridhie kuanzishwe chombo cha kitaifa kuratibu shughuli za serikali hasa zinazoshabihiana kiutendaji. Ninachomaanisha ni chombo au mamlaka kwa nia ya kuondokana na mazoea ya kufanya kazi kisekta/kitaasisi na kutotumia vizuri muda, rasilimali fedha na watu.

Faida ni kuhakikisha mipango ya sekta/taasisi husika hasa inayohusu masuala kama kongamano, semina au mikutano ya kuandaa/kuboresha sera/mikakati ya kufanikisha maendeleo endelevu inaratibiwa ipasavyo (effective co-ordination).

Chombo au mamlaka itapitia na kuangalia ni shughuli zipi zinashabihiana na kuelekeza wahusika wakae na kutayarisha utekelezaji wa pamoja (cross-sectoral linkages). Kwa kufanya hivyo tutaepuka kufanya yanayofanana kwa wakati mmoja na kuokoa fedha na muda.

Si hivyo tu, bali pia kuimarisha ufanisi na kuongeza tija kwa shughuli za serikali na kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi/sekta mbalimbali kwa faida ya taifa letu.

Mwandishi wa makala hii, Dk. Felician Kilahama, ni Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki mstaafu katika Wizara ya Maliasili na Utalii.