Naandika makala hii nikiwa nchi jirani ya Uganda katika mji wa Masaka. Pamoja na kwamba niko nje ya nchi, nafuatilia kwa karibu kinachoendelea hapo nchini.
Kwanza kabisa niseme uchaguzi wa mwaka huu ni tofauti na uchaguzi wa miaka yote iliyopita. Kwa wenye kumbukumbu uchaguzi wa mwaka huu kwa mbali unaweza kuulinganisha na wa mwaka 1995 ulioelekea kuwa na hamasa sawa na huu.
Ikumbukwe mwaka 1995 Mbunge wa sasa wa Vunjo, Augustine Mrema akiwa Naibu Waziri Mkuu katika Serikali ya Awamu ya Pili ya Mzee Ruksa, Ali Hassan Mwinyi, alijiuzulu uwaziri wa Mambo ya Ndani na Unaibu Waziri Mkuu (cheo ambacho hakikuwapo kikatiba) akajiunga na NCCR-Mageuzi.
Mrema alibebwa, alielekea kuwa tishio la wazi kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), japo aliangukia pua.
Mwaka huu, Edward Lowassa Waziri Mkuu wa tisa wa nchi yetu, naye alijiondoa CCM na anawania urais kwa tiketi ya Chadema chini ya mwavuli wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Mrema aliangukia pua kutokana na sababu kuu mbili za msingi. Mrema alikuwa sawa na kimbunga, hakuwa na mtandao ndani ya CCM, Lowassa anao. Pili, Mrema alikutana na kisiki cha mpingo, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Mwalimu Nyerere alibadili upepo, baada ya kutumia ushawishi na mbinu za kisaikolojia kubadili mawazo ya Watanzania.
Wakati Serikali ya Mzee Mwinyi ilikuwa inafanya kazi ya kupiga mabomu misafara ya Mrema na kuagiza vijana wenye kushiriki maandamano ya Mrema wakamatwe, Nyerere alibaini kuwa mbinu hiyo haifanyi kazi.
Akasema: “Kama Mrema anataka kubebwa, mwacheni tu abebwe. Kubeba si jambo la ajabu, kwani hata maiti huwa wanabebwa kwenye jeneza.”
Sitanii, kauli hiyo ya Mwalimu Nyerere ilibadili upepo. Kwa bahati mbaya, Rais Benjamin Mkapa aliyetarajiwa kuwa angesimama jukwaani akabadili upepo kama Nyerere alivyomsaidia kubadili upepo wakati anagombea urais mara ya kwanza, ameingia jukwaani na sera ya matusi. Akawaita watu malofa, wapumbavu. Kauli hii ikachochea moto wa kuupenda upinzani kabala ya kuufifisha.
Mzee Ali Hassan Mwinyi, alitarajiwa naye atumie busara zake kuushawishi umma kuwa upinzani haustahili kuchukua nchi, badala yake akawaaminisha Watanzania kuwa upinzani hauna shida sana kwa CCM kwa kusema: “Hakuna tatizo, ile ni CCM – B, na hii yetu ni CCM – A.”
Hii ikawajengea matumaini hata baadhi ya wana-CCM wakaona si shida kuunga mkono upinzani, kwani hutokea timu A ikashindana na B na zipo nyakati timu B hushinda.
Kama hiyo haitoshi, mawaziri wakuu wawili; Lowassa na Frederick Sumaye wakahama kutoka CCM kwenda upinzani. Siku Lowassa anapokelewa upinzani, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alimwabia Lowassa hawezi kufahamu alivyosaidia jamii ya Watanzania kuondoa hofu dhidi ya upinzani. Kama hiyo haitoshi, Sumaye naye akajiunga na upinzani na akasema ameamua kujiunga kupunguza unyanyapaa dhidi ya upinzani.
Sitanii, katika muktadha huo, utaona uchaguzi wa mwaka huu ulivyo na mbinde. Wiki iliyopita niliandika makala yenye kichwa cha habari kisemacho, “M4C ya Magufuli, Lowassa na Sauli.” Nitakuwa mwizi wa fadhila nisipowashukuru wapendwa wasomaji wangu kwa mrejesho mzito mlionipa. Nimefarijika kuona nchi hii bado ina waamini safi wa dini, hasa niliponukuhu Matendo ya Mitume 26:1-31.
Mrejesho ulikuwa mkubwa na nilipata kufahamu Watanzania wanataka nini. Ni kutokana na mrejesho mkubwa wa wiki iliyopita, wiki hii nimeamua kuangalia maisha baada ya uchaguzi. Nimeamua kujadili mada hiyo kutokana na mwelekeo wa kinachoendelea katika viwanja vya kampeni. Mwezi mmoja wa mwanzo tulishuhudia mnyukano wa Richmond na afya za wagombea.
