Hivi karibuni nilikutana na bwana mmoja mtaalamu wa masuala ya kompyuta, aliyenishawishi na kunishauri niwe na “application” kwenye “google play”. (Nimeshindwa kupata Kiswahili cha “Google Play” na “Application”). Kwa kifupi huu ni mfumo unaopatikana kwenye simu za “Smartphones, tablet na iPads”, ambao unakuwezesha kuwasiliana na kufanya biashara.

Kwa upande wangu mtaalamu huyu alinieleza kuwa ninahitaji kuwa na “application” ambayo nitaipa jina nitakalo na ambayo itaniwezesha kuuza na kutangaza bidhaa na huduma zangu ikiwamo vitabu, semina na machapisho mbalimbali. Ni kama kumiliki duka la mtandaoni lakini unaloweza kuwafikia watu wengi kupitia vifaa vya kielektroniki wanavyotembea navyo mikononi.

Ninafahamu uwepo wa maduka ya mtandaoni; na nimekuwa nikifuatilia kwa ukaribu mabadiliko yanayotokea kwa kasi kwenye biashara mbalimbali kutokana na mageuzi makubwa ya kimawasiliano. Kinachotokea sasa ulimwenguni ni “mapinduzi ya kiuchumi” ambayo dunia haijawahi kushuhudia. Mapinduzi haya yanamuathiri kila mtu, yanaathiri biashara zote – ndogo na kubwa; uwe unafahamu ama uwe mbumbumbu ni kwamba unaathirika.

Uchumi unahama, biashara zinahama hivyo ni lazima wafanyabiashara nao wahame kifikra na kimatendo. Kinachotokea China leo kinaweza kukuathiri wewe uliyepo kule kijijini Namanyere, Sumbawanga. Ngoja nikupe mfano mmoja. Sasa hivi kumetokea mapinduzi makubwa ya nishati ya jua (solar) kiasi kwamba kuna taa za sola, tochi za kuchaji kwa sola, redio za sola na vifaa vingine lukuki.

Katika mapinduzi haya hebu mtafakari mtu ambaye uchumi wake ulikuwa unategemea biashara ya kutengeneza na kuuza vibatari. Bila shaka biashara ya vibatari imetikiswa sana. Suluhu kwa mfanyabiashara wa vibatari si kulia na kulalamika; bali suluhu ilikuwa kubadilisha biashara mapema ama kuamua kubadilika sasa.

Mabadiliko yanayotokea katika ulimwengu wa uchumi na biashara yamenisukuma kutafakari kwa kina mambo mengi kuhusu mgeuko unaopaswa kuchukuliwa.

Nimekuwa nikifuatilia kwa ukaribu mwenendo wa uchumi wa dunia na nadharia zake zinavyobadilika. Na nimekuwa nikijitathmini na kujiweka sawa “repositioning” kwa uchumi wangu binafsi na wa biashara zangu ili mabadiliko yanayotokea ‘duniani pote’ yasinichinje.

Kimsingi Adam Smith ndiye anayetajwa kuwa baba wa uchumi wa kisasa (Classical Economics) kupitia kazi yake iliyotukuka iliyochapwa katika andiko liitwalo “Wealth of the nations”. Kazi hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1776. Smith alifuatiwa na warithi wake wakiwamo John Stuart Mill na Mfaransa machachari Jean-Baptiste Say.

Hata kizazi cha wanauchumi kilichoibuka miaka ya 1970 wakiongozwa na Robert Lucas na Edward C. Prescott bado waliendelea kujenga misingi ya kazi zao kwa kukosoa nadharia za Smith. Hawakuwa na mapya mengi isipokuwa walijitahidi kubomoa alichosimamisha Smith. Wanauchumi wengine waliibuka wakiwamo John B. Taylor na Huw Dixon.

Taylor na Dixon walipinga vikali ukosoaji wa akina Lucas na Prescott kitu ambacho kilisababisha kuzaliwa kwa mawazo mapya katika uchumi yaliyobatizwa uchumi fungani wa kimamboleo (neo-classical synthesis). Vile vile mwanauchumi Amartya Sen akaja na uchumi wa kimaendeleo (development economics) na mwingine Joseph Stiglitz akaibuka na nadharia ya uchumi wa mawasiliano (information economics).

