Kuna mambo nadhani ni mhemko wa utandawizi (mnaitaga utandawazi) au ujinga tu wa kuiga wazungu tuliyapokea na kuyafanya ndio utamaduni wetu na hata kuyatungia sheria bila tafakari ya kina!
Na ilikuwa mtu ukiyatolea maoni tofauti unaonekana wewe wakuja au hamnazo! Bahati nzuri nchi imepata uongozi unaokerwa!
Nianze na hili la jana au juzi kuhusu mimba mashuleni. Kama mazuzu fulani hivi na tukiongozwa na wanaharakati uchwara taifa lilijikuta linaruhusu mimba mashuleni bila kujijua!
Kukazuka hoja za haki za binadamu! Ikaonekana kumzuia mtoto wa kike aliye pata ujauzito au aliyejifungua akiwa mwanafunzi kuendelea na masomo ni ukiukwaji wa haki za binadamu! Na mikataba ya kimataifa ikanukuliwa! Nchi ikashinikizwa kutunga kanuni za kuruhusu waliopata uja uzito na wamama warudi shule! Hata katika Umoja wa Afrika kukapitishwa maazimio ya kuwaruhusu waliopata ujauzito na waliojifungua wasome!
Kabla sijachambua ujinga huu nidurusu hali tuliyosomea sisi enzi za mkoloni na enzi za Mwalimu. Hakika zilikuwa enzi wala haingii akilini kuwa mwanafunzi atapata mimba! Na hata akipata eti aendelee kukaa darasani na waliozingatia uanafunzi wao. Nakumbuka enzi za Assumpta, Ashira, Machame na Kibosho Girls!
Ni enzi ilikuwa ikifika likizo mabinti wanapandishwa basi na matroni wawili watatu wanasindikizwa kwao! Siku ya kurudi hivyohivyo! Halafu muda mfupi kabla ya kupelekwa kwao wanapimwa uja uzito na karatasi ya kuonyesha kuwa binti karudi salama inakabidhiwa kwa mzazi anasaini!
Siku ya kurudi wakifika shule basi kituo cha kwanza dispensary ya shule au iliyo karibu wakapimwe! Ukikutwa na uja uzito unakuwa umeupatia kwenu na si shuleni! Unarejeshwa kwa walioshindwa kukulea fasta!
Wazazi hawakupenda aibu au fedheha hii kwa hiyo waliwapa ushauri nasaha binti zao mara kwa mara na kuwachunga vyema kama kondoo wa bwana! Mabinti wakamaliza masomo na wengi wao ni hawa wamekuja kutumikia taifa katika nyanja mbalimbali. Hivi ndio ilivyokuwa jamii yetu huko nyuma kabla hawajatokea wenye mtindio wa ubongo wazungu pori na wanaharakati majinuni! Vichwa maji watupu!
Sasa nichambue udhaifu wa hoja za kuruhusu binti alipata mimba kuendelea kukaa darasani.
Hoja ya kwanza; Hata wanaoshabikia ni aidha waislamu, wakristo au wana madhehebu fulani, na zote zinakataza zinaa. Cha kusikitisha kwenye nyumba zao za ibada na imani zao wanakemea zinaa lakini kwa wanafunzi wa kike wanaona sawa tu! Natambua kuna wachache tena wachache mno wanaobakwa na kupata mimba! Lakini hii haiwezi kuwa sababu ya kuidhinisha zinaa ya wengi! Hata ukidai ni watoto wanarubuniwa tutakuuliza kwani watoto ni wao tu? Mbona watoto wengine wamekataa kurubuniwa?
Pili; Mashabiki wanadai kuwakatalia wasisome ni kukiuka haki za binadamu! Hivi mwalimu yeye hana haki ya kufundisha mwanafunzi asiye na ujauzito? Hivi wanafunzi waliojiheshimu wao hawana haki ya kukaa darasani bila kuwa na mjamzito miongoni mwao? Mzazi yeye hana haki ya kumsomesha asiye na ujauzito?
Hivi wazazi ambao watoto wao wamejiheshimu hawavunjiwi haki kwa kujua anaposoma mwanae mwema kuna mjamzito darasani, hatapata hofu? Hivi huyo mjamzito si ana kichanga tumboni, chenyewe hakina haki ya kutosumbuliwa kutembezwa kila siku?
Na aliyezaa si ana kichanga, nacho hakina haki ya kukaa na mama? Sie mama zetu wangeenda kusoma wakatuacha majumbani si wangekuta tumeliwa na simba au chatu? Au tumeibiwa na mumiani wa enzi zile?