Wakati mgombea wa CHADEMA/UKAWA, Lowassa akishushiwa shutuma nzito za Richmond, yeye aliweka wazi kuwa Rais Jakaya Kikwete ndiye anawafahamu wamiliki halisi wa Richmond. Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, Tundu Lissu akafafanua kwa kina jinsi Kikwete anavyoifahamu Richmond. Kikwete naye akaibuka na kusema Lissu anazunguka na mmiliki wa Richmond. Sikuona sera mpya katika hili zaidi ya sera za kuchafuana kuomba kura za huruma.
Afya ya Lowassa nayo iligeuka mjadala. Sumaye alilifafanua kwa kina hili, akihoji mbona Mkapa alikwenda nje ya nchi kutibiwa baridi yabisi, Kikwete akaenda kutibiwa tezi dume, na baada ya muda zikasambaa taarifa kwenye mtandao kuwa mgombea wa CCM, Dk. John Magufuli ana matatizo ya moyo. Hata tukashuhudia Magufuli akilazimika kupiga push-up kuthibitisha kuwa hana tatizo la moyo.
Mambo mawili hapa yamejitokeza. Waliokuwa wakisimamia mkakati wa afya ya Lowassa, mwisho wa siku wameuweka kando mkakati huu. Wamebaini kuwa Watanzania wanasema hakuna mtu aliye kamili kiafya. Wakagundua kwamba kumbe kwa kulisema hilo, wanamwongezea wapigakura. Na wengine wakakumbushia Kikwete alivyoanguka Jangwani siku ya ufunguzi wa kampeni, lakini haikumzuia kuongoza nchi kwa miaka 10.
Si hilo tu, Magufuli amefanya vyema kupiga pushup kwa nia ya kuuthibitisha umma kuwa ana nguvu na afya yake haiko matatani. Hii imezua mjadala, wapo wanaosema viongozi wetu wanapaswa kuwa makini kabla ya kujibu kila tuhuma inayoelekezwa kwao. Wanahoji iwapo Magufuli angerushiwa dongo kuwa hajatahiriwa angesimama jukwaani akatoa kiungo chake cha uzazi kudhibtisha iwapo ametairiwa au la? Niambie.
Sitanii, kampeni za mwaka huu zimetawaliwa na matusi. Sitaki kuingia kwenye mtego ule ule, lakini kwa waliomsikiliza Mzee Yusufu Makamba wanajiuliza maswali mengi. Wanahoji wakati akimmwagia matusi Lowassa yeye anakumbuka nini kilimwachisa ualimu na kwenda kuwa Katibu Kata? Watu wanakifahamu, na wanasema kama ana ujasiri asimame hadharani na kukisema.
Sera za nini kitafanyika katika uchaguzi wa mwaka huu zimewekwa kando. Chama tawala kimepoteza muda mwingi kumtukana Lowassa au kuuaminisha umma kuwa ni mgonjwa. Kuna kibwagizo kizuri anachokitumia Magufuli cha ‘Hapa ni Kazi Tu, Tanzania ya Magufuli ni ya Viwanda.’ Niliamini mjadala ungekwenda mbali zaidi ya kutaja viwanda.
Vyama vya upinzani na wanazuoni wangechambua matamko haya yanamaanisha nini. Mfano wakati CCM wanasema watatoa elimu hadi kidato cha nne, huku Ukawa wakisema watatoa elimu hadi Chuo Kikuu bure, basi ulihitajika mjadala wa kina juu ya jinsi gani elimu hii itatolewa, elimu hii inawezaje kusaidia wananchi kujiondoa katika umaskini, kuboresha afya zao, kuimarisha pato la mtu mmoja mmoja, familia na hatimaye taifa.
Mgomeba wa Ukawa anaposimama akasema atafuta ushuru wa mazao kwa wakulima, anapaswa kuhojiwa pengo la fedha zinazopatikana sasa kupitia ushuru huo atalizibaje. Mgombea anaposema atamaliza tatizo la wahamiaji haramu, basi anapaswa kufafanua atafanyake kwa wahamiaji haramu ambao wapo tayari.
Sitanii, naufurahia ushindani wa kweli ulipo katika uchaguzi wa mwaka huu. Ni maombi yatu kuwa baada ya uchaguzi tuwe na wabunge nusu upinzani na nusu chama tawala. Siombei upinzani upate wabunge wengi kama wa CCM wa sasa au CCM iendelee kuwa na wabunge wengi kama ilivyo sasa. Tukifanya hivyo, tutarejesha tatizo. Nahitaji wawe nusu kwa nusu, kwa maana wakipitisha jambo bungeni lipite kwa masilahi ya taifa.
