*Wakenya wajipenyeza hadi ndani ya CCM na kushinda udiwani wakati si raia
*Maslahi binafsi yatawala, wafikia hatua ya kumkashifu Waziri Mkuu hadharani
*Waamini wao ndio wenye turufu kuamua nani awe Waziri wa Maliasili Tanzania
*Seneta wa Narok aishambulia Tanzania bungeni kwao, apinga Loliondo kuhifadhiwa
ARUSHA
Na Manyerere Jackton
Mgogoro wa ardhi unaoendelea katika Pori Tengefu la Loliondo (LGCA) mkoani Arusha ni wa kiuchumi, huku raia na walowezi kutoka Kenya wakiwa vinara wa mgogoro huo.
Ripoti zinabainisha uwepo wa mamia kwa maelfu ya Wakenya katika tarafa za Loliondo na Sale wakiendesha shughuli za ufugaji ng’ombe, mbuzi na kondoo.
Wageni hawa wameigeuza Loliondo na Sale kuwa eneo la kuchunga na kunenepesha mifugo kabla ya kuwauzia wenye viwanda vya kusindika nyama walioko Narok (mpakani na Loliondo) na Nairobi.
Uchunguzi uliofanywa miaka kadhaa iliyopita ulibaini kuwapo kwa mamia ya Wakenya wakiwa na maelfu ya mifugo katika vijiji vya kata za Engaresero, Orgosorok, Oloipir, Oloirien-Magaiduru, Oloosoito-Maaloni na Ololosokwan.
Wakenya hao wamejipenyeza hadi kwenye uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na kwenye serikali za vijiji. Ushahidi wa madai haya upo wazi. Baadhi ya Wakenya wameshika hadi nafasi za udiwani kabla ya kuomba na kupewa uraia. Baadhi ya NGOs zinaongozwa na Wakenya na ndizo zimekuwa mstari wa mbele kupinga uamuzi wowote wa serikali.
Lakini mbaya zaidi, kwa siku za karibuni kumejitokeza viongozi wa jumuiya za CCM, wabunge na baadhi ya watu wenye masilahi binafsi kuhakikisha wanakwamisha mpango wowote unaolenga kuilinda Loliondo. Wengine wamejitokeza hadharani kumkashifu na hata kumtukana Waziri Mkuu na viongozi wengine wakuu.
Kutokana na jamii inayoishi eneo la mpakani mwa Tanzania na Kenya kuwa ni ya koo mbili za Loita na Purko; hali hiyo imefanya mwilingiliano uwe rahisi. Ardhi ya Tanzania imekuwa shamba la bibi kutokana na sheria zinazohalalisha rasilimali hiyo kuwa mali ya umma chini ya udhamini wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Tofauti na Tanzania, ardhi ya Kenya ni mali ya mtu binafsi, hali iliyowafanya wachache wenye ukwasi wawe wamiliki.
Pale upande wa Kenya unapoona Serikali ya Tanzania ikitaka kuratibu matumizi ya ardhi hasa kwa kutenga eneo la uhifadhi na la matumizi ya vijiji, mara moja upande wa Kenya kupitia viongozi wao mapandikizi na asasi za kiraia (NGOs), husimama imara kuikwamisha serikali.
Oktoba 5, 2017 viongozi wa vijiji na kata, hasa kutoka Ololosokwan walizuru Kenya na kupitia msaada wa Seneta wa Kaunti ya Narok, Ledama Olekina, wakafanikiwa kumuona kiongozi wa upinzani wakati huo, Raila Odinga; rafiki mkubwa wa Rais John Magufuli.
Wakamuomba Odinga amshawishi Rais Magufuli asitishe mpango wa kuhifadhi eneo la kilometa za mraba 1,500. Odinga alikubali kufanya kazi hiyo; na baadaye taarifa zikapatikana kwamba ameshamwambia Rais Magufuli juu ya kilio chao.
Hazikupita siku nyingi aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Jumanne Maghembe, aling’olewa kwenye nafasi hiyo; hali iliyoibua shangwe kubwa.
Ni Ledama huyu huyu ambaye juzi alisimama bungeni kwao Kenya na kuishambulia Tanzania kwa msimamo wake wa kuihifadhi Loliondo. Kwa ufupi Wakenya wanataka Loliondo iendelee kuwa himaya yao ya malisho na huduma nyingine za kiuchumi.
Kabla na baada ya tukio hilo, Wakenya wanaamini kuwa wao ndio wenye turufu ya nani awe nani katika Wizara ya Maliasili na Utalii alimradi tu awe upande wa masilahi yao, hasa kwa kuhakikisha hagusi habari ya Loliondo.
Baadhi ya viongozi waliokwenda na maji ni aliyekuwa Diwani wa Ololosokwan, Yanik Ndoinyo na Mwenyekiti wa Kijiji cha Ololosokwan, Kerry Dukunyi.