Kimsingi mwanauchumi Smith (na wengine wa zama zake) waliibua nadharia za uchumi wakati wa mapinduzi ya viwanda yaliyokuwa yanatokea hasa katika nchi za Ulaya. Ni wakati huo ikathibitika kiuchumi ya kwamba ili uzalishaji uwepo ni lazima kuwepo na mambo yafuatayo: ardhi, rasilimali watu, mtaji na ujasiriamali. Mambo haya ndiyo yaliyokuwa msingi wa uchumi, biashara na mafanikio.

Ni katika zama hizo ndipo yalipotokea mambo ya mabwana (landlords) na watwana (watumwa/wafanyakazi). Utajiri wa mtu ulikuwa unapimwa kwa kuangalia kiwango cha ardhi anayomiliki, idadi ya wafanyakazi alionao kisha baada ya hayo inafuatia suala la mtaji na ujuzi alionao katika kusimamia rasilimali anazomiliki (ujasiriamali). Katika zama hizo mtu asiemiliki ardhi ilikuwa ni vigumu sana (haiwezekani) kujikomboa kiuchumi.

Dunia imebadilika sana na tayari imeingia kwenye zama nyingine mpya inayoitwa zama ya taarifa, ama kizazi cha taarifa (information age). Zama hizi za taarifa zimeambatana na zama nyingine pacha iitwayo zama ya huduma (service age). Licha ya kwamba viwanda bado vina umuhimu lakini uchumi sasa unaondoka kuegemea kwenye viwanda kwenda kwenye taarifa na huduma.

Zama hizi mbili pacha zimebadilisha kabisa mfumo wa uchumi wa dunia, zimepindua biashara na zimeielekeza dunia mahali ambako haikufikiria kwamba itafika. Yale mambo ya msingi katika uzalishaji yaliyokuwepo katika uchumi wa akina Adam Smith (wa mapinduzi ya viwanda) nayo yamebadilika sana.

Kabla sijaendelea nataka nitanabaishe jambo moja. Katika nchi hasa zinazoitwa “zinazoendelea”, tumekuwa wazito sana kuendana na mabadiliko yanayoendelea duniani. Hii ni pamoja na kutobadilika haraka hata katika mitaala yetu ya kielimu. Mathalani, mimi nimehitimu shahada ya Uchumi na Biashara mwaka 2011, lakini sehemu kubwa ya mtaala ulionipika katika uchumi ni wa kutoka nadharia za mwaka 1776 za Adam Smith!

Licha ya kwamba kila siku kuna mapinduzi mapya ya nadharia za kiuchumi inachukua muda sana kubadilisha mitaala yetu. Nachelea kusema kwamba tunazalisha wasomi waliopitwa na wakati kwa sababu tunatumia maarifa yaliyopitwa na wakati. Ndiyo maana msomi yeyote anayeacha kujisomea baada ya kupata vyeti, muda wowote anakuwa “outdated”.

Zama mpya za uchumi tulizonazo, ambazo ni za vizazi pacha vya taarifa(information age) na huduma (service age), vinatajwa kwamba vilianza rasmi baada ya kumalizika Vita Baridi (Cold War) kulikodhihirika baada ya kuanguka kwa ukuta wa Berlin kuelekea miaka ya 1990. Vile vile uzinduzi wa mtandao wa kompyuta (world wide web — www), kunatajwa kama ndiyo sherehe ya uzinduzi wa zama za mawasiliano.

Kwa nini nimekujulisha historia hii ya uingiaji wa zama za taarifa? Ni kwa sababu ninataka utambue kuwa uchumi wa dunia umebadilika na uelewe umebadilikaje. Kabla ya zama hizi mpya ilikuwa haiwezekani kuzalisha mali (utajiri) pasipo kuwa na ardhi na tena haikuwezekana kuzalisha mali pasipo kuwa na mtaji (fedha, mashine, malighafi, n.k). Katika zama mpya za kiuchumi na kibiashara unaweza kuzalisha mali na utajiri pasipo kutumia ardhi na pasipo kutumia mtaji (wa mtazamo wa uchumi wa zama za viwanda).

