Serikali ya Hispania imefanya mabadiliko ya sheria ya haki za matangazo ya uonyeshaji wa mechi za soka kupitia vituo vya runinga. Ilipofika mwaka 2016, timu zote za Hispania zilikuwa na haki sawa kwenye suala la malipo ya haki za mechi kuonyeshwa na vituo vya runinga.

Kabla ya hapo Real Madrid na Barcelona walikuwa na haki ya kujadiliana na wamiliki wa televisheni juu ya malipo ya haki za kuonyeshwa kwa mechi zao. Matokeo yake Barcelona na Real Madrid waliendelea kutajirika huku timu nyingine kama vile Cordoba na Malaga zinabakia katika hali ya umaskini, kwani wanachokipata kama malipo ya haki za mechi zao kuonyeshwa ni kidogo.

England klabu zimefaidika kupitia malipo ya haki za televisheni, hawatumii mfumo wa kinyonyaji kama ule unaotumika nchini Hispania.

Kuwapo kwa usawa katika mgawanyo wa fedha zipatikanazo kutokana na malipo ya haki za mechi kuonyeshwa kwenye runinga na vituo vingine vya mawasiliano, kutaziimarisha klabu kiuchumi, hivyo kuziwezesha kusajili wachezaji wakubwa na kuweza kwenda sambamba na upandaji wa gharama za kuendesha timu.

Chini ya mfumo huu timu zote zinaweza kujenga ushindani.

Hispania wanataka kuleta mapinduzi kwenye soka lao ili ushindani uongezeke na si kila siku Real Madrid na Barcelona wawe kwenye daraja lao la kipekee, ndani na nje ya uwanja.

Hivi karibuni kiongozi mmoja wa Simba amesikika akiongelea juu ya klabu anayoiongoza kupewa mgawo mkubwa zaidi kulinganisha na timu nyingine za mikoani.

Hispania yenye kutupatia starehe ya mechi za El Clasico kila mwaka wanataka kuondokana na mfumo huu wa mwenye kisu kikali ndiye mwenye kustahili kula nyama iliyonona, lakini sisi bado tunataka kuukumbatia mfumo uliopitwa na wakati.

Sababu inayotaka kutumika katika kuendeleza hali ya kutokuwepo kwa usawa kwenye Ligi Kuu yetu, ni ile ile ya ukongwe wa timu. Mechi nyingi za La Liga kati ya timu zinazokuwepo kwenye nafasi za katikati ya msimamo wa ligi, hazina ushindani kulinganisha na zile zinazokutanisha timu za katikati kwenye msimamo wa  Ligi Kuu England.

Kuna tofauti kubwa sana kati ya timu tatu za juu za La Liga kulinganisha na zilizobakia, tofauti ambayo huweza kuiona kama unafuatilia kwa ukaribu Ligi Kuu England.

Kama fedha za Azam zinastahili kuongezeka kwa timu za Ligi Kuu, basi ziongezeke katika hali ya usawa na si timu za Dar es Salaam zipate mgawo mkubwa zaidi kuliko timu za mikoani.

Tukijenga fikra za kuzibeba timu kongwe tutazionea timu nyingine za mikoani. Lakini tusisahau kuwa maana ya neno TFF ni Shirikisho la Soka Tanzania na limeanzishwa kwa faida ya soka la nchi nzima kwa maana ya kila wilaya na vitongoji vyake na si timu tatu au nne za mkoa mmoja tu.

Ndanda wanastahili kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu, kama ilivyo kwa Kagera Sugar na Mbeya City na timu zote hizo tatu zinatakiwa zicheze mechi zote za Ligi Kuu kwa nguvu ile ile kuanzia mechi ya kwanza mpaka ya mwisho.

Kuna maneno mitaani, kwamba Ligi Kuu yetu huwa na ushindani kwenye mechi za mzunguko wa kwanza pekee, unapoanza mzunguko wa pili wale wenye uhakika wa kubakia katika msimu ujao wanaanza kucheza ‘kirafiki’.

Kama hali iko hivyo, kwa nini timu za mikoani zisijengewe mazingira ya ushindani ili Ligi Kuu iweze kuwa na mvuto kuanzia mechi ya kwanza mpaka ya mwisho?

Hispania wanataka kuondokana na ule ushindi wa magoli 8-0 ambao Real Madrid na Barcelona wamekuwa wakiupata ndani ya misimu michache ya hivi karibuni. Simba na Yanga na wao wanatakiwa wazoeshwe kucheza na timu ambazo zimejengewa uwezo wa nje ya uwanja ili wachezaji wetu wakutane na soka la ushindani kwenye kila michuano wanayoshiriki.

Wachezaji wa timu nyingi za mikoani, wanaonyesha udhaifu tangu wakati timu zinafanya mazoezi ya viungo kabla ya kuingia vyumbani.

Tofauti kubwa inayojionyesha ni adui wa Taifa Stars ya ushindani ingawa viongozi wa klabu zetu wanashindwa kulitazama soka letu katika mapana yake. Kiongozi wa Simba anayetaka mgawo wa Azam uongezwe anapendekeza pia ongezeko hilo lilenge katika kuipendelea timu yenye umri wa miaka 80, na si zile timu kama Stand United, Ndanda FC na nyingine ambazo hazijafikisha hata umri wa miaka 10!

Kama Azam TV wataona ipo haja ya kuziongezea timu lile fungu la mwaka mzima, basi uamuzi wao uwe na faida kwa kila timu inayoshiriki kwenye Ligi Kuu na si kutoa upendeleo kwa timu za Jiji la Dar es Salaam. Timu kongwe zinao wadau wenye kuweza kuishawishi serikali ikatoa ndege kwa ajili ya kwenda Zimbabwe na Tunisia kucheza mechi za Kombe la Shirikisho.

Vipi kuhusiana na ushiriki wa African Sports, Majimaji na Toto Africans kwenye michuano mikubwa ya Afrika? Wao wanaweza kupata upendeleo maalumu kama ule wanaopewa wakongwe?

Sven van der Broeck

“Kuna kazi kubwa, lazima Tanzania ipige hatua kutoka hapa ilipo, ni  ushauri tu, ila kama tunataka mafanikio lazima tukubali kujitazama upya.”

Luc Eymael

“Nimeitazama Tanzania kuna vipaji vingi, kubwa zaidi lazima tuanze chini, ukiwa na timu bora lazima utakuwa na timu ya taifa bora, lakini umezalisha wachezaji?” anahoji kocha huyu wa Yanga.