Kwa miaka yote tumesema raia wengi wa Kenya wamejipenyeza Tanzania na kujifanya ni Watanzania, lakini ukweli ni kwamba ni Wakenya wanaofanya mambo kwa manufaa ya Wakenya kwa kutumia ardhi ya Tanzania.
Mifugo mingi iliyoko Loliondo ni mali ya Wakenya. Inanenepeshwa Loliondo na baadaye kuuzwa Kenya kupitia minada ya Wasso na mnada mkubwa kabisa uko Posmoru upande wa Kenya.
Wafugaji kutoka Kenya wamevuka kutoka Pori Tengefu la Loliondo hadi kuingia ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti. Vijiji kama Ololosokwan, Kirtalo, Maalon na Arash ni mfano halisi wa namna walowezi walivyojipenyeza nchini.
Katika kipindi cha Machi na Aprili, 2017, Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya, kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya, Kata na Vijiji ilifanya operesheni kuwabaini walowezi na mifugo yao walioingia kiharamu kutoka Kenya.
Hawa ni wa jamiii zote za Purko na Loita katika vijiji vya Ololosokwan, Kirtalo, Mondoros, Oloipiri, Arash, Olalaa na Piyaya. Idadi iliyopatikana kwa majina na vitongoji walipokuwa wamevamia ilifikia 175 (orodha tunayo).
Hawa watu 175 peke yao walikuwa na mifugo 31,371; ng’ombe wakiwa 15,461. Fikiria, idadi hiyo ya mifugo ya nje ndani ya ardhi ya nchi nyingine huru!
Kisingizio ilikuwa ni ukame mkubwa uliokuwapo maeneo ya kwao, yaani Narok na Kajiado nchini Kenya. Hili la ukame linatumika kama kisingizio lakini ukweli ni kuwa Loliondo ndilo shamba lao!
Tunao ushahidi wa maandishi unaoonyesha namna viongozi wa Kenya wanavyowasiliana na baadhi ya viongozi wa vijiji ili wawaruhusu kuingiza mifugo yao kwa ajili ya malisho.
Kudumu kwa mgogoro wa Loliondo kunatokana na aina ya masilahi hatarishi ambayo yamekuwapo kwa baadhi ya watu wasio na nia njema na taifa letu. Mgogoro huu ulianza kwa mara ya kwanza baada ya kuanzishwa kwa shirika (NGO) la KPOK mwaka 1992.
Shirika hili liliongozwa na Lazaro Parekipunyi. Baadaye zikaanzishwa NGOs za LADO na OSEREMI. Mwanzoni mwa miaka ya 2000 ikaanzishwa Pastoralist Women Council (PWC) na viongozi wake walikuwa marafiki wa Parekipunyi.
NGOs zilikuwa na kazi ya kuwaelimisha vijana wa jamii ya wafugaji kupata elimu, hasa elimu ya sheria ili kufanya kile walichokiita kuwa ni kulinda ardhi yao. Wazo hilo la ‘kulinda ardhi’ lilitolewa na William ole Ntimama ambaye hadi anakufa nia yake ilikuwa kuwafanya Wamasaai wawe na nchi yao (Maasai Land). Mpango huo ungali hai.
Umoja huu wa kuwa na ‘nchi yao’ umezima mgogoro wa kikabila katika tarafa za Sale na Loliondo ambao ulikuwa ukisababisha vifo na maafa mengine.
NGOs za PWC, UCRT, PINGOs, NGONET, PALSEP, RAMAT, TPCF na nyingine nyingi zimeanzishwa na kujipatia fedha nyingi kwa kigezo cha kuwatetea Wamaasai. Japo ajenda yao inaonekana ni ya utetezi, lakini nyuma ya pazia kuna siri kubwa inayobebwa na dhana ya masilahi binafsi ya kiuchumi.
Kuna kiongozi mkubwa wa zamani wa Tanzania akiwa msibani Loliondo, alisema: “Nawapongeza sana Wamaasai kwa kusimamia imara na kuhakikisha ardhi ya Wamaasai haiondoki. Hii ni vita yetu sote na tutashinda, mimi nipo nyuma yenu nafuatilia kwa karibu na tutashinda kwa umoja wetu.”
Kauli hii ilipokewa kwa furaha kubwa na Wamaasai wa Loliondo na wenzao kutoka Narok, Kenya. Mara moja ramani ya eneo la ‘nchi ya Wamaasai’ ikatolewa na kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii. Hapo ndipo ikafahamika kuwa kumbe suala si mgogoro wa ardhi tu, bali ni kujenga himaya ya kiutawala.
