Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk. Edward Hoseah, alipotamka kwamba taasisi hiyo haina uwezo wa kuwabana mapapa wa rushwa nchini, alishambuliwa.

Kauli yake ilitokana na ukweli kwamba kwa mfumo wa sheria na taratibu za uendeshaji kesi katika Taifa letu haviipi taasisi hiyo uwezo wa kupambana na wala rushwa, wahujumu uchumi na wezi wakubwa wa mali za umma. Kwa maneno mengine, Takukuru imefungwa mikono kisheria.

 

Wabunge kadhaa hawakufurahishwa na maneno ya Dk. Hoseah. Wapo waliodiriki kumtaka ajiuzulu kwa madai kwamba kama anaona hana nguvu hizo za kisheria, anasubiri nini kujiuzulu. Miongoni mwao ni Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi. Huyu ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mbeya.

 

Kwa wanaomjua Zambi, walishangaa kumsikia akimshambulia Hoseah. Wakarejea kwenye Hansard na kumkuta akiwa miongoni mwa wabunge waliotajwa bungeni kwamba ni vinara wa rushwa. Aliyewataja ni Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila. Zambi hana mamlaka ya kimaadili (moral authority) ya kuzungumzia masuala ya rushwa. Na yeye anajua hivyo na ndiyo maana hadi leo hajakanusha kilichosemwa na Kafulila.

 

Siku mbili tu baada ya Dk. Hoseah kutoa kauli yake, na akiwa ameshambuliwa mno, Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Dk. Elieza Feleshi, alitangaza kuifuta kesi ya “wazi kabisa” ya ufisadi wa aina yake katika Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) ambalo ni mali ya Watanzania wote. Waliokuwa wakimshambulia Dk. Hoseah wakakosa la kusema. Maneno yake yakawa yametimia. Kama kawaida, DPP hakutoa sababu za kufutwa kwa kesi hiyo ya uhujumu uchumi wa Sh zaidi ya bilioni 7. Hii ni ishara ya wazi kwamba hata hizo kesi nyingine zinazoendelea, mchezo unaweza kuwa huu huu.

 

Watu wamejiuliza, imekuwaje kesi yenye maelezo na vielelezo vya wazi kabisa ifutwe kirahisi namna hii? Je, ni utashi tu wa DPP? Je, ni msukumo kutoka ngazi za juu za uongozi? Je, ni kukosekana kwa vielelezo? Na kwanini ifutwe na DPP badala ya kuachwa itupwe na hakimu aliyekuwa akiisikiliza?

 

Si hayo tu au je, ni ubutu wa sheria za kuwabana wezi na wahujumu uchumi? Nani anaweza kukubali maelezo mepesi ya kufutwa kwa kesi hii? Je, kama Taifa, tuna dhamira ya kweli ya kulinda mali za umma? Nani atakuwa na imani na aina hii ya vyombo vya haki katika Taifa letu? Kwanini watuhumiwa wa wizi wa kuku wataabike magerezani, lakini watuhumiwa wa ukwapuzi wa mabilioni waachwe wakitamba mitaani?

 

Wenye akili walitambua tangu mapema kabisa kwamba kuunganishwa kwenye kesi hii kwa yule mnunuzi wa UDA, ambaye kimsingi alipaswa kuwa shahidi muhimu kabisa upande wa Jamhuri, ulikuwa ni mpango wa kuifuta kesi hii! Tumetoa mwanya kwa watu sasa kuendelea kuiba mali za umma kwa sababu hakuna kushitakiwa tena!

 

Hapa chini naomba nieleze namna sakata la UDA lilivyokuwa ili wasomaji waone kama kweli kulikuwa na sababu za msingi za kumwezesha DPP kumwachia Mwenyekiti wa Bodi ya UDA, Iddi Simba, na wenzake. Maneno haya ya chini si yangu, bali ni ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kwenye ripoti yake ya mwaka 2011/2012.

 

Anasema, Waziri Mkuu wa Tanzania alimuomba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kufanya ukaguzi Maalum juu ya taratibu zilizotumika wakati wa uuzwaji wa hisa za Shirika la UDA kwa mnunuzi wa hisa hizo na pia kufanya ukaguzi maalumu wa Menejimenti ya UDA.

 

Ukaguzi ulifanyika kutokana na maswali yaliyoibuka kwenye kikao cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Julai, 2011 kuhusiana na uuzwaji wa hisa za Serikali zilizokuwa katika Shirika la UDA na uuzwaji wa hisa ambazo zilikuwa bado hazijatengwa kwa mwekezaji.

