Na Deodatus Balile, Beijing, China

Naandika makala hii wakati naanza safari ya kurejea nyumbani baada ya kuwa hapa nchini China kwa muda wa wiki mbili hivi. Nimetembelea vyuo vikuu viwili, miji minane na maonyesho ya zana za kilimo. Ziara hii imefadhiliwa na Bill & Melinda Gates Foundation, Ubalozi wa Tanzania nchini China, Ubalozi wa China nchini Tanzania na Wakfu wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF).

Ziara hii ilikuwa ziara ya mafunzo. Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki alitaka timu ya Watanzania tupatao saba tufike katika maeneo haya tushuhudie maonyesho zana za kilimo, vyuo vinavyoendesha utafiti na bidhaa zitokanazo na muhogo. Kwangu hii ni mara ya pili kuja hapa China katika suala hili la muhogo baada ya Oktoba, mwaka jana kuwa tumetembelea miji tisa, ikiwamo miji mitatu maarufu masikioni mwa Watanzania; Beijing, Guangzhou na Yiwu.

Zamu hii tumetembele miji ya Beijing, Nanning, Haikou, Pingdu, Danzhou, Qingdao, Nanjing na Lianyungang. Huko tumeshuhudia bandari, vyuo vya kilimo, vifaa vya kilimo kuanzia ulimaji, upandaji, uvunaji na uchakataji. Tumeshuhudia kwa macho yetu viwango vinavyokubalika na tukapata siri kuwa China wana upungufu mkubwa wa muhogo.

Sitanii, kimsingi China wanahitaji muhogo kutoka kwetu kwa ajili ya kuzalisha mafuta (gongo) ya kuendeshea magari. Nitafafanua zaidi taratibu wanazopitia kuzalisha mafuta ya kuendesha magari kutokana na muhogo katika makala zijazo. Leo nasema kwa ufupi tu kuwa tumeonyeshwa aina ya mbegu zinazofaa kwa muhogo.

Tumeelezwa kiwango cha wanga kinachotakiwa katika muhogo. Tumeonana na wafanyabiashara wa kati na wafanyabiashara wakubwa wanaozalisha mafuta moja kwa moja na wale wanaopeleka viwandani kuuza muhogo (makopa) wapate cha juu. Kimsingi kama kuna biashara kama nchi tunaweza kuifanya basi ni hii ya muhogo.

Sitanii, kuna dhana potofu hapo nchini ya kuanza kutafuta bei ya muhogo ni kiasi gani hata kabla ya kuwaza kulima. Nikiri mwanzo hata mimi nilikuwa na dhana kama hii. Hata hivyo, kadri nilivyotembelea maeneo mbalimbali ya hapa China nimebaini sikuwa sahihi. Ni kwa bahati mbaya viongozi wengi wa serikali waliopo katika nafasi ya kufanya uamuzi wanawaza kwa mkondo huo.

Tumezungumza na watu walio tayari kuwekeza katika biashara ya kilimo cha muhogo. Watanaka kuweka viwanda Tanzania. Muhogo unaweza kuzalisha unga, wanga na bidhaa nyingine nyingi nitakazozitaja baadaye, ila leo nigusie angalau suala la bei.

Tanzania tunapata wakati mgumu katika suala la bei kwa sababu moja tu. Unakuta shamba la muhogo katika ekari moja mkulima anavuna wastani wa tani 2 za makopa. Hapa ukiweka gharama za kulima, kuweka mbolea, kupalilia na kuvuna, ukiambiwa unapewa dola 160 kwa tani ya makopa unaruka kimanga.

Kwa aina ya kilimo chetu, mkulima anajikuta amepata wastani wa Sh 720,000 kwa ekari jambo ambalo ni hasara. Tukitumia teknolojia na mbegu stahiki mkulima atapata hadi tani 15 za makopa kutoka kwenye ekari moja. Ukipata wastani wa tani 15 za makopa kwa ekari moja, basi mkulima atajikuta anapata Sh milioni 5.4 kutokana na ekari moja hiyo hiyo.

Sitanii, najaribu kuwaza kwa sauti tu. Kahawa nani anapata Sh milioni 5.4 kwa ekari moja kwa sasa? Pamba, katani, ulezi, mahindi, ufuta… Naamini wakati umefika sasa tuache mawazo ya kufikiri kupata zaidi kabla ya kuwekeza. Tuwaze kupata baada ya kuwekeza. Naamini muhogo tukiufanya zao la biashara unalipa.

Ninachosema hapa, serikali inapaswa kujipa muda ikautangaza muhogo kama zao la biashara. Kwa kufanya hivyo, mkulima atajikuta anawajibika binafsi kuzalisha bila kusukumwa na mtu yeyote. Ni katika misingi hiyo, nimeona leo nigusie hesabu hizi kwa uchache tu, kisha mengine yataendelea niliyoyashuhudia katika ziara hii. Tukutane wiki ijayo.