Kwa sasa hali ya Loliondo si nzuri. Kumekuwapo hamasa ya chini kwa chini inayofanywa na viongozi wa kisiasa na NGOs kwa ajili ya kuendeleza vurugu kwa nia ya kuivuta jumuiya ya kimataifa ione kuwa wananchi wa Loliondo wanapokwa ardhi yao, jambo ambalo si la kweli.
Ardhi ya Lolindo ya kilometa za mraba 4,000 ni mali ya serikali ndani ya Pori Tengefu. Hakuna ardhi ya kijiji na ndiyo maana Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewahi kusema hakuna Tangazo la Serikali (GN) la kutambua kijiji katika eneo la Loliondo.
Serikali kupitia kwa Waziri wa Maliasili na Utalii mwaka 2013 iliamua kuachia kilometa za mraba 2,500 ili zitumiwe na wana vijiji kwa kupitia mpango wa matumizi bora ya ardhi. Kilometa za mraba 1,500 zikapendekezwa ziendelee kutunzwa kwa sababu eneo hilo ni muhimu mno kwa ikolojia ya Serengeti – Maasai Mara.
Kwanini eneo hili ni muhimu?
Ni muhimu kwa sababu kadhaa:
i) Mosi, ni chanzo cha mito sita inayomwaga maji katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Asilimia 48 ya maji yanayoingia Serengeti yanatoka ndani ya Pori Tengefu la Loliondo. Eneo hili ni muhimu kwa ikolojia ya Serengeti ikiwa na vyanzo sita vya maji, mapito na mazalia ya wanyamapori.
Pia eneo hili linategemewa na wakazi wa kata saba kama maeneo ya makazi, malisho ya mifugo na upatikanaji wa maji kwa ajili ya shughuli zao za kila siku.
Baadhi ya vyanzo vya maji vilivyomo katika eneo hili:
*Mto Pololeti – vijiji vya Oloipiri, Soitsambu, Maaloni, Arash, Ololosokwan.
*Mto Irmolelian – vijiji vya Piyaya, Arash, Malambo, Maaloni.
*Mto Orgumi – Losoito, Arash, Oloipiri, Magaiduru, Piyaya.
*Vyanzo vya maji vya Lima One – vijiji vya Soitsambu, Oloipiri, Oloirien, Ololosokwan.
*Chanzo cha Maji Mlima Loilale – vijiji vya Ololosokwan, Kirtalo, Soitsambu.
*Chanzo cha Maji Mlima Loili – vijiji vya Ololosokwan, Soitsambu.
ii) Ni sehemu ya mazalia ya nyumbu na pundamilia ambao ni kivutio kikuu cha utalii.
iii) Ni mapito ya wanyama (ushoroba) wahamao kwenye ikolojia ya Serengeti-Maasai Mara.
iv) Pori Tengefu la Loliondo ni eneo la ‘kupumulia’ la hifadhi za Serengeti, Ngorongoro na Maasai Mara.
v) Pori hili ni chanzo kikuu cha mapato kwa serikali kutokana na utalii wa uwindaji na picha.
Mgogoro umekuwapo kwa kuwa NGOs zina masilahi binafsi – zinataka udumu ili ziendelee kuvuna fedha kutoka kwa wafadhili. NGOs. Serikali nayo imekuwa ikikosa utayari wa kuumaliza mgogoro huu mapema licha ya taarifa zote za wataalamu kuonyesha hatari inayolikabili eneo la Loliondo na Ngorongoro.
Baadhi ya viongozi wenye mamlaka ya kutoa uamuzi, ama wamekuwa waoga, au wanazembea kutekeleza mapendekezo ya wataalamu wa uhifadhi na Sheria ya Uhifadhi Namba 5 ya mwaka 2009, na kanuni zake za mwaka 2010. Mfano halisi ni kusuasua kwa uwekaji vigingi vya mpaka katika eneo la kilometa za mraba 1,500 linalopendekezwa kubaki Pori Tengefu.
Nguvu za wafugaji kutoka nchi jirani kutaka waendelee kutumia Loliondo kama sehemu yao ya malisho ni miongoni mwa sababu hizo. Lakini pia kuna taarifa za kiintelijensia za mkakati wa nchi jirani kuua utalii nchini mwetu ili watalii na wawekezaji waende kwao.
Kwanini mgogoro baada ya mwekezaji mpya?
Wizara ya Maliasili na Utalii kwenye taarifa yake ya Desemba 2017 inasema hivi: Tangu kipindi cha ukoloni eneo hili lilitumika kwa shughuli za uwindaji kwa wageni mbalimbali waliokuja nchini.
Kutokana na upatikanaji wa nyara nzuri na kubwa, tena kwa urahisi, serikali ililitumia eneo hili kwa ajili ya kuwindisha wageni wa kitaifa. Shughuli za uwindaji zilifanyika kwa wageni mbalimbali chini ya serikali hadi lilipoundwa Shirika la Wanyamapori Tanzania (Tanzania Wildlife Cooperation – TAWICO) mwaka 1978.