Nilikwenda Nairobi, Kenya wakati wa utawala wa KANU na nimekwenda Nairobi mara kadhaa sasa wakati wa utawala wa NARC na sasa chini ya Uhuru Kenyatta (Jubilee), ambaye baba yake aliasisi KANU ila sasa yeye ameingia Ikulu kupitia Muungano wa wapinzani.
Mzee Mwai Kibaki alikuwa mwana KANU, lakini alipoihama NARC akapata urais, nenda Nairobi uone walivyojenga barabara ya Tika, ugunduzi wa mafuta na sasa wanajenga reli ya umeme chini ya Uhuru Kenyatta.
Tanzania ina kila kitu, ila kwa kuendelea na mtindo wa Ilani ya Uchaguzi inasema, ni wazi hatuwezi kufika popote. Wapo wanaomshangaa Magufuli kwa kusema Tanzania ya Magufuli, lakini mimi nasema afanyacho ni sahihi.
Anajua kuwa mfumo wa chama tawala ni vigumu kuleta mabadiliko ya kweli. Akiyaweka asemayo kwenye matendo iwapo Watanzania watamchagua, tunaweza kushuhudia mabadiliko katika nchi hii.
Wasiwasi unakuwapo kuwa inawezekana Magufuli pamoja na kujitutumua mfumo wa Chama tawala hautamruhusu kufanya hayo mabadiliko anayohubiri. Ndiyo maana watu wanasema huenda wakati umefika sasa upinzani ujaribiwe angalau kwa miaka mitano, kisha tushuhudie wamepanga kuifanyia nini nchi hii.
Watu wenye mawazo haya wanasema mfanyakazi bora hustahili likizo baada kila miezi 12. Wanasema hata CCM kwa zaidi ya miaka 50 ya kufanya kazi usiku na mchana, sasa inapaswa kwenda likizo.
Sitanii, wakati hayo yakiwazwa tatizo ninalopata ni mhemko kati ya wafuasi wa CCM na vyama vya upinzani au nisema Magufuli na Lowassa. Unajua tutakuwa waongo ikiwa kuna mtu ana akili timamu anadhani mchuano wa uchaguzi wa mwaka huu kuna washindani zaidi ya Lowassa na Magufuli. Ni wazi hawa ndio watarajiwa wa urais
Kinachonisikitisha ni chuki, utafiti uliojikita kwenye uongo, uzushi na watu kununiana kama vile si Watanzania. Watanzania tumefika mahala tumesahau kuwa kuna maisha baada ya uchaguzi. Narudia, badala ya kurushiana matusi, vijembe eti Magufuli wakati anamalizia kupiga pushup aliuinua mguu wa kulia kwa shida, tujadili reli ya umeme itajengwa lini hapa Tanzania.
Tujadili uwekezaji wa boti za kasi katika ziwa Victoria zitakazopunguza gharama ya ndege kutoka Sh 160,00 kwa safari ya Mwanza – Bukoba hadi Sh 40,000 kama ilivyo kwa Zanzibar. Ikiwapo boti ya kasi inayoweza kutoka Mwanza hadi Bukoba kwa dakika 90 kwa gharama ya Sh 20,000 hii ikaimarisha maisha ya wa watu wa Bukoba.
Mwishoni mwa wiki, Simba wamewakosa Yanga, lakini kinachoendelea sasa ni ushabiki wa kutambiana usiozua chuki. Wapo watani zangu wamenitumia picha ya simba amepakatwa, lakini nikawambia tufurahi kwa pamoja maana tungewafunga tena Yanga mgegawana mbao. Kwa nia ya kujenga umoja wa kitaifa tukawaachia angalau mpate hivyo vigoli viwili. Naombea siasa ziwe sawa na utani wa mpirani.
Sitanii, nahitimisha makala hii kwa kusisitiza kuwa wagombea na wapambe wao wajadili sera na si matusi au kusambaza fitina na chuki. Wanahabari tunafanya kazi katika mazingira mgumu kwa sasa. Tunatishwa. Wapo watu wasiotaka tuseme ukweli. Hawa nawashauri wavumilie na watufurahie kwa sisi kujitokeza tukawa wasema ukweli. Hatuna sababu ya kumwambia mfalme amependeza wakati tunaona yuko uchi. Mungu ibariki Tanzania, Mungu dumisha amani na upendo sasa na baada ya uchaguzi.