Tatu; Hivi mtaala utatekelezwaje? Mara mwanafunzi aende clinic, mara aende labour ward! Waalimu watafundishaje? Au kutakuwa na mihula maalum kwa wazazi?
Nne; Hivi ni ujumbe gani tunapeleka kwa wanafunzi wa kike? Kwamba ruksa? Haiwezekani kwa ruksa hii tukajikuta darasa zima kila mwanafunzi wa kike ana kakibuyu kake ka udongo analamba? Darasa litaenda?
Tano; Hivi tatizo la wanafunzi wa kike ni mimba tu? Akitokea mlevi, tumruhusu? Au kulewa si haki bali kusoma ndio haki? Kama kulewa si haki viwanda vya Nassari vinajengwa kwa nini? Tutatoa haki ipi na tuache ipi? Kama kulewa si haki hata kupata mimba ukiwa mwanafunzi si haki pia.
Ujauzito si kufutuka kitumbo! Kuna mambo yanaendelea ndani ya mwili wa mjamzito ambayo hayaruhusu elimu ya ngazi ya shule ya msingi wala sekondari. Inafaa tu kwa elimu ya vyuo, tusichanganye mambo.
Aliye shule ya msingi na sekondari ubongo wake bado haujakomaa kiasi cha kumudu masomo na uja uzito. Hasomei kozi kama wa chuoni. Na ukumbuke mwanafunzi huyo alichaguliwa na mwingine aliye faulu kama yeye akaachwa kwa kuwa nafasi hazitoshi. Ni bora hata apishe aliyeachwa aitwe!
Hii hoja ni hoja ya wazazi wenye uwezo na wenye shule binafsi. Wanataka wawaamulie masikini walio wengi! Mtoto wa tajiri anayesoma shule ya bei mbaya na abebe mimba na aendelee hukohuko shule ya kitajiri. Lakini wasilazimishe ndio iwe utamaduni wa wote.
Kwa masikini watoto ni mtaji! Watoto wakisoma na kuimaliza bila mimba ndio nafuu ya familia masikini, ndio mkombozi wao. Tusiwaharibie investment yao kwa kuiga matajiri!
Kama kweli mja mzito hatakiwi anyimwe huduma mbona mama akiwa na mimba anakataliwa kupanda ndege na hatusikii hawa wanaharakati uchwara wakidai ni ukiukwaji wa haki za binadamu? Mbona shirika la ndege likiruhusu na mama akapata matatizo angani wanalishitaki?
Unashitaki aliyempa mtu haki! Hizi double standards za nini? Tukubali kuna vitu ukiwa hali fulani huwezi. Mathalani ukawa na kitambi japo mwanamume wa 8 pack huwezi kudai usajiliwe Simba eti kwa kuwa una haki ya kucheza mpira! Hutaweza kucheza utafia watu uwanjani!
Kuna mambo mila na desturi zetu zinakataza na hakuna ubaya! Si kila mila yetu mbovu tuiache kama ambavyo si kila mila ya wazungu ni nzuri tuifuate! Mila yetu ni binti ajistahi hadi aolewe! Hakuna ubaya na hakika ni mila njema kuliko ya wazungu, ndio history yetu, ndio kitambulisho chetu cha uzawa.
Ndio maana haingilii akilini kwa mwanamke wa kiafrika kubeba jeneza. Si kwamba akibeba halitaenda la hasha, ni kwamba si mila yetu. Sawa na kuona mwanamme wa kiafrika anatoboa masikio au anavaa herein, si kwamba hawezi kuvaa lakini si utamaduni wetu, ni kuiga tamaduni za vichwa maji wa ulaya maana hata ulaya wenye akili hawafanyi hayo.
Sasa hawa wanaodai turuhusu wanafunzi wajawazito wakae darasani sijui wanakubali mathalani wakute mwalimu anafundisha mwanafunzi wodi ya wazazi? Maana ni kinyume cha utamaduni wetu, watadai ni haki ya binadamu.
Hivi hawa wanaodai mimba ziruhusiwe wao wana mabinti? Hivi wanakaa na kuwaambia ‘mwanangu nenda kasome ntakulipa ada hata ukipata mimba’? Au wanawaonya wasichanganye mapenzi na shule?
Kwa hili la mimba nimpongeze mheshimiwa Rais JPM kwa kuliona na kutamka bila soni kuwa si sahihi hata kidogo. Hongera Rais, sasa ntakuombea kwa kujua unachukia zinaa.
NA PRUDENCE KARUGENDO