Kuna njama za kuhujumu uchumi na kudhulumu utu na uchumi wa Mtanzania daima dumu. Njama hizo si ndogo, ni kubwa na zinatekelezwa usiku na mchana na mabeberu wa dunia wakishirikiana na Watanzania wenzetu. Wananchi hatuna budi kulifahamu hilo na kuwa makini kulishinda.
Hivi ninavyozungumza mabeberu na Watanzania hao walioshiba mali ya dhuluma ya mkulima na mfanyakazi katika majiji, miji na sehemu nyingine, wana kula njama za kudhalilisha uhai na utu wako, watoto wako, wazazi wako na jamii nzima ya Watanzania.
Watanzania hawa wanahujumu mali na mipango yetu ya maendeleo kwa sababu tu za kuendekeza nafsi zao za kutaka mali, madaraka, heshima na ubwana. Hawawezi kuacha njama hizi hadi wamekumaliza kifikra na kiuchumi, huku wakighilibiwa na kufanywa mazuzu kwa ulimbukeni wao wa anasa za dunia.
Tamaa ya kutaka mali na kupata madaraka kunawazuzua na kutawaliwa mioyoni kupuuza utu wao, utaifa wao na kuwa kama wanyama. Huu ni uhayawani usio vumilika na kukubalika kuachiwa kustawi na wananchi wa taifa hili, kwani unyonyaji wa mali ni unyama.
Wahujumu uchumi hawafurahi kuona taifa lolote linajikwamua katika umaskini na kuuendea utajiri, kwa sababu watakosa utamu wa kunyonya na kudhulumu mali na kudhalilisha heshima ya taifa hilo.
Taifa kama letu, tunapoamua kuuvua umaskini na kukataa dhuluma ya aina yoyote, tutapata misukosuko na kupigwa vita ya kiuchumi kupitia milango ya masilahi ya nchi. Nazungumzia mambo ya diplomasia, misaada ya kiuchumi, propaganda, uchochezi na vita.
Mambo kama haya mabeberu huyatumia kutekeleza na kufikia masilahi ya nchi moja ndani ya nchi nyingine. Ili wapate fursa hiyo huwatumia raia au wananchi wa nchi husika kusaliti na kuhujumu uchumi wa nchi yao. Katika muktadha kama huu mapambano yake huwa makali na makubwa.
Katika kujenga maisha bora na kuondoa umaskini wa mtu na wa taifa, ni kupambana na mabeberu, vibaraka na wasaliti wenye shahada ya dhuluma, ujinga, ulimbukeni au ya kutojitambua. Watanzania ni wajibu na haki yetu kuitambua vita hii ya kiuchumi. Wakombozi wa uchumi wetu ni sisi.
Naomba ifahamike kwamba ‘kutojitambua’ ni maradhi hatari na makubwa kuliko maradhi yoyote unayoyafahamu. Ni maradhi yenye kukupumbaza akili na nguvu za fahamu. Yanamfanya mtu kutenda mambo ya ubwege, ujinga hata ya upumbavu. Katika hali kama hii tuwe makini katika shughuli zetu.
Tambua wapo ndugu zetu ambao hawajitambui. Wanahitaji kufundwa na kupewa elimu maarifa ili wapate kujikomboa. Kwani wana akili hawazitumii, wana macho hawaoni na wana masikio hawasikii. Dawa ni kuwatia adabu, kuwazibua masikio na kuwafumbua macho.
Tendo lililofanywa na beberu wa Kizungu akishirikiana na Watanzania ( kama inavyotuhumiwa ) kuzuia ndege yetu ya abiria huko nchini Afrika Kusini, kwa takriban siku 10 ni tendo la kuhujumu uchumi wetu na udhalilishaji wa taifa letu. Ukweli wananchi tumefedheheshwa na tumehuzunika.
Ni kweli Watanzania tuna wiwa na beberu huyo, lakini ndege na deni havina uhusiano. Vipi unazuia chombo kinachotafuta pesa ili ulipwe deni lako? Ama kweli wahenga wanasema: “Akili nyingi huondoa maarifa.” Alhamdulilahi! Tumeshinda shauri. Na ndege yetu imeachiwa na sasa inakata mawingu.
Tukio hili ni somo tosha kwenu Watanzania. Tukumbuke mtu hupata jando au unyago mara moja tu. Na dawa ya deni ni kulipa. Watanzania tujitambue, tubadilike na tuache mazoea katika kuendesha maisha yetu, kwani sayari tunayoishi ina vituko vya dhuluma, wizi na hiyana.
Si wajibu wetu tu, bali pia ni haki yetu kutunza na kulinda mali zetu kwa uwezo na maarifa yote tuliyonayo. Tusikubali kuhujumiwa katika nyanja yoyote. Hili linawezekana. Tuanze ukombozi huu sasa. Narudia kusema tunaweza.