 

Matokeo ya Ukaguzi Maalum wa UDA ni Kama Ifuatavyo:-

(a) Uuzwaji wa Hisa za UDA:

UDA likiwa ni Shirika ambalo lilitengwa kwa ajili ya ubinafsishaji (specified) chini ya usimamizi wa Shirika Hodhi la Mali za Serikali (CHC) ambalo lina jukumu la kuyaunda upya mashirika ya aina hiyo. Kwa mantiki hiyo, CHC ndiyo iliyokuwa na mamlaka ya kuidhinisha uuzaji wa hisa za UDA na siyo Bodi ya Wakurugenzi wa UDA kama ilivyofanyika. Julai, 2010, CHC iliishauri Bodi ya Wakurugenzi wa UDA kupata idhini ya Serikali kabla ya kuendelea na uuzaji wa hisa za UDA. Bodi ya Wakurugenzi wa UDA iliendelea na uuzaji wa hiza hizo bila kupata kibali cha Serikali.

 

Shirika Hodhi la Mali za Serikali (CHC) lilitoa ushauri kwa Bodi ya Wakurugenzi wa UDA kuwa njia ya wazi itumike kulingana na Sheria ya Ununuzi wa Umma ili kumpata mwekezaji bora katika Shirika la UDA. Bodi ya Wakurugenzi wa UDA ilipuuza ushauri huo na kuendelea na uuzaji huo wa hisa za UDA kwa anayedaiwa kuwa mmiliki wa UDA bila kufuata taratibu za ushindani wa zabuni kama Sheria ya Ununuzi wa Umma Na.21 ya mwaka 2004 inavyotaka.

 

● Hisa za Shirika la UDA zilithaminishwa na kuwa Sh 744.79 kwa kila hisa mwezi Oktoba, 2009. Novemba, 2010 thamani ya kila hisa ikawa Sh 656.15. Hata hivyo, katika uuzaji huo, Bodi ya Wakurugenzi ya UDA ilitoa punguzo la asilimia 60 kwa kila hisa kwa mwekezaji huyo (kwa tathmini ya bei ya hisa ya Oktoba, 2009), bila kuwepo na sababu za kufanya hivyo. Kwa hiyo kila hisa ilitakiwa kuuzwa kwa Sh 298 kutoka Sh 744.79 kwa hisa moja ambayo ilithaminishwa Oktoba 2009 na hivyo kusababisha UDA kupata hasara ya Sh bilioni 1.559.

 

Vilevile ukaguzi ulibaini kuwa Bodi ya UDA iliingia mkataba wa kumuuzia mwekezaji hisa 7,880,303 ambazo hazikugawiwa kwa bei ya Sh 145 kwa jumla ya Sh bilioni 1.142 badala ya Sh 744.79 kwa hisa kulingana na ripoti ya mshauri ambapo hisa hizo zingekuwa na thamani ya Sh bilioni 5.869 hivyo kulisababishia Shirika hasara ya Sh bilioni 4.727. Kwa kutumia bei ya hisa ya Sh 298 na 145 badala ya Sh 744.79 kwa hisa moja iliisababishia Serikali hasara ya jumla ya Sh bilioni 6.285 (Sh 1,558,694,380 + Sh 4,726,526,936).

 

● Mnunuzi (mwekezaji) alilipa kiasi cha Sh 145 kwa hisa moja na kulipa jumla ya Sh milioni 285 kinyume na thamani ya hisa ya Sh 744.79 au 656.15 kwa hisa moja. Bodi ya Wakurugenzi ya UDA ikatoa punguzo la bei ya hisa hadi kufikia Sh 145 kwa hisa moja ukilinganisha bei ya punguzo iliyokuwa imeshafanyika mwanzoni ya Sh 298 kwa hisa moja ambapo inaonekana iliongeza tena punguzo la asilimia 53.

 

(b) Ripoti ya Makadirio ya Thamani ya Hisa na Mali za UDA

Ripoti ya makadirio ya thamani ya hisa iliyoandaliwa Oktoba 30, 2009 na Novemba 15, 2010, ilionesha thamani ya mali za UDA ikiwa ni pamoja na mitambo na vifaa. Makadirio yaliyofanyika Agosti, 2009.

 

Makadirio hayo hayakuainisha Shirika ukiondoa madeni yote (Net Assets). Pia haikuonesha madeni ya Shirika ambayo ni jumla ya Sh milioni 473.241 ambayo yaliripotiwa kuwa yalishahamishiwa kwa Msajili wa Hazina. Haikuweza kufahamika ni sababu zipi zilizofanya hisa za UDA kuuzwa kwa punguzo la asilimia 60 kutoka kwenye bei ya makadirio ya thamani ya kiasi cha Sh 744.79 kwa hisa.

