Na Joe Beda Rupia
Mungu aliumba kusahau. Ndiyo. Kusahau ni jambo zuri sana. Tusingekuwa tunasahau, dunia ingejaa visasi. Wakati ukipita, watu husahau na maisha yanaendelea.
Tanzania katika miaka yake 60 ya uhuru, imekuwa na mawaziri wa Mambo ya Ndani wengi tu. Huenda ni wengi kuliko wa wizara nyingine.
Mambo ya Ndani ya Nchi. Wizara nyeti hii. Augustine Mrema aliikamata na kuiendesha kwa mbwembwe na umahiri mkubwa miaka ya 1990 mwanzoni.
Aliikamata kwelikweli na kuitikisa nchi. Aliujua unyeti wa wizara hii. Akaanzisha ulinzi wa sungusungu kama njia mojawapo ya kukabiliana na ujambazi uliokuwa umeshamiri wakati ule.
Alifanikiwa kwa kweli, lakini kwa bahati mbaya ‘wakubwa’ wenzake wakamwona ana kiherehere. Akaambiwa anavuka mipaka.
Wanamuziki mashuhuri wakati ule, Dk. Remmy Ongola na Cosmas Tobias Chidumule wakahoji; ‘ni mipaka gani hiyo ndani ya nchi?’ hawakujibiwa.
Naam! Waziri wa kawaida tu anatungiwa muziki? Hili si jambo la kawaida. Naamini hakujawahi kutokea Waziri wa Mambo ya Ndani mahiri kama Mrema kwa miaka hii 60 ya uhuru. Kama ni upungufu, basi ni wa kibinadamu tu.
Wakapita mawaziri wengine wengi na kuondoka au kuondolewa. Hatimaye akaja au akaletwa Afande Alphaxard Kangi Ndege Lugola.
Askari polisi aliyeamua kuvua magwanda hata kabla ya kustaafu na kuingia kwenye siasa.
Baada ya miaka michache ya mikwara ndani ya Bunge, Afande Kangi Lugola akateuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani. Wizara aliyoifanyia kazi awali. Anaijua. Anajua mipaka yake. Kwa hiyo asingetarajiwa ‘kuvuka mipaka’ kama Mrema.
Kwa muda mfupi aliokuwapo katika wadhifa huo, Kangi alifanya mambo kadhaa. Alitoa maelekezo mengi tu. Alisimamia majeshi yaliyokuwa chini yake, likiwamo Jeshi la Polisi.
Lakini kwa nini mimi huwa ninamkumbuka Alphaxard Kangi Ndege Lugola?
Kuna amri yake moja ambayo nilitamani sana kabla hajatolewa iwe imeanza kutekelezwa; safari za usiku za mabasi ya abiria.
Safari hizi zilikuwapo nchini kwa miaka mingi tu baada ya uhuru. Mabasi yalisafiri usiku na mengi yalifika asubuhi yalikokuwa yakienda. Safi kabisa.
Yaani mtu unafanya shughuli zako mchana kutwa, jioni unajisogeza stendi (Kisutu, Mnazi Mmoja au Msimbazi) na kuanza safari kwenda Mbeya, Moshi, Arusha, Dodoma na kwingineko. Safi kabisa!
Tulisafiri namna hiyo. Sikuwahi kupaona Mombo au Mbwewe mchana. Ni usiku tu!
Baadaye safari hizo zikapigwa marufuku. Kwa nini? Kwa sababu eti zinasababisha ajali za mabasi. Kwamba madereva wanalala.
Waziri Mkuu John Malecela (wakati huo) akaagiza kuanzia Mei 1, 1992 marufuku mabasi kutembea usiku.
Serikali imeamua. Tukaanza kusafiri mchana. Mbwewe na Mombo zikafa, kwa kuwa watu wanakula wanapotaka. Waliochukia wakachukia, waliofurahi wakafurahi.
Miaka karibu 30 baadaye, Afande Alphaxard Kangi Ndege Lugola, akaona hakuna sababu ya watu kulazimishwa kusafiri mchana na kuwalazimisha kulala usiku.
Akalielekeza Jeshi la Polisi kujipanga ili kurejesha safari za usiku. Miaka 30 ni mingi. Watu wameshasahau kama mabasi yanaweza kuondoka Dar saa 11 jioni kwenda Mbeya au Mwanza.
Wengine wamekwisha kusahau hata sababu za kupigwa marufuku kwa safari za usiku, achilia mbali mtu aliyepiga marufuku.
Wengine wengi wala mwaka huo hawakuwapo na kama walikuwapo hawakuwa na habari kuhusu safari na usafirishaji.
Eti walikuwa bado ‘malaika’ kana kwamba malaika ni viumbe wadogowadogo na wazuuuri, wakati ukweli ni kwamba malaika ni ‘mijitu’, kwa kuwa moja ya kazi zao ni kupambana na shetani.
Wakati Afande Lugola akitaka kurejeshwa kwa safari hizo, sababu za kuzikataza zikawa zimeshabadilika. Si ajali tene, bali ni ujambazi!
Hivi Tanzania kuna majambazi wangapi? Yaani watu milioni 20 au 30 wanaosafiri mara kwa mara wasumbuliwe na vijambazi ‘uchwara’ 100 tu!
Tanzania nzima inalazimika kujifungia ndani kuanzia saa 4 usiku sababu ya majambazi! Hili halimuingii akilini Afande Kangi.
Naam! Jeshi la Polisi limejitahidi kwa kiasi kikubwa kudhibiti ajali nchini. Wanastahili sifa.
Na kwa kuwa ajali ndizo zilisababisha Mzee Malecela akakataza safari za usiku; na kwa kuwa sasa zimedhibitiwa; basi safari hizo zirejeshwe na za mchana pia ziwepo.
Tunaopenda kusafiri usiku tupewe haki!
Ndiyo maana nilitamani sana maelekezo ya Alphaxard Kangi Ndege Lugola yangetekelezwa kabla hajaondoka kwenye nafasi ile.
0679 336 491