Nilisoma, hivi karibuni, makala inayotoa matokeo ya taarifa ya kitafiti juu ya uwiano uliyopo kati ya msamiati wa mtu na uwezo wake wa kumudu somo la hisabati. Matokeo yanaonyesha kuwa msamiati mzuri unaongeza uwezo wa kumudu somo la hisabati.
Tafiti nyingi za aina hii zinaripotiwa kwenye maeneo yanayotumia lugha ya kiingereza, lakini bila shaka matokeo yatafanana hata kwa watumiaji wa lugha nyingine, pamoja na Kiswahili.
Uelewa wa somo linalofundishwa ndiyo msingi wa mwanafunzi kuelewa somo vyema. Kwa hiyo si jambo la ajabu kuwa mwanafunzi mwenye msamiati mzuri akaweza kumwelewa vyema zaidi mwalimu mwenye msamiati mzuri wa maneno mbalimbali yanayotumika kufundishia hisabati.
Lakini suala la umahiri katika msamiati na matokeo chanya haukomei kwenye hisabati pekee. Zipo tafiti zinazoonyesha kuwa watu walio mahiri katika matumizi ya msamiati wana akili zaidi kuliko wale ambao hawana msamiati mzuri.
Kipimo cha akili hakiwezi kuakisi mazingira yote yanayohitaji matumizi ya akili. Kila kazi inaweza kuwa na kigezo chake kupima kiwango cha akili kinachohitajika kufanikisha kazi hiyo. Na tunaweza kusema, bila kuathiri matokeo ya utafiti, kuwa mfugaji wa Kizanaki mwenye msamiati mzuri wa lugha ya Kizanaki ataonekana kuwa mwenye akili kuliko ambaye hana, kama ambavyo mhandisi mwenye msamiati mzuri wa kazi zake ataonekana mwenye akili kuliko wenzake wenye msamiati mbaya.
Tafiti hizi zinaibua swali ambalo linajitokeza kwenye matumizi mabaya ya lugha ya Kiswahili ambayo tunayashuhudia kwenye enzi hizi za teknolojia nyingi za kila aina zinazoambatana na uwezo hafifu kabisa wa matumizi sahihi ya lugha.
Hapa sizungumzii lugha za asili ambazo wengi wetu zimeanza kutupiga chenga, au lugha za kigeni ambazo hatujajifunza vyema. Nazungumzia Kiswahili, lugha yetu ya taifa.
Kuna kila aina ya matumizi mabaya ya lugha, lakini nitajikita kwenye matamshi yasiyo sahihi. Inashangaza kwamba mara nyingi Watanzania hushindwa kutamka maneno na majina yanayotumika mara kwa mara kwenye mazungumzo. Tatizo hili halipungui, bali linaongezeka, siku hadi siku, na mshangao unaanza kugeuka kuwa imani kuwa tatizo linaweza kuwa na athari pana zaidi kwa jamii.
Nimeshaandika kwenye safu hii juu ya kushangaa kwanini mtu huyo huyo atamke neno au jina kwa usahihi dakika moja, lakini akosee kutamka jina au neno hilo hilo dakika inayofuata. Utasikia watangazaji mtu akitamka “ruhusa” na “luhusa” kwenye sentensi moja.
Ni watu ambao bila shaka wamefundishwa na wanao uelewa wa kutamka kwa usahihi maneno au majina yanayotumika kwenye mazungumzo, lakini ni watu pia ambao hawaoni au wanashindwa kuzingatia umuhimu wa kutumia matamshi sahihi kila wakati.
Kwa mtu ambaye anawasikiliza atadhani kuna nafsi mbili ndani ya mwili wa mtu mmoja na, kwa kupitia matamshi, linajitokeza suala la kupeana zamu ni ipi nafsi kati ya hizo inaibuka na matamshi sahihi na ili inaboronga.
Kwa walimu wa lugha suala la kuongea au kuandika lugha ni suala linalozingatia kanuni za lugha husika. Miongoni mwa kanuni muhimu kabisa ni kutamka maneno au majina kwa usahihi. Maneno mengi yasiyotamkwa kwa usahihi hayaleti maana yoyote au yanaleta maana isiyokusudiwa, na maana nyingine zinaweza kuwa zilizokosa staha.
Tunasikia mara kwa mara kuwa upo umuhimu mkubwa wa kuzingatia sheria, kanuni, na taratibu ndani ya jamii ili kulinda uwepo wa uhusiano mwema baina ya wanajamii. Kwenye kampeni yake ya Utii wa Sheria Bila Shuruti, Jeshi la Polisi linaeleza kuwa kampeni hiyo inakusudia kuongeza amani, utulivu, na kupunguza vitendo vya uvunjaji sheria.
Lakini unaanzaje kujenga utamaduni wa kuheshimu kanuni ndani ya jamii kwa baadhi ya watu ambao wanashindwa au hawana desturi ya kuheshimu kanuni ndogo tu za matumizi ya lugha?
Mimi naamini kuwa, kwa sehemu kubwa ya watu ambao hawaoni umuhimu wa kuzingatia sheria, msingi wa uvunjaji wa sheria ni mlolongo wa athari ambazo wanazifyonza katika makuzi na mazingira wanamoishi, katika tamaduni, na katika desturi walizozoea. Sioni kuwa ni jambo linalofanyika kwa makusudi, ila matokeo tu ya kuwapo ndani ya mazingira ya aina fulani.
Naibua nadharia tete, suala ambalo sina uhakika nalo, lakini ambalo naamini linaweza kuthibitishwa kwa utafiti, kwamba binadamu asiyejali sana au hana mazoea ya kuheshimu kanuni ndogo za matumizi sahihi ya lugha anaweza kuwa na urahisi mkubwa zaidi wa kupuuza kanuni, taratibu, na sheria zilizopo ndani ya jamii.
Mtu anayepuuzia vikanuni vidogo vidogo vya lugha atakuwa mwepesi zaidi kuendelea kutoheshimu kanuni na taratibu nyingine, na hatimaye sheria. Kwamba anayeheshimu kanuni ndogo ataheshimu zile kubwa pia. Si zote zinavutwa?
Napata ujasiri kidogo kuibua hoja ya aina hii baada ya kusoma kuwa msamiati mzuri unajenga uwezo mkubwa zaidi wa hisabati.
Kisichoelezwa kwa uwazi kwenye matokeo ya tafiti hizi ni kuwa uwezo mpana wa msamiati unamsaidia anayetumia ile lugha kujifunza vyema darasani na nje ya darasa juu ya masomo na dhana nyingine muhimu za jamii: hisabati, ujasiriamali, umuhimu wa kufuata kanuni, taratibu, na sheria, na hata demokrasia. Unaanzaje kuheshimu katiba kama hujawahi kuisikia? Unaanzaje kuheshimu katiba bila kuzingatia kanuni, taratibu, mazoea, na desturi?
Ni wazo tu.