Kuanzisha biashara katika zama za viwanda ilikuwa sio rahisi lakini katika zama hizi za taarifa kuanzisha biashara ni rahisi mno. Kwa nini? Ni kwa sababu, vigezo vya uzalishaji katika uchumi wa taarifa ni hivi: taarifa, wazo, uwezo wa kuwasiliana na ujasiriamali. Utagundua kuwa mambo matatu kati ya manne yaliyoaminika kuwa ni kikwazo cha mtu kuzalisha mali na kupata utajiri, hayapo tena katika zama hizi za uchumi wa taarifa. Ujasiriamali ndio kigezo pekee kinachoendelea kubaki.

Ardhi, rasilimali watu, na mitaji sio mambo yanayokuja juu unapowaza kuanzisha biashara katika zama za uchumi wa taarifa. Najua wachumi wengi watanikunjia sura zao kwa nadharia mpya ninazowaletea hapa. Ni kwa sababu miaka nenda rudi wamefundishwa, wakaamini na wanaendelea kutumia nadharia ya mwaka 1776, isemayo ardhi, watu, mitaji na ujasiriamali ndio vigezo vya kuzalisha mali na utajiri (factors of production).

Nafahamu kuna watu wataniuliza, “Je, ardhi, watu na mitaji haina umuhimu katika kufanya biashara?” Hayo bado yana umuhimu lakini sio kwa asilimia mia moja katika uchumi wote na tena sio kwa biashara zote. Uhalisia ni kwamba hii sio misingi mikuu (ama niseme si misingi pekee) ya uzalishaji mali katika uchumi wa zama za taarifa.

Unachotakiwa kufahamu ni kwamba zamani (zama za viwanda) uchumi ulishikwa na biashara zinazotegemea ardhi, mitaji na watu. Lakini biashara zinazoshikilia uchumi wa sasa(zama za taarifa) ni zile ambazo hazitegemei ardhi, mitaji wala watu kuzalisha fedha, mali na utajiri. (Kwenye sehemu ya pili ya makala hii nitakueleza zaidi kuhusu hili).

Hata unaposoma machapisho ya Joseph Stiglitz, mwanauchumi aliejitahidi kuelezea uchumi wa taarifa; bado utagundua kuwa anapata kigugumizi kikubwa kuhusiana na kubadilika kwa misingi ya uchumi iliyoaminika kwa miaka mingi. Hata hivyo uhalisia uliopo sasa ni kwamba biashara zinategemea akili kuliko mitaji.

Zinategemea mawasiliano kuliko ardhi, zinategemea  taarifa kuliko hata fedha na zinategemea mawazo (ideas) kuliko hata rundo la wafanyakazi. Uchumi wa zama za taarifa unakuwezesha kuzalisha mali na utajiri wa kiwango chochote pasipo kutegemea ardhi wala mtaji(wa maumbo ya zama za viwanda).

Ukweli ni kwamba katika zama hizi mpya za kiuchumi tunahitaji watengeneza ajira wengi kukabiliana na wimbi la watafuta ajira; kwa maana hiyo tunahitaji biashara zinazokua na kustawi  katikati ya mabadiliko. Hatuwezi kufika hapo kwa kutumia fikra za zamani. Kwa sababu dunia imeshaingia kwenye zama mpya za kiuchumi ni lazima tujifunze kuzisoma nyakati na kuyajua yatupasayo kutenda.

Katika makala hii leo nimejaribu kukujengea msingi na picha kinagaubaga ili ufahamu kuwa tupo kwenye zama mpya kabisa za kiuchumi. Wiki ijayo nitaendelea na sehemu ya pili ya makala haya. Ikiwa una mpango wa kuanzisha biashara; ama ikiwa umo kwenye biashara yeyote ile; iwe ni kupika maandazi, duka, ama hata kama unamiliki kiwanda; nitakuonesha namna unavyotakiwa kuwemo katika ulimwengu mpya wa biashara.

Kwa wanaohitaji kitabu changu nilichokiandika kiitwacho, “Ni wakati wako wa kung’aa” kinachoeleza kung’aa kiuchumi na kimaisha wasiliana nami kwa maelezo ya kukipata.

Biashara isiyouingia ulimwengu mpya, kufa ni lazima itakufa!

0719 127 901, [email protected]