Shughuli zote za uwindaji wa kitalii zilisimamiwa na TAWICO hadi mwaka 1988 zilipokabidhiwa rasmi kwa Idara ya Wanyamapori. Wakati TAWICO ikisimamia uwindaji wa kitalii, eneo la Loliondo liligawanywa katika vitalu viwili; Loliondo North iliyotumiwa na Kampuni ya Safari East Africa Tanzania Ltd na Chasse de Afrique Safaris (ikisimamiwa na Munisi) na eneo la Loliondo South ambalo liliendelea kusimamiwa moja kwa moja na TAWICO.
Kwa kipindi hicho pia Gordon Gordon na mwindaji mahiri (PH) wa Kampuni ya TAWICO, Dan Tarimo, kupitia Kampuni yake ya Dan Tarimo Hunting Safaris, waliendesha shughuli za uwindaji wa kitalii katika eneo la Loliondo chini ya usimamizi wa TAWICO.
Kampuni ya TAWICO na Chuo cha Taaluma ya Wanyamapori Mweka waliwinda katika eneo hilo kwa ajili ya kupata nyara za kutumika katika kiwanda cha nyara cha TAWICO kilichopo Tengeru, Arusha.
Baada ya shughuli za usimamizi wa uwindaji wa kitalii kukabidhiwa Idara ya Wanyamapori mwaka 1988, TAWICO ilijiendesha kama kampuni ya uwindaji wa kitalii na iligawiwa baadhi ya vitalu vya uwindaji ikiwa ni pamoja na vitalu vya Loliondo hadi mwaka 1992 serikali ilipokodisha eneo hilo kwa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ambako ilibidi kuanzisha kampuni ya kusimamia shughuli hizo, yaani kampuni ya uwindaji wa kitalii ya Otterlo Business Cooperation (OBC).
Kampuni ya OBC ilitaarifiwa kuhusu matumizi ya eneo la Loliondo kwa uwindaji kwa wageni wa kiserikali/taifa.
Eneo la Pori Tengefu la Loliondo ni sehemu ya mtandao wa uhifadhi wa wanyamapori wa mfumo-ikolojia wa Serengeti (Serengeti ecosystem) unaojumuisha pia Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, Hifadhi ya Taifa Serengeti, Mapori ya Akiba Grumeti, Ikorongo, Kijereshi na Maswa.
Kwa mujibu wa Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009, makazi na kuchunga mifugo haviruhusiwi katika Mapori Tengefu.
Ushauri
Serikali haina budi kuumaliza mgogoro huu. Ripoti nyingi za Loliondo na mapendekezo vimeshatolewa kwa miaka zaidi ya 15. Hakuna taarifa isiyojulikana kwa mamlaka za uamuzi. Muda na fedha nyingi vimetumika kwenye mgogoro huu, na sasa ni wakati wa kuona thamani ya vitu hivyo.
Kwenye ripoti zote kumeelezwa umuhimu wa kuihifadhi Loliondo, hasa lile eneo la kilometa za mraba 1,500 linalopendekezwa litungiwe sheria maalumu ili kulilinda.
Walowezi kutoka Kenya waliojiingiza kwenye uchochezi wa mgogoro huu wasiachwe watambe. Tanzania ni nchi huru inayostahili kuachwa iamue mambo yake kwa masilahi ya watu wake, lakini pia na walimwengu. Faida za kuilinda Loliondo hazikomei kwa Watanzania pekee, bali kwa walimwengu, hasa kwenye suala la ikolojia.
Mamlaka za nchi zisiiache Loliondo ikawa ‘jamhuri’ ndani ya Jamhuri ya Muungano. Sharti taratibu na sheria za nchi kama vile uhamiaji zitumike katika kulinda usalama na masilahi ya nchi.
Kiburi kinachojengwa Loliondo cha baadhi ya watu kudai ardhi ni mali yao, na kwamba hawapaswi kuamuliwa na serikali, ni dharau kwa mamlaka za nchi.
Dharau ndiyo hii tunayoshuhudia viongozi wetu wakuu wakitukanwa hadharani. Endapo kila kabila likiamua kupinga uamuzi na mipango halali ya serikali nchi haitatawalika.
Suala la Loliondo na Ngorongoro limezungumzwa mno. Huu ni wakati wa kuondokana na hii migogoro inayochochewa na watu wasiotaka kuangalia masilahi mapana ya nchi, bali masilahi yao na wafadhili wao. Maneno yametosha. Sasa ni wakati wa kuzilinda Loliondo na Ngorongoro. Tusipofanya hivyo kizazi kijacho kitatushangaa.