 

(c) Kuthibitishwa Kiasi Kilicholipwa na Mnunuzi

 

Mkataba wa kuwasilisha hisa wa Februari 11, 2011 unatamka kwamba mnunuzi (mwekezaji) atalipa jumla ya Sh bilioni 1.143 kama bei ya ununuzi ya hisa zote ambazo hazijatolewa na UDA ingawa mkataba haukuonesha akaunti ya benki ambayo malipo yangelifanyika. Mnunuzi (mwekezaji) alilipa Sh milioni 285 katika akaunti namba 0J1021393700 ya benki ya CRDB inayomilikiwa na UDA.

 

Kulikuwa hakuna malipo mengine ya ziada yaliyofanywa na mwekezaji kuhusiana na ununuzi wa hisa za UDA. Malipo haya ni sawa na asilimia 24.9 ya bei ya kuuza iliyokubaliwa.

 

Mwekezaji alidai kumlipa aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya UDA kiasi cha Sh milioni 320 kama ada ya kukubali kununua UDA katika mwaka 2009. Mwenyekiti wa Bodi alikubali (alipokea) kiasi cha Shilingi milioni 320 katika akaunti yake binafsi kutoka kwa Mwekezaji ikiwa kama ada ya ushauri alioutoa kwa Mwekezaji, ambayo ilizua mgongano wa kimaslahi.

 

(d) Utendaji Usio sahihi na Ukiukwaji wa Taratibu Katika Kuuza Hisa za UDA

Bodi ya Wakurugenzi ya UDA haikupata kibali kutoka kwa wanahisa wake kuhusiana na kuuza hisa zao hizo. Kwa mujibu wa sheria ya Mashirika ya Umma, kifungu Na. 257. Ibara ya 39(2) ya Sheria ya Mashirika ya Umma iko wazi kuwa PSRC/CHC inaweza ikaelekeza njia ya uundwaji upya wa mashirika ya umma ambayo itatekelezwa, uthamini wa mali, ualikaji wa wanunuzi wenye nia na shirika linalobinafsishwa na kubaini bei ya hisa na rasilimali zitakazouzwa.

 

Mchakato wa zabuni ya uuzaji wa hisa za UDA haukuwa wa kiushindani kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 21 ya mwaka 2004 na kama ilivyopendekezwa na Shirika Hodhi la mali za Serikali (CHC).

 

Ripoti ya uangalifu kuhusiana na Mwekezaji ilionesha kwamba mwekezaji hakukamilisha masharti yaliyowekwa na PSRC kwa ajili ya kuwekeza kwenye Shirika la UDA. Bodi ya Wakurugenzi ya UDA haikuzingatia kanuni na sheria tajwa hapo juu na iliendelea na uuzaji wa hisa hizo.

 

Hitimisho langu

Haya yote yaliyobainishwa na ofisi ya CAG yametupwa! Walioifuta kesi hawataki kuyasikia! Tanzania imekuwa pepo ya majizi. Sina shaka kwamba kuna siku mambo yatabadilika katika Tanzania yetu. Kama utawala wa sasa umeshindwa kulinda rasilimali za umma na kuwachukulia hatua stahiki watuhumiwa, sidhani udhaifu huo utaweza kujitokeza huko tuendako. Mali za umma zinapoishia kwenye mifuko ya wenyeviti wa bodi za mashirika ya umma, si tu kwamba inakera, bali ni dhambi hata kwa Mungu.

 

Fedha za umma ndizo zinazopaswa kutumiwa na Serikali kuufikishia umma huduma muhimu za kijamii. Mali hizo zinapoliwa na wachache, hiyo ina maana wengi watakosa huduma za elimu, matibabu, miundombinu na nyingine muhimu. Kila mwaka bajeti itakuwa ya sigara na pombe. Kila mwaka mapato ya ndani hayatatosha, matokeo yake tutaendelea kuwaangukia na kuwaenzi wafadhili ambao wameanza kuchoka kuliona bakuli letu la ombaomba.

 

Kwenye Katiba mpya tuanze na hili la mali za umma. Tutazame pia nguvu za Ofisi ya DPP na uhuru wake kwenye kesi ambazo hata akili isiyohitaji elimu ya cheti, unaweza kuona kabisa kuwa ni uhujumu uchumi. Mambo kama haya ndiyo yanayowafanya wakati mwingine Watanzania waone umuhimu wa kuwa na uongozi mbadala.   Wakishafika hapo, hawatakuwa na jingine, isipokuwa wenyewe kuanza kuwaadhibu wezi wa mali za umma. Inauma sana kuona kuuibia umma ni sifa ya kumfanya aliyetenda dhambi hiyo anyenyekewe. Kuna siku Watanzania watasema, “Imetosha”.